Dodoma. Tatizo la udumavu ni tatizo ambalo linawakumba watoto wengi wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Tanzania. Tatizo hili kwa kiasi kikubwa linasababishwa na mtoto kushindwa kupata lishe bora tangu akiwa tumboni kwa mama yake. Akina mama wajawazito pindi wanapohudhuria kliniki husisitizwa kuzingatia lishe bore ili kumuepusha mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo hayo.
Kutokana na baadhi ya akina mama wajawazito kushindwa kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya, uelewa duni wa namna bora ya kuandaa chakula kwa ajili ya mtoto, na hali ya maisha duni inayozikabili familia nyingi nchini, Tanzania imeendelea kukabiliwa na tatizo la udumavu, huku jitihada kadhaa zikiendelea kuchukuliwa na wadau mbali mbali kwa lengo la kukabiliana na hali hiyo.
Kuweza kufahamu jitihadi hizi zimesaidia kiasi gani katika kupunguza, au kutokomeza kabisa tatizo hili nchini Tanzania, hususani hapa mkoani Dodoma, The Chanzo imefanya mahojiano maalumu na Afisa Lishe Mkoa wa Dodoma Heriet Carin, na hapa anaanza kwa kuelezea hali ya lishe mkoani kwake:
Heriet Carin: Kwa kweli, kwa mkoa wa Dodoma, hali ya lishe hairidhishi sana. [Hii ni] kwa sababu Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo haiko vizuri kutokana na takwimu ambazo zilitolewa mwaka 2018 [ambapo ilionekana] kwamba Dodoma bado hali si nzuri, kwa sababu ukiangalia udumavu kwa mkoa wa Dodoma ni asilimia 37.2. Maana yake ni kwamba katika kila watoto 100, watoto 37 wamedumaa. [Hii maana yake ni] kwamba ukiangalia kimo na umri haviendani.
Lakini pia ukondefu kwa hawa watoto pia ilionesha ni asilimia 5.5. [Hapa] walau ifike tano kushuka chini ndo tunasema siyo mbaya. Lakini kwa mkoa wetu bado tuko juu ya ile tano . Lakini pia, uzito pungufu kwa mkoa wa Dodoma ni asilimia 17.8. Kwa hiyo, maana yake watoto wale wanakuwa na uzito ambao usio sahihi na uzito ambao walitakiwa kuwa nao kwa kipindi kile.
Lakini pia ulishaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita bado ni changamoto kwa wazazi wengi. Mama anapojifungua, anahitaji kumnyonyesha mtoto tu bila kumpa kitu kingine chochote kwa muda wa miezi sita. Lakini kwa mkoa wetu wa Dodoma utafiti ulionesha kwamba ni asilimia 47.7 tu ya akina mama wanaonyonyesha ndo hufanya hivyo.
The Chanzo: Samahani, huo utafiti ulifanywa na nani ?
Heriet Carin: Utafiti wa mwaka 2018 ulifanywa na Tanzania National Nutrition Survey, [ambao ni utafiti wa hali ya lishe ya kitaifa]. [Utafiti huu] ulifanywa nchi nzima lakini kwa Dodoma ilionesha hivyo. Kwa sasa, bado hatujafanya utafiti mwingine ambao unaweza ukatupa matokeo ambayo ni ya karibu zaidi.
Lakini pia kwenye kumnyonyesha mtoto tunasema kwamba, mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama peke yake bila kupewa kitu chochote, hata maji kwa mkoa wetu bado tuna asilimia 47. Kwa hiyo, bado jitihada zinahitajika ili kuweza kuimarisha hali ya lishe katika mkoa wetu hasa hasa kwa watoto na jamii nzima kwa ujumla.
The Chanzo: Tatizo la udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano linasababishwa na nini hasa?
Heriet Carin: Udumavu? Kama nilivyokwisha kusema ni ile hali ambayo mtoto unakuta umri wake na kimo haviendani. Mtoto labda ana umri wa miaka mitano lakini ukimuangalia kimo chake utadhani ni kama ana miaka miwili. Kwa hiyo, unakuta hakui. Harefuki.
Hili ni tatizo kubwa ambalo linatokana na lishe duni. Tunapoongelea lishe duni tunaongelea virutubisho. Kuna virutubisho ambavyo hakuvitapata [mtoto] kuanzia ujauzito. Hapa tunaongelea zile siku 1,000 kuanzia mama anapotunga mimba mpaka mtoto anapofikisha miaka miwili.
Na mtoto asipopata virutubisho kuanzia mimba mpaka mtoto anapozaliwa, anapofikisha miaka miwili basi unakuta hii hali ya udumavu inaweza ikamtokea kama hatapata virutubisho sahihi.
Kwa hiyo, kwa Dodoma hali hii sana inasababishwa na lishe duni. Na tunaposema lishe duni kuna virutubisho [ambavyo mtoto] anavyovikosa. Unakuta mtoto anakunywa uji tu peke yake [au] anakula wanga mpaka anafikisha miaka miwili au unakuta mama kipindi cha ujauzito hakupata vile virutubisho sahihi. Kwa hiyo, hata makuzi ya mtoto tumboni yakawa siyo mazuri akaja akazaa mtoto dhaifu. Udumavu unatokea ndani ya ile miaka miwili siyo zaidi ya pale.
Na pia kitu kingine [ambacho kinahusiana na] elimu duni kuhusiana na masuala ya lishe. Bado elimu watu haijawafikia. Unakuta muda mwingine mtu anavitu vyote nyumbani lakini hajui aleje. Jinsi vya kuvipangilia [au] jinsi ya kula mlo kamili.
The Chanzo: Kama mkoa, mna mikakati gani ya kuhakikisha kuwa tatizo hili linapunguzwa au kutokomezwa mkoani hapa?
Herit Carin: Mikakati ambayo kama mkoa umejiwekea kwanza ni kutoa elimu, hasa ile elimu ya siku 1,000 za mtoto. Tatizo la udumavu linawaathiri watoto, kwa hiyo elimu ikitolewea ya ulaji, [ikiwemo] jinsi ya kuwalisha watoto itasaidia kuokoa watoto. Lakini mama mjamzito, kama mama ale nini.
Lakini jamii inamsaidiaje yule mama mjamzito, lakini mama anapojifungua mtoto amlishe nini mpaka umri gani, awe anakula vitu gani, amnyonyeshe miezi sita kwanza, kisha aanze kumpa vile vyakula vya nyongeza ambavyo vinakuwa ni vya aina gani, vyakula mchanganyiko, kwa hiyo wakipata hii elimu, hii hali itapungua katika mkoa wetu wa Dodoma.
Lakini pia kutokomeza mila potofu [katika jamii, ni sehemu ya jitihada hizi]. Kuna mila potofu [miongoni mwa wananchi]. Mtu anasema mtoto akishazaliwa labda atapewa vidawa fulani au apewe maji utakuta umeshamuathiri mtoto katika makuzi yake.
Lakini pia elimu kuhusiana na wababa kushiriki katika masuala ya makuzi kwa watoto. Kwa hiyo, baba akielewa akajua kwamba mke wangu akiwa mjamzito lazima ale vitu fulani, lakini akifikia kujifungua basi yule mama anatakiwa kula vitu fulani, lakini mama yule yule anyonyeshe kwa miezi sita huku akiwa anakula ule mlo kamili, mwisho wa siku baada ya miezi sita aanze kumlisha mtoto vyakula vya nyongeza ambavyo vinakuwa na virutubisho sahihi kutoka katika yale makundi matano basi, itasaidia pia kurekebisha hali ya mambo.
Lakini pia mkakati mwingine katika kila halamshauri fedha zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza hizi shughuli za lishe kama ni elimu, basi itolewe. Ni moja pia ya mikakati ambayo mikoa tumejiwekea inatekelezwa.
The Chanzo: Unatathmini vipi utoaji wa fedha kwa halmashauri za Dodoma katika kutekeleza hatua za uboreshaji lishe ili kupunguza athari za za ukosefu wa lishe bora mkoani kwenu?
Heriet Carin: Asante! Kwa suala la utoaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza zile shughuli au afua za lishe katika mkoa wa Dodoma kwa kweli hii inafanyika vizuri. Tumeanza kutekeleza mkataba ambao ulikuwa umesainiwa na wakuu wa mikoa lakini na wakuu wa wilaya kuhusiana na utoaji wa fedha. Lakini kuna shughuli nyingine tofauti kwa ajili ya kutekeleza katika halmashauri.
Katika mkoa wa Dodoma, ukiangalia tulivyoanza [kipindi cha] 2018 /2019 cha mwaka wa fedha, tuliweza kutoa fedha kwa asilimia 55 lakini tukafika 2019/2020 tukawa tumetoa kwa asilimia 53. Ila ukiangalia kwa mwaka [wa fedha] 2020/2021, fedha zilitolewa ni asilimia 69. Kwa hiyo, tunaamini kwa jinsi tunavyoendelea tutaweza tukafika kwenye kutoa asilimia 100.
[Hii ni] kwa sababu wakurugenzi wameelewa, makatibu tawala, wakuu wa wilaya, hata jamii kwa ujumla imeelewa umuhimu wa utoaji wa zile fedha. [Hii inatokana na kufahamu hizi] fedha zinafanya nini. Wameona kwamba zikitolewa basi zikienda kufanya ile kazi na wameona madhara ya udumavu na utapiamlo.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jackline@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.