The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Angela Merkel: Sauti Iliyovuma, Kuheshimiwa Barani Ulaya na Kwengineko

Kansela huyo wa kwanza mwanamke nchini Ujerumani anategemewa kuachia ngazi mwisho mwa mwaka huu baada ya kulitumikia taifa hilo la Ulaya kwa kipindi cha miaka 16.

subscribe to our newsletter!

Angela Dorothea Merkel ni  miongoni mwa viongozi wa dunia ambao wamegonga vichwa vya habari. Bibi huyu sasa anakaribia kuondoka kwenye jukwaa la kisiasa, kwa maneno yake mwenyewe ameamua kustaafu. Je, uongozi wake ulikuwa wa aina gani na anaacha alama gani katika siasa za ndani nchini mwake, Ulaya na hata kimataifa ?

Katika kipindi cha miaka 16 ya utawala wake, Kansela wa Ujerumani  Merkel amekuwa na uzito mkubwa kidiplomasia. Kwa mfano, katika Umoja wa Ulaya (EU), si kiongozi aliyekuwa akikurupuka katika kuchukua maamuzi, bali alisikiliza na baadae kuja na mtazamo wake ambao kwa sehemu kubwa ulisaidia kutuliza mivutano na jazba na hata kama suluhisho halikupatikana, alifungua njia ya kuweza kuelewana. 

Angela Merkel akiapa kuwa Waziri wa Wanawake na Vijana, January 18, 1991| Picha na Bundesregierung

Mfano wa mafanikio yake katika siasa za ndani ambazo zimekuwa na mafungamano na Ulaya ni suala la wakimbizi kutoka nchini Syria waliovikimbia vita vilivyoanza Machi 2011 nchini mwao.

Kwa hatua yake ya kuwapokea maelfu ya wakimbizi kutoka taifa hilo la Mashariki ya Kati 2015, Merkel alikuwa amechukua maamuzi muhimu kabisa kuwahi kuonekana katika kipindi chake cha uongozi. Licha ya kuwepo na mabishano makali baadhi ya wakati juu ya  sera  ya wakimbizi ndani ya  Serikali yake ya mseto kati ya  chama chake cha kihafidhina Christian Democratic Union(CDU) na kile cha  Social Democratic (SPD), Merkel alisimama kidete na kuweza kulivusha jahazi. Wengine wamemuona kuwa mhafidhina aliyewajali walio tabaka la chini na sio matajiri.

Mdhibiti wa Trump

Kimataifa  alisimama kidete kupingana na sera za Rais wa Marekani Donald Trump bila kutetereka, ukiwemo msimamo wa Trump kuelekea Jumuiya ya kujihami ya NATO. Vile vile, pamoja na kuzikosoa Urusi na China, hasa katika suala la haki za binadamu na utawala bora, Merkel alipendelea zaidi kuendelea kujongeleana na mataifa hayo mawili, licha ya wapinzani wake kudai akizingatia zaidi masilahi ya kiuchumi.

Merkel aliutetea msimamo wake, huku akizungumzia umuhimu wa China kiuchumi  na ule wa Urusi katika kupunguza mivutano barani Ulaya, hasa baada ya Urusi kulitwaa jimbo la Ukraine la Crimea mnamo mwaka 2014 na kuliingiza katika mamlaka yake.

Angela Markel katika mazungumzo ya kuagana na Rais Xi Jinping wa China, Oktoba 13,2021| Picha Bundesregierung

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, alijishughulisha sana na suala la kushajiisha vitega uchumi  vya Ujerumani barani Afrika na kujaribu kuimarisha uhusiano na bara hilo, lakini janga la UVIKO-19 lilizorotesha kupatikana mafanikio makubwa.

Kinyang’anyiro cha kumrithi

Tangu alipotangaza kwamba hatogombea tena uchaguzi wa Septemba 2021 hali ndani ya  chama chake cha CDU na mshirika wake wa jadi CSU, haikuwa shwari. Kuliibuka mvutano wa chini kwa chini katika kumpata mtu atakayekuwa mgombea wa kuwaongoza katika uchaguzi. 

Katika kinyang’anyiro baina ya  Waziri Mkuu wa  mkoa mkubwa kabisa Ujerumani wa North Rhine Westfalia Armin Laschet (CDU) na Waziri Mkuu mwenzake wa mkoa tajiri wa Bavaria Markus Soder, hatimaye kutokana na ushawishi na nguvu za wajumbe wa CDU, Laschet akachaguliwa kuwa mgombea.

Tayari kulionekana upinzani huku wengine wakihoji Soder alikuwa mgombea bora, kutokana na haiba na umri mdogo kuliko mpinzani wake, jambo ambalo liliashiria  wakitaka mabadiliko na hasa vijana.

Utafiti wa maoni ya wapiga kura ulionesha kuanza kuanguka taratibu kwa uwezekano wa Laschet kushinda na kuwa Kansela atakayemrithi Merkel na nafasi kubwa mgombea wa SPD Olaf Scholz. Scholz , Meya wa zamani wa jiji la Hamburg aliyewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa SPD, ni Waziri wa Fedha katika Serikali ya muungano  kati ya chama chake na CDU chini ya Merkel, inayomaliza muda wake.

Angela Markel aliposhinda uchaguzi mwaka 2005| Picha bundesregierung

Scholz alifanikiwa sio tu kumpiku Laschet lakini hata mgombea Ukansela wa Chama cha Kijani Annalena Baerbock ambaye wakati mmoja akiongoza katika utafiti wa kura  za maoni ya wapiga kura na kutajwa kuwa na uwezekano wa  kumrithi Merkel na kuashiria huenda Ujerumani ingeongozwa tena na Kansela mwanamke, wa pili katika historia yake.

Hilo halikuwa na sasa inaonekana kana kwamba taifa hili kubwa kiuchumi barani Ulaya huenda likaongozwa na chama cha SPD kwa kuwa na Serikali ya muungano ya vyama vitatu SPD, Free Democrats (FDP) na  chama cha Kijani, huku Scholz akiwa Kansela. Ni matumaini ya Wajerumani kwamba hilo litafanikiwa, kutokana na kuanza rasmi kwa mazungumzo baina ya vyama hivyo.

Azma ya Laschet kuwa Kansela ni ndoto iliotoweka  na binafsi anakabiliwa na vuguvugu ndani ya chama chake CDU kumtaka  ajiuzulu. Bado hilo halijatokea lakini kuna dalili ya kwamba  hatokuwa na chaguo jengine, ili kukipa chama mwelekeo mpya hasa kikiwa upinzani na uongozi mpya. 

Maoni ya wana CDU wengi ni kuwa chama chao kinahitaji mabadiliko ya kizazi katika ngazi ya juu ya uongozi. Merkel anasubiri Serikali mpya kuundwa ili afunge rasmi virago na kumuachia mrithi wake uongozi wa taifa.

SPD, FDP na Kijani, vimeingia kwenye mazungumzo vikiwa na misimamo tafauti katika baadhi ya masuala kama si mengi ya masuala. Hata hivyo, viongozi wao wamezungumzia haja ya maridhiano ili kuweka mbele masilahi ya taifa. 

Ingawa kiongozi wa FDP Christian Lindner anatajwa kuwa na msimamo mkali linapokuja suala la matumizi ya fedha, akipendelea kwa mfano kutoongezewa kodi kwa matajiri na makampuni makubwa, kuna uwezekano wa kupatikana maafikiano, ikiwa vyama vingine vipate pia ridhaa ya FDP katika mambo vinavyoyapigania. 

Lindner anayefikiriwa  ndiye atakayekuwa waziri ajaye wa fedha pia amekuwa akiwatia hofu baadhi ya  viongozi wa Umoja wa Ulaya kutokana  na kupinga kwake muelekeo wa Umoja huo panapohusika na sera yake ya fedha, lakini  wachambuzi wanahisi atalazimika kulainisha msimamo wake.

Sababu kubwa ni kwamba hautokuwa na msimamo wa Lindner au FDP utakaokuwa dira ya Ujerumani mbele ya Umoja huo mjini Brussels bali ni msimamo wa serikali ya Ujerumani pamoja, yaani uamuzi wa pamoja wa   serikali ya mseto. 

Ujerumani itakuwa na sauti ile ile bila Merkel?

Kwa hakika, inatarajiwa Ujerumani itaendelea kuwa na sauti katika Umoja wa Ulaya, ingawa  kuwa na  haiba ile ile  ya Merkel ni jambo litakalochukuwa muda. Scholza anatajwa kuwa mtu wa busara na kama Merkel si wa malumbano, jambo ambalo liliwarahisishia kushirikiana pamoja katika  kipindi cha miaka minne iliopita.

Merkel anaacha alama ya kisiasa ambayo itakumbukwa kwa muda mrefu ndani  ya Ujerumani, Ulaya na nje ya bara hili. Alikuwa na mtindo wake wa kipekee wa kukabiliana na changamoto. 

Angela Markel na Rais wa Italia Sergio Mattarella mjini Berlin Oktoba 12, 2021 | Picha na Bundesregierung

Wajerumani wanasubiri kuona ikiwa SPD, Kijani na FDP hatimaye vitafikia makubaliano  na kuunda Serikali ya muungano. Kufanikiwa kwao kutaandika historia kwani itakuwa ni mara ya kwanza ambapo inaundwa Serikali ya vyama vitatu. Serikali za muungano zilizopita zilikuwa ni za vyama viwili pekee. 

Palishaundwa Serikali ya aina hiyo kati ya CDU na SPD mara mbili ikiwemo hii inayomaliza muda wake. Ya kwanza iliojulikana pia kama muungano wa vyama vikubwa iliongozwa na Kansela  Konrad Adenauer wa CDU na Kiongozi wa SPD Willy Brandt. CDU na FDP waliunda Serikali  mara mbili, SPD na Kijani mara mara moja. 

Kwa upande wake, Merkel akifikisha rekodi ya miaka 16 Iliowekwa na Kansela Helmut Kohl na anaweka historia ya kuwa Kansela wa kwanza mwanamke katika historia ya Ujerumani.

Kansela mtarajiwa Scholz amezungumzia uwezekano wa kufikiwa makubaliano kabla ya Noeli na Wajerumani wanasubiri kwa hamu kujua muundo wa Serikali mpya utakavyokuwa, tayari  kutekeleza kazi iliowatuma kwa miaka minne ijayo.

Mohamed Abdulrahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Alishawahi kuwa Naibu Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, DW, katika idhaa yake ya Kiswahili. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mamohamed55@hotmail.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts