Dar es Salaam. Shirika linalotetea haki za binadamu la Human Rights Watch limemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kutunga sheria ambayo itabatilisha sera inayokataza wanafunzi wa kike waliopata ujauzito wakiwa masomoni kutokuendelea na masomo kupitia mfumo rasmi wa elimu nchini.
Tofauti na Zanzibar ambako binti aliyepata ujauzito akiwa masomoni anaruhusiwa kuendelea na masomo kwenye mfumo rasmi wa elimu, hali ni tofauti kwa Tanzania Bara ambako binti huyo anapaswa kuendelea na masomo kwa mfumo mbadala, unaojulikana kwa kitaalamu kama Alternative Education athways (AEPs).
Kwenye taarifa yao iliyotolewa Jumatano, Oktoba 6, 2021, Human Rights Watch imesema kwamba hatua hiyo ya Serikali ya kuwazuia wasichana waliopata ujauzito wakiwa masomoni kuendelea na masomo kupitia mfumo rasmi umewanyima maelfu ya wasichana haki yao ya kupata elimu, huku ikizishutumu shule za umma za Tanzania Bara kuwafanyia vipimo vya ujauzito vya lazima wasichana wanaoshukiwa kuwa na ujauzito na kuwafukuza wale wanaogundulika kuwa na ujauzito.
“Wasichana wa Tanzania [Bara] wanasumbuka kwa sababu Serikali inaweka mkazo kwenye sera holela ambayo inasitisha elimu yao, inawanyanyasa, inawatenga na kuwaharibia maisha yao ya baadae,” ripoti hiyo inamnukuu Mtafiti Mwandamizi wa Haki za Watoto kutoka Human Rights Watch Elin Martinez akisema. “Ni lazima Serikali ikomeshe sera hii isiyojali utu na kuwaruhusu wanafuzi wajawazito na wale ambao wameshajifungua warudi shule.”
Alipotafutwa na The Chanzo ili aweze kueleza kwamba Serikali imepokea taarifa hii ya Human Rights Watch na kwamba anadhani mapendekezo ya Human Rights Watch yanaweza kutekelezwa nchini, Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa alikuwa akikata simu kila alipokuwa anapigiwa na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya WhatsAPP hakuweza kujibu.
Human Rights Watch inasema iliongea na wasichana 31 wenye umri kati ya miaka 16 na 24 kati ya kipindi cha mwezi Julai na Agosti, 2021. Wasichana wote waliohojiwa walifukuzwa au waligoma kuendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari kwa sababu ya ujauzito kati ya kipindi cha mwaka 2013 na 2021.
Kwa mujibu wa Human Rights Watch, wakuu wa shule na walimu ni wasimamizi na watekelezaji wakuu wa sera ya Serikali ya kuwazuia wasichana waliopata ujauzito kuendelea na masomo wenye mfumo rasmi. Utekelezaji wa sera hii mara nyingi unafanyika katika mazingira yanayowadhalilisha na kuwanyanyapaa wasichana waliopata ujauzito wakiwa masomoni.
Kinyume na matarajio ya Serikali kwamba wasichana wanaozuiwa kuendelea na masomo kupitia mfumo rasmi watafanya hivyo kupitia mfumo mbadala, au Alternative Education Pathways (AEPs), wasichana wengi wanaofukuzwa shule hujikuta wanalazimika kujiunga na mafunzo yasiyo rasmi ya ushonaji na kazi nyengine zisizo rasmi, utafiti wa Human Rights Watch unabainisha.
“Tanzania inatofautiana na nchi zingine za Afrika zilizoko katika ukanda wa Jangwa la Sahara ambazo zimeweka sheria, sera, na mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa haki ya elimu kwa wasichana wajawazito na wale waliojifungua,” taarifa ya Human Rights Watch inamnukuu Martinez akisema. “Rais [Samia] ana wajibu wa kukomesha katazo la wasichana waliopata mimba au waliojifungua wakati wakiwa masomoni kuendelea na masomo kupitia mfumo rasmi wa elimu wa nchi. [Rais] anawajibu wa kuhakikisha kwamba kila mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu nchini [Tanzania].”
Kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazotawala sekta ya elimu nchini Tanzania, uongozi wa shule unaruhusiwa kumfukuza mwanafunzi endapo kama amebainika “ametenda kosa kinyume na maadili” au endapo kama “ameoa au ameolewa.”
Wakati sheria na kanuni hizi zilikuwepo siku nyingi, utekelezaji wake ulishamiri kuanzia Juni 22, 2017, pale Rais wa awamu ya tano Hayati John Magufuli aliposema kwamba chini ya utawala wake hataki kuona msichana aliyepata mimba anaruhusiwa kuendelea na masomo. Mpaka sasa, Rais Samia hajatoa tamko lolote kuhusiana na suala hilo tangu aapishwe kuwa Rais mnamo Machi 19, 2021.
Tanzania inatajwa kama mojawapo ya nchi zenye viwango vikubwa vya mimba za utotoni, huku asilimia 22 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 20 na 24 wakitajwa kujifungua wakiwa na umri wa miaka 18, kwa mujibu wa Human Rights Watch. Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na Guttmacher Institute, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya afya ya uzazi, jumla ya wasichana 360,000 wenye umri kati ya miaka 15 na 19 hujifungua kila mwaka nchini Tanzania.
Lukelo Francis ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni lukelo@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.