The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sintofahamu Mahakamani Polisi Wakizuia Watu Kuingia na Simu Kwenye Kesi ya Mbowe

Wadau wanaitaka Mahakama kufuata nyayo za nchi jirani kwa kuruhusu baadhi ya kesi kurushwa mubashara. 

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Sintofahamu imejitokeza leo Septemba 16, 2021, katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi jijini hapa, baada ya polisi kuamrisha kwamba watu wachache tu ndiyo wataruhusiwa kuingia kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu na kwamba hao watakaoingia watalazimika kuacha simu zao za mkononi nje ya mahakama.

Mbowe na wenzake watatu, ambao ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa, na Mohamed Abdillahi Ling’wenya, wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama ya kutenda kosa na kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya ugaidi. Kesi hiyo kwa sasa ipo katika ngazi ya usikilizwaji wa mashahidi, huku mashahidi wanaotoa ushuhuda wao kwa sasa ni wale wa upande wa Serikali.

Tangu jana, Septemba 15, 2021, ambapo shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri Kamanda wa Polisi Kinondoni Ramadhan Kingai ameanza kutoa ushahidi wake, umma wa Watanzania waliweza kufuatilia kwa karibu kilichokuwa kinatokea mahakamani hapo kupitia taarifa za papo kwa hapo ambazo baadhi ya wafuasi na wanachama wa CHADEMA waliopo mahakamani wamekuwa wakituma kwenye mitandao ya kijamii, hususan Twitter.

Leo, kesi ya akina Mbowe ililetwa tena mahakamani ili Kingai aendelee kutoa ushahidi wake lakini tofauti na jana, leo maafisa kutoka Jeshi la Polisi waliweka ukomo wa watu wanaopaswa kuingia kusikiliza kesi hiyo na kutaka simu ziachwe nje, huku wakiwaambia wafuasi wa CHADEMA kwamba, “Jana [Sept 15] mmefanya ujinga sana” bila ya kufafanua, watu waliokuwa karibu na eneo hilo wamedai.

Kufuatia hatua hii, viongozi wa CHADEMA waliamua kugomea kesi hiyo kwa muda na kulitoa jopo la mawakili linalomtetea Mbowe na wenzake nje ya Mahakama, wakisema hakuna sheria inayokataza watu kuingia ndani ya Mahakama bila simu. Makamo Mwenyekiti wa CHADEMA (Tanzania Bara) Tundu Lissu na Naibu Katibu Mkuu wa chama (Tanzania Bara) Benson Kigaila walifanya kikao kupitia mtandao wa WhatsApp na kuamua kwamba kama wafuasi wa CHADEMA hawataruhusiwa kuingia na simu mahakamani basi wao wangegomea kesi hiyo.

Hata hivyo, kesi hiyo iliweza kuendelea baada ya Jaji Mustapha Siyani, anayesimamia kesi hiyo, kuamrisha watu waingie na simu zao, na hivyo Kingai aliendelea kutoa ushahidi wake, huku wakili Peter Kibatala, moja kati ya mawakili wanaomtetea Mbowe, akiendelea kumuhoji. Kesi hiyo ilipaswa isikilizwe saa tatu kamili asubuhi lakini kutokana na sintofahamu hiyo iliweza kuanza majira ya saa saba mchana.

Sheria za Tanzania zinaruhusu uwepo ya Mahakama ya Wazi inayoruhusu mtu yoyote kuhudhuria, ukiacha kesi zinazohusu watoto au katika matukio ya kudhalilisha kama vile ubakaji. Mpaka sasa, nchini Tanzania hakuna utaratibu wa kurusha matukio yanayoendelea mahakamani mubashara kwa baadhi ya kesi zenye maslahi ya umma. Waandishi huruhusiwa kupiga picha ndani ya mahakama kabla kesi haijaanza na kutoa taarifa ya kile kilichotokea kwa maandishi.

Hii ni tofauti na nchi jirani na Tanzania kama vile Kenya ambao kesi kurushwa mubashara kwenye vyombo vya habari imekuwa ni kitu cha kawaida. Hivi karibuni, vyombo vya habari nchini humo vilirusha mubashara kesi mashuhuri ya Building Bridge Initiative (BBI). Kwa Uganda, baada ya mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulani kuwekwa kizuizini kwa muda akishutumiwa kufanya uhaini, kesi yake ilipoanza kusikilizwa ilitangazwa mubashara pia. 

Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufanyaji wa kazi zake. Hii inajumuisha uwekaji wa maamuzi ya kesi mtandaoni ambapo mtu yoyote anaweza kufuatilia kesi hizo kupitia tovuti ya Tanzli, ambalo ni jukwa la mahakama. Mahakama ya Tanzania pia imeanzisha mahakama zinazotembea na pia kuendesha baadhi ya mashauri kwa njia ya mtandao.

Kufuatia hatua hizi, wadau wamekuwa wakiisihi Mahakama ya Tanzania kufikiria kuruhusu baadhi ya kesi zenye maslahi mapana ya umma kurushwa mubashara. Wadau hawa wamekuwa wakibainisha kwamba hatua hii siyo tu itaongeza imani ya wananchi juu ya Mahakama, lakini pia itawasogeza wale ambao ni waoga kutumia Mahakama katika kudai haki zao na kuanza kufanya hivyo.

“Haki lazima ifanyike na ionekane imefanyika. Haki haiwezi kufanyika gizani na ikaonekana imefanyika,” Tundu Lissu aliandika kwenye ukurusa wake wa Twitter kufuatia sintofahamu hiyo iliyodumu kwa takribani masaa manne. “Ni haki yetu kujua. Mahakama ya gizani sio mahakama huru au ya haki. Tunataka mahakama huru [na] ya haki,” alisema Lissu kwenye andiko jengine la Twitter.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *