Dar es Salaam. Pili Mtambalike, mwandishi wa habari, mkufunzi na mshauri wa masuala ya habari wa siku nyingi nchini Tanzania amesema kwamba kipindi cha uongozi chini ya Hayati Rais John Magufuli ndiyo kipindi ambacho Tanzania ilishuhudia kiwango cha chini kabisa cha kuvumiliana kati ya Serikali na waandishi wa habari kuliko kipindi chochote kile katika historia ya Tanzania huru.
Mtambalike, moja kati ya sauti muhimu katika vuguvugu la kudai uhuru zaidi wa vyombo vya habari nchini, alitoa kauli hiyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam hivi karibuni. Amesema kukosekana huko kwa kuvumiliana kulisababisha maumivu makali kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari, ikiwemo waandishi kufunguliwa mashtaka, kutekwa pamoja na vyombo vya habari kufungiwa na kutozwa faini kubwa kubwa.
“Tumeona mabadiliko baada ya kuja Rais Samia [Suluhu Hassan], ni madogo yako polepole lakini hata pia matamshi yake alivyoingia madarakani unaona kabisa kuna nia ya kua na mabadiliko, kue na mahusiano yanayoridhisha kati ya waandishi wa habari na Serikali,” anasema Mtambalike kwenye mahojiano hayo ya takriban saa moja.
Anasema kwamba yeye kama mwandishi wa habari wa siku nyingi, anaamini kwamba kuwepo kwa kuvumiliana kati ya Serikali na waandishi wa habari ni afya kwa taifa. Hata hivyo, mwanahabari huyo anaonya kwamba waandishi wasisubiri kupewa hali hiyo. Anasema: “Tuendeleze hayo majadiliano [kuhusu umuhimu wa kuvumiliana]. Tuyatafute. Tusisubiri tupewe. Kazi za kuongea na watu ambao wanaohusika katika kufanya mabadiliko, hasa ya sheria, kanuni [ni ya kwetu]. Na vile tuelewane kua sisi ni watu ambao ni wazalendo wa nchi hii, tunaipenda nchi yetu.”
Yafuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo kati ya The Chanzo na Pili Mtambalike. Endelea …
The chanzo: Habari za majukumu?
Pili Mtambalika: Tunashukuru mambo sio mabaya, tunaendelea vizuri na majukumu. Wanasema kuwa waandishi wa habari huwa hawaachi uandishi wa habari hata wakisha zeeka [kicheko]. Unakuwa mwandishi wa habari uliekubuhu [kicheko]. Sijui kama ni neno zuri.
The Chanzo: Unasema mwandishi wa habari uliekubuhu? [Kicheko].
Pili Mtambalike: Au aliyekomaa.
The Chanzo: Labda pengine kwa kuanzia, unajua, tukianzia hapohapo ambapo umejaribu kutudokezea jinsi unavyojieleza wewe mwenyewe, labda kwa niaba ya watu wengine ambao hawamfahamu Pilli Mtambalike, labda kwa ufupi unaweza ukatwambia labda Pilli Mtambalike ni nani? Na safari zake na harakati zake kwenye maswala ya vyombo vya habari nchini?
Pili Mtambalike: Sawa sawa. Mimi kusema kweli nimekulia Dar es Saalam japo baba yangu alikuwa anafanya kazi East African Railways Station wakati ule. Kwa hiyo, wengi wetu tumezaliwa kwenye stations za reli lakini baada ya muda yeye alikuja Dar es Saalam akawa anafanya kazi hapa. Kwa hiyo, maisha sasa ya masomo nilisoma St. Joseph Primary School wakati ule, sasa hivi inaitwa Forodhani nikaenda sekondari Zanaki Secondary School O-Level.
Nikaenda Mzizima High School karibu tu pale, halafu kama kawaida yetu ilikuwa zamani ukimaliza kidato cha sita unaenda jeshini. Sasa baada ya kutoka jeshini ndo nikaenda chuo kikuu, nilienda Chuo cha Uandishi wa Habari [SJMC], sasa hivi ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Nikasoma pale astashahada ya uandishi wa habari nikamaliza 1982.
Baada ya hapo nikapata ajira, wakati ule ajira zipo kama nilivyokuwa nasema awali miaka ya nyuma kulikuwa na vyombo vichache sana vya habari. Ile 1982 mimi nilijiunga na SHIHATA kama mwandishi.
The Chanzo: Shirika la Habari Tanzania.
Pili Mtambalike : Shirika la Habari Tanzania ndiyo, kama mwandishi wanaita cub reporter. Nilitoka chuo nikajiunga hapo.
The Chanzo: Ulikuwa unaitwa?
Pili Mtambalike: Cub reporter. Cub ni kitoto cha simba [kwa Kiingereza]. Kwa hiyo, nikajiunga pale SHIHATA nikafanya kazi. Lakini sehemu nyingine ambayo ningeweza kufanya kazi ilikuwa ni redio. Ilikuwa ni Radio Tanzania wakati ule. [Pia kulikuwa na] magazeti ya Daily News na magazeti ya Uhuru. Ndiyo tulikuwa tumemaliza hapo.Kama hujaajiriwa huku utaenda huku ama huku. Kulikuwa na vyombo havizidi vitano.
The Chanzo: Hiyo ni miaka ya [19]80?
Pili Mtambalike: Miaka ya 80 ndiyo. Miaka ya 80 na kurudi nyuma kulikuwa na vyombo [vya habari] vichache sana. Karibuni [waandishi wote] tulikuwa tunajuana. Wote tumesoma chuo hicho hicho. Wengi wetu. Kwa hiyo, kwenye kazi tunakutana wakati tunaripoti habari. Kwa hiyo, tulikuwa wachahe kwanza na wanawake tulikuwa wachache zaidi, [wanawake] wengi walijiunga wengine wakaondoka. Lakini kuna kitu ambacho nadhani kuna watu wengine ambao tunazaliwa kuwa watu fulani fulani. Mimi nilizaliwa kuwa mwandishi wa habari [kicheko] na nimekaa kwenye hii taaluma kwa zaidi ya miaka sasa hivi 37.
The Chanzo: Wow!
Pili Mtambalike: Nimeendelea kuandika lakini kufundisha na vilevile kufanya kazi za ushauri kwenye vyombo mbalimbali vya habari lakini hata kwenye vyombo ambavyo vinahitaji ushauri wa mambo ya mawasiliano. Kwa hiyo, nimefanya pale SHIHATA kwa miaka 10 mpaka 1992. Sijui kama mtakuwa mnakumbuka kulikuwa na tume ya Jaji Nyalali kwenye baadhi ya sheria ambazo walikuwa wanaona ni kandamizi ilikuwa ni sheria ambayo imeanzisha Shirika La Habari Tanzania (SHIHATA) na nafikiri ukandamizi wake ulikuwa kwa kuwa ilipewa jukumu la kukusanya na kusambaza habari na taarifa peke yako Tanzania, nje na ndani.
Sasa kwa akili nzuri ilikuwa ni kufanya mabadiliko kwenye vipengele ambavyo ni kandamizi lakini wakaamua kuiua sheria na wakaua shirika. Mimi kwa mawazo yangu lile shirika lilikuwa na manufaa kwa sababu lilikuwa na ofisi karibu katika kila mikoa. Ilikuwa mikoa yote ilikuwa haijafika kwenye ngazi za wilaya lakini wale waliokuwa wanafanya kazi kwenye mikoa walikuwa wanafursa ya kutafuta habari mbalimbali kwenye sehemu ambazo wanafanyia kazi na walikuwa wanawezeshwa. Walikuwa wana vifaa vizuri mara nyingi wana magari wakati mwingine na walikuwa wanawezeshwa kwenda kutoa taarifa kutoka kwenye ngazi za chini na kuleta kwenye ngazi za kitaifa. Nafikiri kwa kuliua lile shirika hatukufanya maamuzi mazuri.
Lakini baada ya hapo mimi niliondoka katika hilo shirika kabla halijakufa. Nikaenda kujiunga na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF). [[UNICEF] walikuwa wanahitaji mtu wa kwenye kitengo chao cha mawasiliano na habari. Kwa hiyo, nikaenda nikajiunga kule nikafanya nao kazi miaka kadhaa sijui mitatu. Nikajiunga na mpango wa taifa wa kupambana na UKIMWI, National Aids Control Program wakawa wanahitaji mtu wa mawasiliano na habari. Nikaenda pale kusaidia kusimamisha kitengo hicho lakini sehemu ambayo nimefanya miaka mingi sana ni kwenye Baraza la Habari [la Tanzania].
The Chanzo: MCT.
Pili Mtambalike: MCT, ndiyo. Wakati huo ndo lilikuwa linaanza anza tu na mimi ndo nikawa nimejiunga nalo na nikafanya kazi kule miaka 17. Nilianza kama Afisa Programu lakini nikaja kuwa nasimamia programu zote za baraza. Nimekabidhisha ungwe wangu kwenye baraza nilipomaliza kwenye mwaka 2018 [mwezi wa Disemba]. Niliamua kustaafu kwani nimeshatumikia vya kutosha sasa nifanye kazi zaidi za kitaalamu [na] za kiushauri. Kwa hiyo, hiyo ndo tuseme maisha yangu kwenye tasnia ya habari.
Labda kitu kingine naweza kusema kwa sababu kwenye miaka ya nyuma, kwenye miaka ya 1980, kulikuwa na changamoto nyingi sana kwa waandishi wa habari wanawake. Na kulikuwa na vitu ambavyo vilikuwa vinafanyika kitaifa, vinatendeka. Havijaisha lakini sasa hivi angalau kuna uwelewa zaidi. Mambo ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na nafasi ya wanawake kwenye jamii. Kwa hiyo, mimi nilikuwa mmojawapo wa wanawake waandishi wa habari ambao tulianzisha Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA).
Kwa hiyo, mimi ni moja wapo ya waanzilishi wa TAMWA . TAMWA sasa hivi ina takriban miaka 30. Kwa hiyo, ni chama ambacho kimedumu na chama ambacho kimesaidia kubadilisha mitazamo lakini vile vile kubadilisha hata sheria na kuwezesha Serikali kutunga hata sheria mpya ambazo zimesaidia kuangazia maswala ya ukatili kwa vijana.
The Chanzo: Na nisafari ndefu ukiangalia na nilikuwa nataka kufahamu kutokana na hiyo safari yako ambayo umetupitisha, kwa sababu umefanya kazi kama mwandishi, ukawa unaandika habari lakini pia akajihusisha na maswala ya kitaaluma kama hivyo ufundishaji , kutoa ushauri na nini. Na nilikuwa nataka kupata tathmini yako kidogo kuona namna gani unadhani tasnia imebadilika kuanzia miaka ya 1980 ambayo wewe umeanza kufanya kazi mpaka sasa 2021 umekuwa ukijihusisha na hizi kazi. Ipi tathmini yako labda, unaona kuna mabadiliko chanya, hasi au kuna mkwamo fulani?
Pili Mtambalike: Yote mawili naweza kusema. Kuna mabadiliko chanya kuwa kuna mambo mazuri ambayo yamefanyika katika hii miaka kadhaa ambayo nimekuwa kwenye tasnia. Kama nilivyosema, kulikuwa na vyombo vichache sana vya habari, lakini ilipofika mwaka 1992, wakati huo alipokuwepo Mzee [Ali Haassan] Mwinyi, alikuwa Raisi wakati ule kulikuwa na tuseme kama wimbi duniani la kufungua uchumi. Kama sisi uchumi wetu ulikuwa ni uchumi hodhi kwa hiyo tukaamua kuingia kwenye uchumi ambao ni huria.
Kwa hiyo, kuna vitu vingine vikaanza kufata fata moja ilikuwa tasnia ya habari. Mzee Mwinyi alifanya maamuzi, ikiwemo Serikali yake kufungua vyombo vya habari. Kwa hiyo, tukatoka kuwa na vyombo vichache sana kutoka 1992 tumekuwa na vyombo vingi sana vya habari. Kumekuwa na magazeti mengi. Tumekuwa na vituo vingi vya televisheni. Kwa mara ya kwanza tukapata televisheni Tanzania Bara. Kama unajua kihistoria televisheni ilikuwa tu visiwani [Zanzibar] ambayo Raisi [Abeid Amani] Karume alikuwa ameanzisha huko nadhani mwaka [19]72 lakini huku [Tanzania Bara] hatukuwa na televisheni mpaka mwaka [19]92 ambapo ndio televisheni zikaanza sijui ITV, Channel 10 ndo zikaanza.
Lakini vilevile magazeti, tukatoka magazeti sijui mawili tuna magazeti mengi, magazeti ya kikweli kweli, mengine magazeti ya hovyo hovyo lakini yapo . Lakini redio pia, redio tulikuwa na moja tu tuseme huku [Tanzania] Bara tulikuwa na Redio Tanzania baadae ndo ikabadilika ikawa TBC lakini visiwani tukawa na Redio ya Zanzibar kule. Kwa hiyo, mabadiliko chanya ndo kama hayo tumekuwa na vyombo vya habari vingi. Tumekuwa na wigo mkubwa wa kutoa taarifa mbali mbali. Tuna vyombo vya habari vidogo vidogo. Redio ambazo zipo mikoani ambazo nazo zinatoa habari au zinapasha habari kwa umma ambao zinazunguka hizo redio. Hayo ni mabadiliko maziri.
Kitu ambacho mpaka leo, mpaka sasa mimi kinanipa shida ni mabadiliko katika sheria zetu. Kwa muda mrefu sana tulikuwa tupo chini ya Sheria ya Magazeti kwa mfano ya mwaka 1976 na kwenye redio tulikuwa na sheria ambazo zinasimamia mambo ya utangazaji kwa kipindi kirefu sana tulikuwa na mazungumzo sisi tuliokuwa kwenye tasnia na Serikali kwa takribani miaka 10 hivi tulikuwa na mazungumzo marefu tu na yakina na wakati mwingine ya kuelewana wakati mwingine hatuelewani.
Lakini tulikuwa na mazungumzo ambayo kusema kweli tulidhani baada ya mazungumzo hayo tungepata sheria ambazo zingesaidia zaidi sasa kukuza vyombo vya habari na kutoa wigo wa ile haki ambayo tunayo kwenye Katiba ya kujieleza na haki ya kusambaza taarifa na haki ya kupata taarifa na haki ambazo nyingi zipo kwenye zile haki za msingi za binaadamu.
Lakini mwaka 2016, kama mtakumbuka, ilipitishwa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari. Ile sheria sio sheria ambayo kwa mfano mimi ningeitegemea tuwe nayo mwaka 2016 sheria hiyo. Siyo sheria nzuri. Ina sehemu nyingi sana ambazo zina matatizo. Kwa mfano, mambo ya uchochezi, zile [sehemu] zinazofanya makosa ya kitaaluma yawe makosa ya jinai. Yapo kadhaa kwenye uandishi. Kwa hiyo, licha ya kujaribu kuzungumza na wenzetu serikalini na kutoa ushauri kuwa haya makosa ya kitaaluma yabaki kuwa ya kitaaluma sio ya jinai tulishindwa.
Kuna sheria zingine ambazo zilipitishwa 2017 ile ya maswala ya Makosa ya Mtandao ambayo pia ina vipengele vinavyoshika sana waandishi wa habari kwenye kufanya kazi zetu. Kuna sheria wanaita Electronic and Postal Communications Act pia ina sehemu ambazo sio nzuri na hasa kwenye kanuni na upande wa mitandao ndo inawashika sana. Inashika sana mitandao.
Nakumbuka mitandao ilianza ilikuwa mingi kwa hiyo watu walikuwa wanapata wigo wa kupata taarifa sehemu mbalimbali na kujieleza na nini. Lakini baada ya kupitisha zile kanuni na ile sheria nyingi zikaacha kwa sababu waliweka tozo kubwa, weka masharti makubwa makubwa sana. Lakini hata kwenye [Mamlaka ya Mawasiliano] TCRA maswala labda ya vyombo vya mtandaoni bado ni changamoto.
Kwa hiyo, nikifanya tathmini naona hatujafanya vizuri sana kwenye upande wa sheria na zile zinazo simamia vyombo vya habari. Nafikiri tunaweza tukafanya vizuri zaidi na kwenye kipindi kifupi hiki kilichopita pia tumeona sheria hizi zikitumika vibaya sana kufunga vyombo vya habari, kuadhibu watu, kuadhibu watu wanaofanya kazi kwenye blogs mbalimbali kwa sababu labda hawajajiandikisha au hawajalipa tozo ambazo wanatakiwa kulipa. Zile siku hizi sijui ndo wanaita tozo. Sijui. Siku hizi kila mtu na neno jipya ambalo kila mtu analitumia. Lakini ni ada fulani ambayo unatakiwa kulipa na kuendesha …
The Chanzo: Kuendesha account YouTube, blogs.
Pili Mtambalike: Kwa hiyo, kusema kweli ukifanya kwenye hiyo tathmini hatujafanya vizuri kwenye upande wa sheria na zile kanuni zake. Upande wa utashi wa kisiasa wa kuruhusu vyombo vya habari vifanye kazi zake pia katika miaka ya hivi karibuni hatujafanya vizuri sana pia kumekuwa na wasiwasi sana kwa upande wa taarifa na upande wa habari kwenye tasnia hasa kuto kupata au kuingiwa na uoga kuwa unaweza kuchukuliwa hatua kwa sababu ya hizo sheria. Kiasi ambacho kuna kipindi tulikuwa tunaji-censor sisi wenyewe [waandishi wa habari]. Yaani tuna jichuja wenyewe na kujizuia tusiandike taarifa ambazo zitaudhi Serikali au tutaudhi watu wa kwenye mamlaka ili tusipate hizo adhabu.
Kwa tathmini hiyo, mimi naona bado tunaweza tukafanya vizuri zaidi na nilikuwa nataka kuongeza kuwa kidogo tunaona sasa hivi mambo kidogo yanafunguka funguka. Kumekuwa na juhudi au kumekuwa na, tuseme kutoka serikalini kutaka kuwa na mazungumzo na wadau mbali mbali kwenye tasnia ya habari ili tuweze kubadilisha badilisha baadhi ya hizi sheria na taratibu. Mimi nachukulia kama ni kitu ambacho ni kizuri na wale ambao wapo active kwenye maswala hayo wachukue hii fursa wasiiache, wasiikose. Huu wakati ambao tunaona kuna aina fulani ya kutaka meridhiano tuwe na sheria nzuri.
The Chanzo: Kuna fursa ya kufanya vizuri.
Pili Mtambalike: Ipo fursa ya kufanya vizuri zaidi.
The Chanzo: Nilikuwa nataka kufahamu labda, na hapo umegusia kwamba ukiangalia kwa upande mmoja kuna mabadiliko chanya yametokea kama ulivyoelezea na sitaki kurudia, kuna vyombo vingi vya habari, lakini pia kuna vyuo vingi vya habari ambavyo zamani kulikuwa hamna, na kuna internet sasa hivi sio lazima uajiriwe unaweza kufanya kazi ya uandishi kutokea nyumbani mwenyewe lakini upande mwingine una sheria ambazo zinakinzana na hayo maendeleo, na huo ukosefu wa utashi wa kisiasa wa kukubaliana na hali kwamba dunia inabadilika na vyombo vya habari lazima viwepo. Nilikuwa nataka kupata mtazamo wako unadhani, maslahi ya Serikali kuweza kutengeneza sheria hizi mbaya kwa mfano inakuwa ni yapi? Ni kwa sababu hawaelewi au hawafahamu umuhimu wa vyombo vya habari au ni kitu gani kwa mtazamo wako wewe?
Pili Mtambalike: Inakua vigumu sana kupima lakini ninavyofahamu mimi, Serikali duniani kote, hata sehemu ambazo kuna uhuru mpana zaidi wa waandishi wa habari, hua kuna kale ka kania kaku-control, kania kakudhitibiti. Kwa sababu, si jukumu lao Serikali, wanavoona wao mara nyingi, kua wawazi sana katika vitu vyao wanavyofanya na inakua vigumu zaidi hasa ukiwa kwenye Serikali ambazo haziko wazi, hazina uwazi, zinataka zifanye vitu vyake vyenyewe vyenyewe tu wajue wanavyofanya na mtu akitaka kujua “jamani, hivi nilifikiaje uamuzi? Hivi kwa nini pesa kiasi hichi zinatumika? Hivi kwa nini mmefanya hivi?” Inakua shida.
Kwa sababu hawataki kuhojiwa. Sasa ukiwa na, labda sheria au mfumo wa sheria na kanuni ambao unazuia baadhi ya vitu kuulizwa, ni vizuri kwao. Ni vyema kwao. Lakini nayo ni shida kidogo hasa ukiwa unaingia kwenye Serikali kwa nia ya kusema kwa mfano, unapambana na maswala ya rushwa. Watu wa kukusaidia sana kwenye kupambana na rushwa hua ni waandishi wa habari kwa sababu ya ile dhima tuliyokua nayo. Lakini ile tabia yetu ya kutafuta na kuchokonoa na kudadisi na kuuliza.
Sisi ndio watu wa kwanza kujua nini kinafanyika ndivyo sivyo, na serikali hua mara nyingi wanaweza wakapata taarifa nzuri kutoka kwenye taarifa ambazo ziko kwenye vyombo vya habari. Sasa ukishawazuia sasa na kazi hizo, vita yako ya rushwa ni kua wameshashindwa kabla hujaanza. Sasa unaweza ukashangaa sana mtu anajinasibu kua yeye anakuja kupambana na rushwa, kupambana na ubadhirifu, kupambana na matumizi mabaya ya Serikali lakini hataki vyombo vya habari ambavyo viko na uhuru zaidi.
The chanzo: Nilikua nataka kufahamu pia tathmini yako kwenye haya mabidiliko ambayo yametokea. Mimi ni mwandishi wa habari na nimekaa kwenye chumba cha habari, nimekutana na waandishi wa habari wa zamani, wa enzi zako na ukizungumza nao ni kama vile wanaonekana kukata tamaa, au kisikitishwa, na hali ya uandishi wa habari tulionao sasa hivi nchini wakijaribu kuangalia na ile aina ya uandishi wa habari ambayo wao walikua wanaifanya. Wewe ulinganifu wako ni upi kwa sasa, yani unatathmini vipi?
Pili Mtambalike: Kuna shida. Nafikiri nakuelewa. Kuna shida kwenye, tuseme professionalism, utaalam. Mimi hua wakati mwengine naangalia taarifa ya habari, au naweza kuchukua gazeti, nasoma kichwa cha habari nashtuka kweli kua, tunaweza kweli tukaandika hiki kitu hiki? Sasa ukishasoma kichwa cha habari unaingia kwenye ile habari yenyewe unaona imepwaya. Kwa hiyo, nafikiri ile ndio inawapa tabu sana watu ambao wanahariri, wengi wao watakua kwenye madawati ya uhariri kwenye vyumba vya habari. Hua hatufati sana ule ueledi, unakuta taarifa ambazo ni hazijaiva vizuri zinatoka na zinaweza zikatuletea matatizo.
Mimi jana sijui juzi nilikua naangalia, tena kwenye mtandao, gazeti moja hata jina lake nimelisahau linasema “Mbunge apata uchizi” halafu kuna vichwa vingine vya habari vidogo vidogo sijui kapelekwa Milembe sijui kafanya nini. Huandiki habari kama hizi kwa sababu unajitafutia kashfa sio? Vitu kama maradhi ya mtu, tunaambiwa kabisa kwenye zile tunaziita maadili ya waandishi wa habari tue na uangalifu sana hata kama huyo mtu ni mtu ambaye, tunasema ni mtu labda maarufu kwa sababu ni mbunge, maarufu kwa sababu ni mwanasiasa, maarufu kwa sababu ni, labda ni raisi. Lakini tue na uangalifu sana katika kuingilia faragha za watu na kuita maradhi mengine uchizi ni kama matusi tu.
Kwa hiyo, wakati wengine unashtuka kua tunawezaje kuruhusu vitu kama hivi. Na wakati mwingine kwa sababu tunaruhusu vitu kama hivi kama wahariri, ndio tunapata mapigo sasa kutoka kwa watu wenye mamlaka ya kutupiga wakitumia zile sheria. Lakini tukifanya kazi zetu kwa ueledi, tukifanya kazi zetu kwa kufata maadili, pamoja na hizo sheria, tunaweza tu tukafanya kazi zetu vizuri na tusiingie matatani.
The Chanzo: Na hiyo labda pengine inakushangaza kwa kiasi flani kwa sababu, hiyo inatokea katika nyakati ambazo vyuo ni vingi vya uandishi wa habari, mafunzo yanayotolewa kwa waandishi wa habari ni mengi lakini pia kuna maendeleo ya kiteknolojia, kuna intaneti, kuna vitabu vingi vimeandikwa unaweza ukajifunza lakini bado tunakuwa na hali kama hiyo. Hiyo inakushangaza kwa namna moja au nyingine?
Pili Mtambalike: Mimi inanipa tabu sana kuelewa kwa nini tunaweza tukafanya vibaya katika muktadha wa sasa hivi. Inanipa kidogo tabu kwa sababu kwenye miaka ya nyuma nakumbuka hasa kwenye vyuo kwa sababu umetaja vyuo, tulikua tunashida katika mafunzo kwenye vyuo vya kati, hivi vinavyotoa cheti na astashahada.
Vilikua havina viwango, vilikua tu vipo vipo. Mimi leo kwa sababu nina ua hapa naweza nikaweka banda langu nikaanzisha chuo cha uandishi wa habari lakini takriban miaka kama 10 sasa Baraza la Habari Tanzania lilikua linafanya kazi na [Baraza la Elimu ya Ufundi] NACTE kuhakikisha kua ile mitaala inakua mizuri, walimu ambao wanafundisha ni walimu ambao ni wana taaluma, ambao wamepata idhibati ya NACTE na vitu kama hivyo ili kuhakikisha watoto wanaopita kwenye vyuo wanatoka wameiva vizuri.
Sasa hutegemei baada ya hapo mtu anaingia chumba cha habari halafu zinakuja habari ambazo zilikua bado hazijaiva au habari ambazo zinaingilia faragha ya watu, zinaingilia zinaharibu ile taaluma nzima, inashangaza kidogo na sielewi tutafanyaje kwa sababu tutazidi kuharibu taaluma na wakati tunaharibu taaluma wale ambao wanaona sisi tunafanya taaluma yetu hovyo hovyo wanapata sababu sasa ya kututungia sheria mbaya zaidi, sheria ambazo zitafanya kazi zetu ziwe ngumu zaidi kufanya.
The Chanzo: Sawa sawa, ni kweli. Na hapo umesema hujui tutafanyaje.
Pili Mtambalike: Kusema kweli vyuo tunavyo, walimu wazuri tunao, taasisi ambazo zinaweza kabisa kuhakikisha hivi vitu vinabadilika, kwa mfano Baraza la Habari [Tanzania] kazi yake ndio hiyo kusimamia ueledi na maadili ya vyombo vya habari vya waandishi. Tuna vyama kama, Jukwaa la Wahariri kwa mfano. Hilo ni jukumu lao kuhakikisha kua wao wanakua na ueledi kwenye kazi zao. Kuna vyama mbali mbali ambavyo ni vya taasisi za habari ambavyo vinasaidia sana kukuza taaluma.
The Chanzo: Labda huu ni mtazamo wangu tu, sijui pengine naweza nikawa sipo sahihi. Labda pengine inawezekana kwamba tofauti kubwa kati ya zama zenu na zama zetu ni kwamba kipindi cha zama zenu watu walikua wanaingia kwenye uandishi wa habari wakiwa wanataka kweli kua waandishi wa habari. Labda sasa hivi ni kwamba tunaingia kwenye uandishi wa habari kwa sababu pengine hatuna ajira, hamna ajira kwa hiyo unaangalia tu ajira ambayo inapatikana, unakwenda lakini moyoni mwako, nafsini kwako unaona hii si kazi ambayo naitaka. Hiyo unadhani inaweza ikawa inachangia?
Pili Mtambalike: Inaweza ikachangia na inaweza ikachangia sana kua unaweza kua na hao watu wanaoitwa wanataaluma lakini sio wataalamu na sio watu ambao wana ile ari ile passion ya kua wanataaluma kwa sababu wameipenda ile taaluma, wameisomea na wanaifanyia kazi, wanaionea wivu wanataka hasa hasa yani hasa, wanataka ile taaluma iheshimike na ichukue nafasi yake kwenye jamii. Taaluma ambayo inaweza kusema kweli kusaidia sana katika maendeleo ya nchi kama ikifanyika vizuri, lakini kama tunaifanya hivi hovyo hovyo na sisi wote tutaonekana watu tu wa hovyo hovyo.
The Chanzo: Unatathmini vipi ushiriki wa wanawake kwenye tasnia ya uandishi wa habari, pengine kwenye kipindi ambacho wewe ulianza kufanya kazi ya uandishi wa habari mpaka saizi.
Pili Mtambalike: Bado tuna wanawake wachache sana kwenye tasnia ukilinganisha kusema wale ambao wanapita kwenye vyuo. Ukiangalia output kwenye vyuo, waandishi wa habari ratio ya wanawake wanazidi kidogo hata wanaume, unakuta ni takriban 60, 40 kati ya watu wanaoingia kwenye vyuo vyetu. Lakini wakitoka pale hawakai kwenye tasnia. Zipo sababu nyingi ambazo wanatuambia.
Wanatuambia hawataki kukaa kwenye tasnia, kwanza ni zile purukushani za kufanya kazi yenyewe. Wanaona ni kazi ambayo ni ngumu, ni kazi ya hatari haswa wakisikia watu wanapigwa, wakiskia watu wanapotea, wakiskia chombo kimefungwa kwa hiyo wanakosa mishahara na wanaweza wakaenda kufanya kazi kwenye sehemu ambazo hawatopata hizo tabu, hawatopata labda unyanyasaji wa kijinsia ambao uko sana kwenye vyombo vya habari, sana tu na sio tu ndani ya vyumba lakini hata nje wakienda kwa sources wanapata hayo matatizo.
Na wakati mwingine ku-balance kazi mbalimbali ambazo kama mwanamke unatakiwa uzifanye, mara nyingi unajikuta wewe ni mwandishi wa habari lakini pia wewe ni mama, wewe ni mke pia wewe ni shangazi, zile kazi, jirani. Kwa hiyo, jirani akiwa na shida inabidi na wewe ushiriki badala ya kwenda kutafuta story labda Kibaha. Kwa hiyo, bado kuna hizo changamoto nyingi sana.
Tulikua tunazungumzia hivi karibuni maswala ya kujaribu kuwaweka, kuwashawishi wanawake zaidi waingie kwenye, sio tu ndani ya vyumba vya habari lakini wapande kwenye ngazi za utawala kwenye vyumba vya habari na kwa hiyo chini ya utaratibu ambao umewekwa na MCT na TAMWA na taasisi ya vyombo vya habari vya Afrika Kusini MISA-TAN. Kumekua na mafunzo kadha wa kadha ambayo yamekua yakifanyika ili kuwapa zile nyenzo za kuweza kukabiliana au kuweza kufanya hizo kazi ambazo ni zakitaaluma lakini katika ngazi ya utawala.
The Chanzo: Nilikua nataka kufahamu kutoka miaka ya themanini mpaka 2021 ni miaka kama arobaini hivi kama sijakosea ya kufanya kazi kwenye uandishi wa habari. Labda, kwa mfano, kama ukipewa fursa ya kusema mafunzo makuu au ya msingi ambayo umejifunza au umeyapata kwenye safari yako yote hii, unawaza ukawa umepata mafunzo gani?
Pili Mtambalike: Kwenye hii safari, mi nilisomea kua mwandishi wa habari nitoke barabarani niingie mtaani huko niongee na watu, watu labda wenye mamlaka waweze kunipa taarifa ambazo mi nitazichakata na kuzitoa kama taarifa. Hicho ndio nilidhani kua ndio kazi yangu nilipotoka chuo. Lakini kwenye hii safari nikaja kujifunza kua hii sio taaluma ya kijinga jinga tu ya kufanya kitu kidogo tu hicho. Kumbe ni taaluma ambayo mimi ni mwalimu.
Mimi naweza nikawa vilevile natoa mafunzo ya udaktari kupitia uandishi kwenye microphone yangu kupitia kalamu yangu. Ni taaluma ambayo unaweza badilisha mitazamo ya watu kwenye jamii kwa kazi tu ambazo unazifanya. Ni taaluma ambayo kweli mimi kwa mawazo yangu imetukuka sana kama inafanywa vizuri. Kwa sababu kwanza wakati mwingine [waandishi] wanasema tunatakiwa tuwe taaluma kama wanasheria au kama madaktari au tuwe kama sjui nani, tuwe na viwango flani vya nanii. Ni sawa sio kitu kibaya.
Lakini tujue kua ya kwetu iko juu zaidi. Nafikiri [uandihi wa habari] ni taaluma pekee ambayo inajikita katika kutoa haki ya mwananchi katika haki zake za kikatiba zile za kujieleza, kutoa, kupata na kusambaza taarifa. Ni taaluma ya uandishi wa habari tu inaweza kusaidia hapa, sio mwanasheria, sio daktari, sio sijui injinia, ni mwanahabari tu.
Kwa hiyo, kwenye hii safari yangu nimeona kua watu ambao tayari tuko kwenye tasnia, vijana ambao wako kwenye tasnia, waione kua hii sio sehemu tu ya kupata pesa, wasione tu kua hii ni sehemu tu ya kujikimu, wasione kua hii ni sehemu ya kupoteza muda kubangaiza bangaiza. Tuna jukumu sijui tuliite, tuna dhima ambayo haipimiki hivi hivi kwa pesa au kwa muda au kwa nini, ni dhima ambayo ni kubwa sana.
Sasa wewe kama mwanahabari ukiweza kujitambua hivyo, utafanya kazi yako vizuri hutailipua, hutaenda kuandika vitu vya udaku vya kijingajinga kwa sababu sio dhima ya hii taaluma. Dhima ya taaluma hii ni kubadilisha jamii iwe jamii nzuri zaidi, jamii ambayo inaweza ikafanya mambo makubwa, jamii ambayo inaweza ikajiendeleza, jamii ambayo inaweza ikajitegemea kwenye mambo yake, jamii ambayo imepevuka kifikra na inaweza kwenda mbele.
Tunaweza kufanya hivyo kupitia hizi kalamu zetu, vyombo vyetu hivi mbali mbali ambavyo tunatumia, microphone, sijui tunatumia siku hizi tuna ma-blogs, tuna vitu kadha wa kadha ambavyo tunaweza kuvifanya ili kuendeleza nchi nzetu. Sio taaluma tu ya kuchezea chezea. Mimi hua nawaambia [waandishi wa habari], kama wanaona kua hii taaluma ni ya kuchezea chezea waondoke tu wakafanye shughuli zingine, waiache kwa watu ambao wanaielewa na wanaithamini na wanaiona kua ni taaluma ya muhimu.
The Chanzo: Hilo ni jambo la msingi sana, kwamba ni zaidi ya kile tunachokipata kama mshahara …
Pili Mtambalike: Mimi satisfaction, ile kuridhika na kua umefanya mabadiliko fulani. Kuna wakati nilikua nipo moja wapo wa majaji kwenye hizi tuzo za MCT zile tuzo za umahiri wa waandishi wa habari na kitu ambacho tulikua tunaangalia ni zile taarifa za habari ambazo zimetoka kwenye vyombo ambavyo vimefanya mabadiliko fulani hivi, na ukienda hauwezi ukashangaa utaiona tu utaijua, utajua hii kulikua na impact fulani kwenye jamii, kwenye taifa lakini hii ikae tu, hii ni habari ya kawaida.
The Chanzo: Na pale mwanzo uligusia, ulisema kweli hayo ni mafunzo muhimu sana. Na mimi kama mwandishi nimepokea nitayafanyia kazi, ni ya msingi sana na nadhani kama kuna waandishi wa habari wowote ambao watasikiliza haya mazungumzo basi nadhani watakua wamepata kitu cha kujifunza. Lakini pale mwanzo uligusia namna kunavyokua na makosa ambayo ni yakizembe yanayofanywa na vyombo vyetu na waandishi wa habari. Lakini nilikua nataka kufahamu labda kuna vitu vingine vina kukwaza unapoviona vinatokea kwenye vyombo vyetu vya habari kwa sababu mara nyingi vyombo vya habari wao wanajiita The Fourth Estate, ni kama vile hakuna mtu wakuwaangalia ni wao ndiyo watchdogs, lakini who is watching the watch dogs?
Pili Mtambalike: Zipo taasisi za ku watch the watchdogs, moja wapo …
The Chanzo: Point yangu ni kwamba unadhani ni vitu gani vinakukwaza na ungependa kuona vinabadilika unapoangalia vyombo vyetu vya habari na namna vinavyofanya kazi.
Pili Mtambalike: Kitu kimoja ambacho ni mabadiliko ya kiteknolojia ni kua, zamani kulikua na gate-keeping inayoeleweka, ukishatoka mwandishi wa habari kwenye eneo lako la kazi huko nje, umepata taarifa, ukiingia chumba cha habari unakutana na mhariri wa habari, kama ni habari au kama ni makala unaandika unakutana na mhariri wa makala.
Lakini ninaambiwa sasa hivi gate-keeping imepungua sana, na ndiyo maana wakati mwingine tunapata makosa, sehemu ya tatizo hili ni mabadiliko ya kiteknolojia, sehemu yake, kua hata mwananchi wa kawaida sasa hivi anaweza akatoa taarifa bila kuichakata wala nini akaona kuna ajali mahali, ajali imetokea akapiga picha akauliza watu wawili watatu aka share kwenye mitandao, hiyo ni citizen journalism wanasema.
Sasa unakuta na sisi ambao tuko kwenye mainstream journalism tunataka tufanye citizen journalism, hamna gate-keeping. Kwa hiyo, wale watu ambao wangeweza wakagundua makosa kabla hatujaenda hewani au kabla hatujaenda kwenye kuchapa, sasa hivi hawapo au hawapo wa kutosha au ni magazeti machache sana wana zile gate-keeping processes zilizokuepo zamani.
Ilikua ukishatoka kwa mhariri wa habari hata yeye kazi yake inaenda kwa wale wanawaita sub-editors, hasa kwenye magazeti, nafikiri hata radio pia wakati ule Redio Tanzania walikua na sub-editor’s desk. Hao ni watu ambao kazi yao huchuja na kuipitisha ile taarifa kwenye uthibitisho mbali mbali, na kama wanaona kama uthibitisho haujatosha watairejesha aidha kwa mhariri wa habari au kwa mwandishi wa habari ili ikamilike. Sasa hivi hamna au imepungua sana. Na kwa sababu hiyo ndio unapata makosa mengi yanatokea kijingajinga.
The Chanzo: Ubora umeshuka.
Pili Mtambalike: Ubora unateremka mno, sana sana, ubora unateremka sana. Baadhi yao wanasema ni kwa sababu wanataka pia kupunguza gharama ya kua na watu wengi kwenye ule mchakato. Kwa hiyo, unakuta wanakata labda anabaki mhariri wa habari tu, subs desk hamna, hamna sub-editors. Kwa hiyo, mtu anakua na mtu mmoja tu ambae anakua na kazi nyingi za kufanya vingine vinampita.
Lakini najua kwenye baadhi ya vyombo vya habari kua mwandishi wa habari anaweza akapandisha taarifa yake kwenye redio yake, ye mwenyewe anaenda kuitafuta, yeye mwenyewe anaiandika yeye mweyewe anaipandisha, bila kupata idhibati. Hicho ni kitu ambacho kidogo mimi hua kinanipa wasiwasi kwamba [kinachangia] ubora kuteremka kwa sababu kuna michakato flani flani ya uandishi ambazo siku hizi tunakua tunaziacha.
The Chanzo: Labda tukiwa tunaendelea kumalizia mazungumzo yetu na pale juu ulidokeza kidogo. Una tathmini vipi mahusiano yaliopo kati ya Serikali na vyombo vya habari au na waandishi wa habari?
Pili Mtambalike: Kwa muda mrefu naweza kusema nikiangalia awamu mbali mbali. Mimi nilifanya kazi wakati marehemu Mwalimu [Julius] Nyerere alikuepo nimefanya kwa kipande kile, na wakati huo ndio kulikua na vyombo vya habari vichache sana. Lakini tulikua tunajua tulikua tunafanya nini, tulikua tunajua ni kitu gani tunaweza tukakiandika, kitu gani tusikiandike, na kitu gani kinaandikika kwa vipi kwa vipi kwa sababu kulikua na miongozo ambayo iliokua inaeleweka.
Vyombo vya habari wakati ule vilikua vinakazi ambazo zilikua kabisa zimeainishwa. Vilikua vichache lakini kazi zake zimeainishwa. Ilikua sio ya kufichaficha mambo na vitu vingi sana vilifichuliwa wakati ule na watu walipoteza kazi kwa sababu ya kazi zetu kama waandishi wa habari. Lakini ikaja awamu zilizofuata ya kina Mzee Mwinyi, vyombo vikafunguka sana, kukawa na uvumilivu, ile mahusiano kati ya vyombo vya habari na Serikali vilikua sio nisiite nzuri au niiteje, lakini kulikua na ile kuheshimiana na kuvumiliana na kila mtu anafanya kazi zake.
[Benjamin] Mkapa sio mzuri sana lakini Mkapa alikua na background ya uandishi wa habari, tulietegemea angetoa support zaidi. [Jakaya] Kikwete tukawa na kuvumiliana pia wakati wake, tukawa na kuvumiliana tu ya kutosha ambayo iliweza kufikisha hata kue na mazungumzo ya mabadiliko ya sheria mbali mbali. Baada ya Kikwete akaja marehemu [John]Magufuli, naweza kusema dhahiri kabisa uhusiano kati ya wanahabari,au tuseme vyombo vya habari, na Serikali kipindi kile ulikua ni mbaya.
Kulikua na vitisho, kulikua na ukosefu mkubwa wa kuvumiliana na wakati huo ndio sheria zile za hovyo zilikua zinaanza kutumika. Kwa hiyo, kulikua na uoga sana kwenye vyombo vya habari, jinsi gani wanaweza wakafanya kazi zao bila ya kuingia matatani. Kulikua hakuna kuvumiliana kabisa na kusema kweli kulikua na matamshi na matamko, waandishi wa habari wengi walipata shida walipelekwa kwenye vyombo vya sheria, vyombo vya habari vilifungiwa, vilipigwa mafaini kibao, zaidi ya kipindi chochote katika historia ya nchi yetu. Kwa hiyo, haukua wakati mzuri kusema kweli, kwenye kipindi kile cha miaka mitano sita iliopita.
Tumeona mabadiliko baada ya kuja Rais Samia [Suluhu Hassan], ni madogo yako polepole lakini hata pia matamshi yake alivyoingia madarakani unaona kabisa kuna nia ya kua na mabadiliko, kue na mahusiano yanayoridhisha kati ya waandishi wa habari na Serikali. Kama mwandishi wa habari wa siku nyingi, nafikiri ni afya tu kwa afya yetu tuendeleze hayo majadiliano, tuyatafute. Tusisubiri tupewe. Kazi za kuongea na watu ambao wanaohusika katika kufanya mabadiliko, hasa ya sheria, kanuni. Na vile tuelewane kua sisi ni watu ambao ni wazalendo wa nchi hii, tunaipenda nchi yetu.
Kwa sababu tunakosoa [haimaanishi] hatuitakii mema nchi yetu. Sisi tunaitakia sana mema nchi yetu kwa sababu hatuna nchi nyingine ambayo ni ya kwetu. Sana sana utakimbia uende ughaibuni ambapo sio kwenu, umeona watu wanapata shida saivi kule Poland sijui na nchi gani ile, Belarus wako kwenye baridi wanapigwa baridi watu wenyewe wanatoka nchi za joto hamna mtu anaowataka.
Sasa kwa nini sisi tupate shida hiyo ya sisi kwenda kwenye nchi ambazo hatutakiwi na nchi yetu nzuri, safi ipo hapa. Kwa hiyo, mimi kwa tathmini yangu kwenye vipindi mbali mbali kumekua na mahusiano tofauti tofauti. Mengine ni mazuri mapana zaidi, mengine mazuri, mengine yamekua mabovu sana.
The Chanzo: Mama Pili Mtambalike mimi nakushukuru sana kwa muda wako, hili kusema kweli limekua ni darasa kwangu, kama vile nilikua nipo kwenye mhadhara napata mahadhara. Labda pengine ukipewa nafasi ya kusema mabadiliko ambayo ungependa kuyaona kwenye tasnia ya vyombo vya habari katika uhai wako ungesema unataka kuona mabadiliko gani ya msingi kutokea?
Pili Mtambalike: Kuna mabadiliko ya kimfumo ambayo ningependa sana yatokee, yaki mfumo hasa kwenye sheria na kanuni zetu ziweze kuakisi Katiba inavyotaka tufanye kazi kwenye haki zetu za msingi za wananchi wa kawaida, kupata taarifa ambazo zitatusaidia katika maisha yetu, nimesema kabisa wazi Ibara ya 18 kua hii ni haki ya msingi, haki ya wanasema uhuru wa kujieleza ambayo kusema kweli vyombo vya habari ndio wana dhima ya kufanya hiyo haki, haki ya kujieleza iweze ikapatikana.
Nataka pia kama nitapata muda wa kuishi miaka mitano, sita ijayo nione kua tunachukua nafasi yetu, hatuwezi tu kujiita The Fourth Estate wakati tunafanya kazi kama watu wa hovyo hovyo fulani. Fourth Estate ina majukumu yake ambayo, kama nilivosema awali, ni majukumu ya kufanya mabadiliko, kusaidia mabadiliko hasa kwenye hizi nchi zetu changa, mabadiliko ambayo yanatakikana katika kuendeleza nchi.
Sio tu kuandika habari ambazo hazina kichwa wala miguu, lakini tuwe zaidi hasa tuingie zaidi katika kuzitafiti na kutoa sauti ambao hizo sauti hawana. Sio siku zote ukifungua televisheni usikie Rais kasema, sijui waziri kanena. Lakini tupate na taarifa za watu ambao ndio wenye nchi hii watuambie shida zao ni nini, matatizo yao ni nini, tuwape matumaini nao wao wasikike waonekane. Hiyo ndio kitu kingine ambacho nadhani kua tunaweza kufanya kama waandishi wa habari mradi tudhamirie kufanya kazi zetu kwa uweledi, na kwa kuzingatia maadili.
Lakini la mwisho ambalo ni wishful thinking, tuendelee tue na vyombo vingi anuwai. Kwa sababu sasa hivi ukizungumza na watu ambao wapo kwenye vyombo mbali mbali na tafiti ambazo zimefanyika imeonekana kua havina uwezo wa kujitegemea kibiashara si ndio? Ile viability yake, vyombo vingi viko hoi hoi.
Nataka nione vyombo ambavyo vinajitegemea, vyombo ambavyo kiuchumi viko vina afya, vyombo ambavyo vinaweza vikamgharamia mwandishi wake aende akafanye habari kwa wananchi bila ya kutegemea labda mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya au sijui au nani. Unafanya kazi kwenye The Chanzo unachukua vijana wako unaenda mwenyewe kutafuta taarifa, husubiri upate udhamini kwa mtu ambaye baadae huwezi andika habari zake zikawa mbaya, na vitu vingi napenda vitokee lakini hivyo ni baadhi yake.
The Chanzo: Asante sana mama Pili Mtambalike, labda tukimalizia kabisa kabisa, kwenye muda wako wa free, muda wako ambao unakua haupo kwenye Zoom maana mambo ya kiteknolojia tunakesha na kuamkia kwenye Zoom, ikiwa haupo kwenye mkutano na waandishia ukiwanoa namna ya kutimizi majukumu yao vizuri, ni vitu vingine unapenda kuvifanya kwenye muda wako wa huru?
Pili Mtambalike: Free time napenda sana kufanya mambo ya bustani, kwa hiyo hata ukiangalia nyumbani kwangu, nafikiri hata wewe uliniuliza heh, maua mengi hivi?
The Chanzo. Nimeona maua mengi sana ndiyo.
Pili Mtambalike: Kwa hiyo nafanya bustani. Lakini vile vile napenda kusoma, mimi nasoma sana. Nasoma kila kitu kinachopita mbele yangu, nasoma riwaya, nasoma encyclopedia. Nasoma kujiongezea maarifa. Na hicho ni kitu ambacho nimeona pia kinanisaidia kama mwanahabari kujua vitu vingi, kuweza hata kama unaandika kuhusu taarifa fulani, unakua tayari una taaluma ya nyuma kuhusiana ba hiko kitu.
Sasa hivi nina wajukuu pia, kwa hiyo wakirejea kutoka shule ni muda ambao naweza kuchangamana nao, tukaongea, ni wadogo bado lakini ni muda mzuri tu wakuweza kuburudika kwa sababu ni kizazi cha tatu kwa hiyo wana vitu vingi vya ajabu ajabu [kicheko].