Kila wakati msimu unapoanza, au klabu zetu zinapojiandaa kwa hatua za juu za mashindano ya kimataifa ya Afrika, huibuka mijadala ya uzuri au ubaya wa jezi, na muda mwingi hutumika kulinganisha ubunifu uliozaa jezi hizo.
Mijadala hiyo huwa haizingatii mambo mughimu katika ubunifu bali uzuri hutokana tu na maoni ya mtu kulingana na marangirangi yalivyojazana kwenye nguo hizo za michezo.
Baadhi hujikita kidogo kwenye mambo ya msingi ya ubunifu wa nguo za michezo ambayo ni pamoja na historia ya timu, au kikosi kilichowahi kutikisa, nchi kupewa heshima, au ubunifu unaoirudisha jezi hiyo kwenye jamii inayoizunguka klabu.
Msimu huu ulianza bila ya mjadala mkubwa kuhusu uzuri wala ubaya wa jezi, bali umejikuta ukiingia kwenye rangi za jezi, hasa ya timu ya Yanga ambayo wiki iliyopita ilitambulisha jezi itakazotumia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Katika jezi hizo aina tatu, yaani ya nyumbani, ugenini na ile ya tatu, hakuna rangi ya njano, ambayo ndio kitambulisho kikuu cha klabu hiyo, ukiachana na rangi nyingine ya kijani na nyeusi.
SOMA ZAIDI: Lini Tutamsikia Toni Kroos wa Tanzania?
Jezi inayodhaniwa ni ya njano na inayotetewa na baadhi ya watu ni ile ya rangi ya dhahabu, ambayo si sehemu ya rangi za klabu hiyo kongwe nchini. Hakuna sababu zilizotolewa na uongozi kuhusu kukosekana kwa rangi ya njano katika sare hizo mpya kwa ajili ya michuano ya kimataifa.
Kama kawaida kunapokosekana taarifa rasmi kuhusu jambo fulani, msimamo wa viongozi unaweza kuupata kwa watu maarufu kwa jina la ‘machawa.’ Hawa hujitokeza mara moja na kuanza kutetea kilichotokea, bahati mbaya sana hujenga hoja za kushawishi mashabiki na si wapenzi wa michezo wanaoangalia vitu kwa makini na kwa undani.
Utetezi
Mmoja alichukua muda wake mwingi kujaribu kueleza umuhimu wa rangi ya dhahabu kwa nchi, kwamba inawakilisha rasilimali za ardhini kama madini ya dhahabu kana kwamba ndiyo pekee yanayoitambulisha nchi. Hoja yao ni kwamba hata bendera ya taifa ina rangi ya njano na maana yake ni dhahubu. Swali linalokuja ni dogo tu: kama rangi ya dhahabu ipo, kwa nini iliwekwa ya njano?
Mwingine akajitokeza na kuandika maelezo marefu kuwa rangi ya dhahabu ina asilimia zaidi ya themanini ya rangi ya njano, kwa hiyo ni sahihi klabu hiyo kutumia rangi ya dhahabu badala ya njano.
Mwingine, ambaye lengo lake linaonekana ni kutaka kupumbaza watu wasiwaze kwa kina zaidi, akasema rangi yoyote ni nzuri ili mradi tu matokeo ya uwanjani yanawapa furaha.
SOMA ZAIDI: Prince Dube Anapitia Ugumu wa Mbappe
Ukiwasilikiza wote huoni hata mmoja ambaye anajua sababu hasa za uongozi wa Yanga kukubaliana na uamuzi wa mbunifu, Sheria Ngowi, kutotumia rangi asilia ya klabu hiyo na ambayo pia imeelezwa kwenye katiba. Hakuna ambaye anahisi kwamba huenda Ngowi alipewa maelekezo kwamba atumie rangi hizo.
Ni utamaduni wa kawaida kwa klabu kulinda asili yake, na hasa kama asili hiyo imeelezwa kwenye katiba. Kunahitajika kazi ya ziada, utafiti na hoja za kutosha kuachana na rangi ya asili kwa sababu zozote zile.
Rangi ya timu
Moja ya vitu muhimu sana katika soka ni rangi ya nyumbani ya timu. Hiyo haibadiliki hjata iweje. Pamoja na kwamba ni rahisi kwa mwenyeji kukimbilia makabatini kuchukua jezi za rangi nyingine iwapo zitagongana na mgeni, ni nadra sana suala kama hilo kujitokeza. Kwa kawaida, mgeni hujua mwenyeji wake huvaa jezi za rangi gani na hivyo kwenda ugenini akijua kuwa amebeba jezi zinazotofautiana na mwenyeji.
Ili kulienzi hilo, Serikali ya Uingereza ilipata somo wakati klabu za nchi hiyo zilipoingia kinyemela kwenye Super League ya Ulaya, lakini mpango huo ukafelishwa na nguvu ya wananchi waliothubutu hata kukwamisha mechi baina ya Manchester United na Liverpool, wakipinga hatua ya klabu hizo kujiunga na Super League.
