Kuna wakati kocha wa zamani wa Manchester United, Alex Fergusson, alilazimika kujiuliza maswali mengi, hadi katika mahojiano na waandishi wa habari, kuhusu mshambuliaji wake, Andy Cole, ambaye alikuwa anaelekea siku zake za mwisho za kusakata soka.
Cole alikuwa anapitia kipindi kigumu katika maisha yake ya soka, akiwa anashindwa kufunga mabao hata katika mechi ambazo zilionekana kuwa rahisi kwa mabingwa hao wa kihistoria katika soka la Uingereza.
Hali yake ilikuwa ngumu kwa kuwa mbali na kutofunga, alikuwa akigombea namba na mshambuliaji mpya wakati huo, Ruud van Nistelrooy, Ole Gunnar Solskajeer, Paul Scholes na Dwight Yorke, ambaye awali alitengeneza naye pacha kali katika safu ya ushambuliaji ya United.
Cole alishaanza kutopangwa na Fergusson, wakati mwingine akianzia benchi na msimu huo wa mwisho wa 1998-99 alimudu kufunga mabao saba tu na kuamua kuhamia Blackburn katikati ya msimu.
Aliiongoza Blackburn kutwaa Kombe la Ligi msimu wa mwaka 2002, kuiwezesha kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mara mbili ikiwa imemaliza katika nafasi sita za juu, aliifungia klabu hjiyo mabao 37 katika mechi 100 alizoichezea.
SOMA ZAIDI: Mwamuzi Omary Mdoe Anastahili Adhabu Kali
Wakati fulani Fergusson alisema, “Haiwezekani ukawa na mshambuliaji katika timu ambayo imeshinda kwa mabao saba halafu asiwemo kwenye orodha ya wafungaji.”
Ulikuwa ni wakati mgumu ambao aliushinda kwa kuhama. Alistaafu akiwa amefunga mabao 187, idadi ambayo imevukwa na Alan Shearer, Harry Keane na Wayne Rooney.
Mtihani wa Mbappe
Hivi sasa, mshambuliaji hatari wa Ufaransa, Kylien Mbappe, ana wakati mgumu kwenye klabu yake mpya ya Real Madrid, akiwa anashindwa kuziona nyavu kwenye mechi za Ligi ya Hispania, La Liga, za hivi karibuni.
Alianza kwa kishindo alipoifungia Real Madrid mabao nane katika mechi 15, lakini ameshindwa kuziona nyavu katika mechi tano zilizopita na kuibua mjadala mkubwa kuhusu juwezo wake.
Ingawa alisajiliwa bila ya kununuliwa baada ya kuichezea Paris Saint Germain (PSG) hadi mkataba wake ulipoisha, kulikuwa na matarajio makubwa kwake kuwa angewasha moto mkali kama ilivyokuwa katika klabu na timu ya taifa ya Ufaransa, lakini mambo yamekuwa tofauti.
SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Wapaze Sauti kwa Pamoja Dhidi ya Upangaji wa Ratiba Unaobadilikabadilika
Faraja kubwa kwake ni kocha Carlo Ancoletti ambaye ameonyesha hadharani kuwa upande wake na kumtetea Mbappe kuwa kipindi kigumu anachopitia ni cha kawaida kwa binadamu yeyote na kinaweza kumkuta mchezaji mwingine yeyote.
Mbappe ameshindwa kuziona nyavu hata pale Real Madrid ilipopata ushindi mkubwa labda tu pale inapotokea vigogo hao wa Ulaya wakapata penati.
Ancelotti amewatuliza mashabiki wa Real kuwa Mbappe hajayumbishwa na ugumu wa kipindi hiki na kwamba amepania kurudisha makali yake, na kuwataka kuwa nyuma yake.
Dube kikaangoni
Ndicho kipindi ambacho mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, anapitia hivi sasa baada ya kuvunja mkataba wake na Azam FC aliyoichezea kwa muda mrefu na kujiunga na mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara.
Kama ilivyokuwa kwa Mbappe, Dube naye alianza kwa nguvu katika mechi za kufungua msimu, lakini akajikuta akipoteza makali yake siku hadi siku tangu Ligi Kuu ianze.
SOMA ZAIDI: Mashabiki Taifa Stars Watoke Wapi?
Na si kwamba hapati nafasi za kufunga, la hasha. Amepata nafasi nyingi tena za wazi, ikiwemo fursa ya kuendeleza rekodi ya kuifunga Simba mfululizo, kuifunga timu yake ya zamani na nyingine kadhaa, lakini akashindwa kuzitumia baada ya ama kipa kupangua mashuti yake, au mpira kugonga mwamba.
Kosakosa hizo za mabao zimeibua mjadala mkubwa, baadhi wakisema kiwango chake kimeshuka, wengine wakisema Yanga haikufanya uchambuzi wa kina kabla ya kumsajili na mengine mengi.
Kwa kocha kama Migeul Gamondi atakuwa hajaangalia sana mshambuliaji huyo kukosa bao, bali uwezo wa mchezaji huyo kupata nafasi hizo kwa kuwa hicho pia ni kipaji kikubwa kama ilivyokuwa kwa Cole, aliyekuwa na uwezo mkubwa kuwakimbia mabeki na kujiweka katika nafasi huru.
Kama ilivyo kwa Mbappe, kocha Gamondi pia amejitokeza kumtetea, akimtaka asijisikie vibaya kwa kukosa mabao kwa kuwa ni sehemu ya mchezo.
Dube amejiunga na Yanga katika kipindi ambacho klabu hiyo inatafuta mchezaji wa kuziba nafasi ya Fiston Kalala Mayele aliyejiunga na Pyramids ya Misri baada ya kuwa na misimu miwili mizuri katika klabu hiyo ya Jangwani.
SOMA ZAIDI: Tumeacha Mapinduzi Kwenye Klabu, Sasa Tunayumbisha Seckretarieti
Mayele aliondoka na taji la mfungaji bora, akifunga mabao 17. Kabla ya msimu huo alifunga mabaop 16 na kuwa wa pili nyuma ya George Mpepo.
Haja ya kupata mbadala wa Mayele imejumuisha pia usajili wa mshambuliaji wa zamani wa Simba, Jean Baleke, ambaye matokeo yake ya mpira ndani ya boksi ni hatari ama “fox in the box”.
Lakini pia yumo Kennedy Musonda, ambaye alishirikiana vizuri na Mayele na pia yupo Clement Mzize, ambaye ameonekana kuwa na athari kubwa kwa wapinzani kila anapopata nafasi.
Mawenge
Ni wazi, mazingira hayo yanampa mawenge kocha Gamondi na mawenge hayo moja kwa moja yanamuathiri mchezaji ambaye klabu na mashabiki wana matarajio makubwa kwake.
Mara kadhaa Gamond amempa Dube nafasi ya kuanza na kutokana na uwepo wa washambuliaji wengine niliowataja awali, hawezi kumruhusu Dube atumie muda mwingi uwanjani wakati klabu inahaha kutafuta ushindi.
SOMA ZAIDI: Serikali Ianze Kutoa Ruzuku kwa Vyama Teule vya Michezo
Ni lazima atamwita nje na kumuingiza mmoja kati ya Mzize, Musonda au Baleke katika kipindi cha pili. Na usisahau kuwa kipindi cha pili ndicho ambacho Yanga huingia na nguvu kubwa inayolazimisha wapinzani kujikuta wakiruhusu mabao.
Kwa hiyo, Dube hupishana na mafanikio. Hupishana na wakati mzuri kwa timu yake, hupishana na nguvu kubwa ya kipindi cha pili. Anakuwa hanufaiki na nguvu ya Yanga katika kipindi cha pili.
Na mechi chache alizoingizwa baadaye alikuta tayari timu iko katika mazingira magumu, kama ilivyokuwa katika mechi dhidi ya Tabora United ambayo pia alipoteza nafasi ya wazi.
Kwa hiyo, kama inavyotokea kwa wachezaji wengi nyota duniani, Dube hana budi kuwa imara kiakili ili aweze kukivuka kipindi hiki kigumu katika maisha yake ya soka kama alivyomudu kukivuka kipindi cha majeraha wakati akiwa Azam.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.