The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Selimundu: Wazazi Walia na Gharama za Matibabu

Mbali na gharama za matibabu kuwa juu, wazazi wenye watoto wenye selimundu pia wanalalamikia uchache wa wataalamu pamoja na ukosefu wa baadhi ya vipimo.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mratibu wa Huduma za Selimundu kutoka Wizara ya Afya Dk Asteria Mpoto amesema kwamba hali ya ugonjwa huo wa kurithi hapa nchini bado ni changamoto, akibainisha kwamba takribani watoto 11,000 wenye ugonjwa huo wa kupungukiwa damu mwilini huzaliwa kila mwaka nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Serikali, mgonjwa wa selimundu huwa hana damu ya kutosha kwa sababu ya seli zake za mwili sio imara kiasi cha kubeba hewa ya oxygen kwenda sehemu mbalimbali za mwili wa binadamu. IIi mtoto aweze kupata ugonjwa huu ni lazima wazazi wawe na vimelea vya ugonjwa huo.

Wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake hivi karibuni, Dk Mpoto ameeleza kwamba kwa sasa Tanzania ina jumla ya wagonjwa 200,000 wa selimundu, huku Watanzania kati ya asilimia 15 na 20 wakiwa wamegundulika na vinasaba vya ugonjwa huo ambao dalili zake hazionekani mpaka mtoto afikishe umri wa miezi minne.

Moja kati ya malamiko mengi ambayo wazazi wanaouguza watoto wenye selimundu wamekuwa wakilalamikia ni ukosefu wa huduma bora kwa watoto wao hao pale wanapokwenda kuwatafutia matibabu hospitalini, hususani zile za umma. Baadhi ya malalamiko haya ni gharama za matibabu kuwa juu; uchache wa wataalamu; pamoja na ukosefu wa baadhi ya vipimo.

Zuhura Hassan ni mkazi wa hapa jijini Dodoma anayeuguza mtoto mwenye ugonjwa huu wa selimundu. Anaieleza The Chanzo kwamba changamoto ya msingi kwake ni gharama za matibabu, akisema ziko juu kitu kinachompa shida kwani ugonjwa wa mtoto wake huyo ni wa kudumu.

“Changamoto kubwa ni pesa kwa sasabu wagonjwa wa selimundu wanahitaji matunzo sana,” anaeleza Zuhura ambaye mtoto wake mwenye umri wa miaka sita aligundulika akiwa na ugonjwa huo akiwa na miezi mitano. “Ugonjwa wowote ukiwa ni wa kudumu unahangaika kuhakikisha yule mgonjwa wako haumwi mara kwa mara, kwa sababu unaambiwa mwili wake yeye ni dhaifu anaweza kupata magonjwa yoyote mara kwa mara. Kwa hiyo, unajitahidi kwa kadiri ya uwezo wako kuhakikisha hapati yale magonjwa. Sasa, kujitahidi kwake ni kuhakikisha unapata madawa  ambayo yatamsaidia kuishi kama watoto wengine.”

Fatuma Jafari Kasongo, mkazi wa Mkuranga, Mkoa wa Pwani, ni mama mwengine mwenye mtoto mwenye selimundu. Fatuma aligundua binti yake ana tatizo hilo alipofikisha umri wa miaka minne. Kwa sasa, binti huyo ana umri wa miaka 12 na anaendelea kupambana na ugonjwa huo.

Akiongea na The Chanzo kwa njia ya simu kuhusu changamoto anazokabiliana nazo, Fatuma anasema: “Hospitali nyingi haziufahamu vizuri ugonjwa wa selimundu. Yaani unampeleka mtoto hospitali unakutana na daktari haijui [selimundu] kabisa. Kwa hiyo, hajui hata mtoto huduma ya kwanza anamfanyaje, [yaani] ampe nini [na] amuandikie vipimo gani! [Madaktari] wengi unakuta hawajui. Hiyo inaweza kupelekea mtoto kupoteza maisha kwa haraka.”

Lakini wakati wa mahojiano na The Chanzo jijini hapa, Dk Mpoto amesema kwamba wakati baadhi ya changamoto bado zipo, hali ya sasa ya kukabiliana na ugonjwa wa selimundu nchini Tanzania imeimarika, tofauti na ilivyokuwa hapo zamani.

“Tulikotoka na tulipo sasa [ni tofauti],” anasema Dk Mpoto. “Tulikuwa na wataalam wachache – yaani specialists waliobobea na ugonjwa huo – lakini sasa hivi karibia kwenye hospitali zetu za Rufaa za Mikoa kuna wataalam. Wapo kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa selimundu na bado wataalam wengine wako vyuoni wanazalishwa kwa ajili ya kuja kuendelea kutibu.”

Dk Mpoto amebainisha kwamba hata gharama za matibatu zimezidi kuwa nafuu, huku akitaja hatua ya Serikali kuingiza nchini dawa ambayo ilikuwa haipo Tanzania kama kielelezo cha juhudi za Serikali za kukabiliana na ugonjwa wa selimundu.

“[Dawa hii] ilikuwa inapatikana kwa shida [nchini] lakini sasa hivi hiyo dawa Serikali ilihakikisha kwamba inapatikana,” anaongeza Dk Mpoto. “[Dawa yenyewe] inaitwa Hydroxyurea (HU) na kila mgonjwa mwenye bima ya afya anapata dawa hizi bila shaka yeyote. Tulipotoka na sasa kwa kweli  kwa matibabu tunamshukuru Mungu.’’

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts