Dodoma. Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Rebecca Ndaki ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalumu kwamba tatito la ulawiti na ubakaji ni kubwa sana mkoani hapa, akibainisha kwamba kati ya Januari na Juni mwaka huu wa 2021 jumla ya watoto 128 wamekumbana na vitendo vya ulawiti na ubakaji, kati ya hawa wanawake wakiwa ni 116 huku na wanaume ni 12.
Ndaki anasema kwamba wastani kwa siku watoto wa kike wanaofanyiwa vitendo hivyo ni asilimia 3.8 huku wa kiume ikiwa ni asilimia 0.4 kwa siku. Akizungumzia sababu zinazochochea vitendo hivyo, Ndaki analaumu utandawazi, akisema unachangia kushamiri kwa matukio hayo.
“Kuna hiyo mitandao ya kijamii inayowahemusha watu ambao wako kwenye rika la ukuaji,” afisa huyo ameieleza The Chanzo ilipomtembelea ofisini kwake hivi karibuni. “Unaweza kukuta mtu anatumia picha kwa ajili ya kufanyia vitendo hivyo watoto.”
Ndaki anawasihi wazazi kuwa karibu na watoto wao, kuongea na watoto na kuwapa elimu ambayo itawasaidia kuwaepusha kukumbana na vitendo hivyo vya ukatili. Anasema: “Kuna ile unamuambia usiruhusu mtu akuguse sehemu zako za mwilii ili hata ikitokea changamoto mtoto atoe taarifa.”
Ushuhuda
Nyemo Matonya,* mzaliwa wa Bahi, Dodoma, ni moja kati ya watoto wengi ambao ni wahanga wa vitendo vya ulawiti mkoani hapa. Nyemo, 8, alilawitiwa akiwa na umri wa miaka sita tu, kipindi hicho akiwa anasoma darasa la awali. Wakati anafanyiwa kitendo hicho alikuwa akiishi na shangazi yake ambaye ndiye alikuwa akimlea wakati huo.
Khadija Sabaya, 56, shangazi wa Nyemo, anasema kwamba mtu aliyefanya kitendo hicho alimrubuni Nyemo kwa pipi, na kumpeleka nyumba ya jirani na kumbaka. Watu walipomuona Nyemo anatoka ndani ya hiyo nyumba huku miguu akiwa ameiachia, ndipo walipomwita Khadija, wakiwaza nini kinaweza kuwa kimemkuta mpaka akashindwa kutembea.
Alipoulizwa, baada ya kugoma kwa muda, Nyemo alisema kuna mtu kamuwekea uume wake kwenye makalio, huku akiwa amewuwekea shati mdomoni, na kumtishia kwamba asiseme jambo hilo kwa mtu yoyote. Baada ya Nyemo kupelekwa hospitali, ikagundulika kwamba amelawitiwa.
“Ingawaje mtu aliyemfanyia Nyemo kitendo hiki alihukumiwa kwenda jela miaka 30, mtu huyo alitumikia kifungo hicho kwa mwaka mmoja tu kabla ya kurudi mtaani,” Khadija analalamika, akiongeza kwamba hali hii ya kutokuwepo kwa uwajibishwaji wa watu wanaobainika kufanya vitendo hivi kunaweza kukwamisha juhudi za kuvikomesha. “Kesi ilituzungusha sana, lakini mwisho wa siku mtu anahukumiwa, halafu tunamuona mtaani.”
Tunapokea kesi nyingi
Nyemo si mhanga pekee wa vitendo vya ulawiti mkoani hapa. Kwa mujiba wa Inspekta wa Polisi Dawati la Jinsia Dodoma Theresia Mdendemi, kwa wiki dawati hilo hupokea kesi tatu hadi nne zinazohusiana na ulawiti na ubakaji.
“Wiki nyengine mnaweza msipokee kabisa na wiki nyengine mkapokea nyingi nyingi,” Inspekta Mdemeni anasema. “Mara nyingi kesi hizi wanaleta watu wa pembeni sio watu wa humo humo ndani [ya familia] kwa sababu watu wa ndani mara nyingi huwa wanataka kumaliza [haya mambo] kifamilia.”
Wiliam Mtwazi ni mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambaye anasema hakuna njia ya moja kwa moja ambayo inaweza kupendekezwa ikawa suluhisho la vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto wadogo
“[LHRC] tumekuwa tukipendekeza njia nyingi ambazo tunaamini zikitumika zinaweza kuwa suluhisho, si kwa mwaka huu, mwaka jana wala mwaka juzi,” anasema. “Hivi vitendo vimekuwa vikongongezeka [hapa Dodoma] na tunaviona kadiri tunavyoendelea kutoa ripoti zetu kwamba badala ya kupungua vitendo vinazidi kuongezeka.”
Mtwazi anataja makuzi mazuri kama moja wapo wa njia zinazoweza kutumika kukomesha vitendo hivi. Mbali na hilo, mwanasheria huyo pia anashauri watu wanaobainika kutenda makosa ya aina hizo kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
*Siyo jina lake halisi
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jaquelinevictor88@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.