Serikali iliona kuwa kitendo cha kuruhusu wafanyabiashara kumiliki klabu kimewafanya wasahau hata mashabiki na kuanza kujiamulia mambo bila ya kujali. Na ndipo ilipoandaa muswada utakaoanzisha ofisi binafsi na huru ya msajili, tofauti na yule wa Chama cha Mpira (FA).
SOMA ZAIDI: Mwamuzi Omary Mdoe Anastahili Adhabu Kali
Moja ya sheria zinazotarajiwa kupitishwa katika muswada huo ni zile zinazolinda asili ya timu, ikiwa ni pamoja na rangi za jezi za nyumbani. Sheria itazitaka klabu kuhakikisha zinapata ridhaa ya mashabiki—sio wanachama pekee—kabla ya kubadilisha rangi na itatakiwa iwasilishe kwa msajili ushahidi huo.
Yapo mambo mengi katika muswada huo, lakini kwa sasa si muhimu sana kwa kuwa lililoibuka wakati huu ni hilo la kutojumuisha rangi ya asili ya timu.
Sijui kama Simba wanaweza kuachana na rangi nyekundu na kuanza kuvaa damu ya mzee eti kwa sababu damu ya mzee inatokana na sehemu kubwa ya rangi nyekundu. Simba akicheza nyumbani ni nyekundu tu na unaona kabisa jinsi jina la utani la “Wekundu wa Msimbazi” linavyoakisi asili hiyo.
Hali ni hiyohiyo kwa Real Madrid, Barcelona, Arsenal, Ajax, Juventus na klabu nyingine zote unazozijua wakati zinapocheza nyumbani. Ni lazima wavae jezi ambayo ni ya rangi ya asili. Ubunifu uje ndani ya rangi hizo na si kutafuta nyingine. Huo si ubunifu.
Katiba kukiukwa
Katika hali kama hiyo, huwezi kushangaa unapoona watu kama akina Juma Ally “Magoma” na mwenzake Georfey Mwaipopo wakiibuka mahakamani kutaka katiba ya sasa ibatilishwe na itumike ile ya mwaka 1968 kwa madai kuwa mabadiliko mengi yaliyofanyika hayakjuzingatia taratibu.
SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Wapaze Sauti kwa Pamoja Dhidi ya Upangaji wa Ratiba Unaobadilikabadilika
Ukimsikiliza sana Magoma utaona pia anapinga baadhi ya mambo yanayoonekana kuwa ni maendeleo kama kiongozi mkuu kuwa rais badala ya mwenyekiti, idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu kupunguzwa na mabadiliko mengine.
Hoja za wawili hao zinaweza kuwa si za msingi, lakini zimeibuliwa kutokana na mabadiliko makubwa ambayo wanaona yalistahili kwenda taratibu na kwa ridhaa thabiti ya wanachama.
Si ajabu watu kama hao wakaibuka leo na kusema “si mnaona, tulitahadharisha.” Na wakajenga hoja kuwa walijua itafikia muda asili ya Yanga, kuanzia rangi hadi nembo, itapotea kabisa na kuwataka wanachama na wana-Yanga kuchukua hatua kusitisha mwenendo huo.
Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa viongozi kufanya mabadiliko ya haraka ambayo yanagusa asili ya timu hiyo. Unaenda kimataifa bila ya rangi ya njano, vipi wale mashabiki walioko Misri, Algeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao watatamani japo wavae rangi moja ya asili ya Yanga ili wafurahie mechi uwanjani?
Kwa nchi kama zetu ambazo ni vigumu kuzifikisha jezi mpya uwanja wa ugenini na kuziuza kwa haraka ili mashabiki wavalie rangi hiyo mpya uwanjani kwa kuwa wengi ama watakuja na nguo zenye rangi maarufu ya timu hiyo hata kama si jezi.
Kwa hiyo, badala ya kuwabeza wanaohoji kutokuwepo kwa rangi ya njano Yanga, ni muhimu sana kwa viongozi wa klabu kuweka akilini suala la mashabiki wakati wa kufanya mabadiliko yoyote, hata kama yanalenga maendeleo.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
2 responses
Kwenye rangi nakupa HEKO ndugu Angetile.
Tuko pamoja sana. Katiba ya Yanga ibara ya 3 inabainisha rangi rasmi za klabu ya Yanga, na hata rangi za logo Kijani, Njano na Nyeusi na bendera zimetajwa kuwa Kijani na Njano.
Ni hali ya kienyeji mno isiyozingatia Katiba, wala uhalisia, desturi na inayoua utambulisho wa klabu kwa kutumia rangi zisizo rasmi kwa klabu.
Tuko pamoja.
Ila hayo ya akina Magoma nadhani usingeyaunganisha hapo. Tuongee rangi pekee.
P9
Tatizo kubwa ni Machawa kama ulivyotaja hapo juu.
Hakuna jambo baya kama kusigina katiba ambayo ndiyo nguzo ya klabu.
Nafikiri tuliangalie hili kisheria na kikanuni zaidi.