Dar es Salaam. Makamu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Gloria Kalabamu amesema kwamba ni muhimu kwa vuguvugu la kudai Katiba Mpya linaloendelea nchini kubainisha kwa wananchi faida nyingine zitakazotokana na nyaraka hiyo muhimu katika uongozi wa nchi badala ya kuzungumzia faida za kisiasa tu, akisema hatua hiyo itawasogeza karibu zaidi wananchi kwenye kuunga mkono vuguvugu hilo.
Kalabamu, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alitoa wito huo siku ya Jumanne, Disemba 7, 2021, akiwa ni mmoja kati ya wazungumzaji wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu cha mwandishi mkongwe Jenerali Ulimwengu Rai ya Jenerali – III, shughuli iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam chini ya mwavuli wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
“[Tuwaambie wananchi] tunaposema Katiba Mpya tunamaanisha kwa upande wa uchumi. Tunamaanisha upande wa upatikanaji wa haki zako. Tunamaanisha upande wa elimu. Tunamaanisha upande wa afya,” alibainisha Kalabamu wakati wa uwasilishaji wa mada yake. “Ili kusudi watu tuweze kujinasibu na hiyo Katiba Mpya badala ya kuwaachia sasa wanasiasa.”
Yafuatayo ni sehemu ya mazungumzo kati ya Kalabamu na Jane Magigita aliyekuwa akiongoza mjadala huo.
Jane Magigita: Pamoja na nia njema ambayo imeonekana kwamba ulianza mchakato wa kuandika Katiba Mpya, na mchakato kweli ukaanza na mpaka hapa tulipofika naona kuna mkwamo, nadhani tunatakiwa kukiri kwamba tumejikwaa. Tulijikwaa wapi na nini kifanyike kujisahihisha? Karibu Gloria.
Gloria Kalabamu: Kama walivyosema wazungumzaji wengine, Katiba ni maafikiano ambayo wananchi tumeyaingia, namna gani tutajiendesha, sio lazima kwamba namna gani tutaongozwa kwa sababu Katiba inagusa nyanja nyingi sana. Na mara hii tumefanya mabadiliko ya Katiba kwa sababu tuliona kuna umuhimu wa watu wote kushiriki katika nchi. Tumeona Katiba zilizopita hatukuwa na ushiriki wetu katika [michakato ya kuandaa] hizo Katiba.
[Katiba] ya kwanza ilikuwa ya mkoloni mwaka 1961 tukaona haitufai. Mwaka 1962 tukasema hatutaki kuendelea na Queen Elizabeth ambalo ni jambo la kawaida. Kwa mfano, sasa hivi Australia na Canada pia wanaliongelea, [kwamba je,] wabaki kwa Malkia au wajitoe kwa Malkia [wa Uingereza, kama Kiongozi wa Nchi].
Na baada ya hapo ikaja kwa ajili ya kushughulikia mambo ya Muungano [kati ya Tanganyika na Zanzibar] kwa mpito. Na mwaka 1977 ikaja ya mambo ya Muungano pamoja na mambo mengine yote ya kudumu ambayo ndio tunayo mpaka leo.
Na kitu kingine ambacho napenda pia kusisitiza ni kwamba lazima Katiba ibadilike. Kama walivyosema [wachangiaji] wengine, kuna mambo mengi sana yamebadilika katika nchi sasa hivi. Kuna utandawazi ambao haukuwepo mwaka 1977 wala 1995 wala miaka ya nyuma ambayo sasa hivi inatuendesha. Kwa hiyo, kubadilika kwa Katiba ni jambo la kawaida.
Hata ile wanayoita Katiba nzuri zaidi duniani ya Ujerumani imeshabadilishwa. Hizo sheria zaidi ya mara sitini na sasa hivi wanaongelea kufanya marekebisho ya sheria nyingine kwa ajili ya mambo ya teknolojia na kwa ajili ya wakimbizi kwa sasa hivi.
Kwa hiyo, kubadili kwa Katiba hata hii tutakayoifanyia kazi ikitoka bado tutaendelea kuibadili. Kwa hiyo, sio kwamba yale marekebisho kumi na nne yasitushtushe sana hata tukipata nyingine huenda tukaibadili kwa kuifanyia marekebisho. Maisha yanabadilika. Binadamu hatulii. Leo yupo hivi, kesho yupo vile na kadhalika na kadhalika. Kwa hiyo, tutaendelea kuwa na mabadiliko hayo.
Sasa twende kwenye hili tulilonalo. Tunaangalia, kama ulivyosema, je, nini kilitukwamisha katika mwenendo mzima [wa upatikanaji wa Katiba Mpya]? Kwa mtazamo wangu, na kwa kusoma pia mtazamo wa watu wengine, kilichotukwamisha zaidi, zaidi ni kwa sababu tulitaka watu washiriki, watu walishiriki, je ushiriki wao ulikuwaje? Uliwashirikisha watu kwa uwiano sahihi, ama haukuwa uwiano sahihi?
Na je, maoni yaliyotolewa ndio hayo hayo yaliyobebwa na yapo mpaka sasa hivi au kuna mabadiliko? Tulitaka watu washiriki wakatoa maoni moja kwa moja kwa kutumia njia mbalimbali. Je, zile njia zilifaa? Watu wote waliweza kweli kushiriki, kulikuwepo kuna ana kwa ana, kuna jumbe fupi za simu, kuna barua pepe, kuna kadhalika. Je, zilifaa, zilitosha, zilimfikia kila mtu?
Kama alivyosema comrade Jenerali Ulimwengu je, watu waliona kwamba hiki ni kitu chetu, watu wote kwa maeneo yote waliona hiki kweli ni kitu cha kwetu sisi, tumeshiriki kweli kikamilifu? Nitakupa takwimu moja ya haraka haraka ambayo nimeipata. Ni kwamba Kigoma walihojiwa watu zaidi ya 23,000 na Dar es Salaam walihojiwa watu zaidi ya 10,000. Lakini Kigoma kuna watu 2,000,000 na Dar es Salaam kuna watu 4, 000, 000. Je, huo uwasilishwaji wa njia iliyotumika ilikuwa kweli inatupeleka mahali?
Lakini kikubwa zaidi ni hili zoezi zima la Katiba Mpya mpaka sasa hivi tunafikia tulimwachia nani? Ukiangalia kimsingi tuliwaachia zaidi wanasiasa, haijalishi wapo wanasiasa wa chama gani au chama gani, lakini wao ndio tuliwaachia. Hata tulivyoenda kwenye Bunge la Katiba, wao ndio tuliwaweka wengi ama wawakilishi kutoka Zanzibar au wabunge kutoka bunge la Jamuhuri.
Wale wananchi ambao tulisema Katiba hii iwe juu yao je, ushiriki wao kweli tulihakikisha upo, na nini kilitokea? Wanasiasa wasipoelewana hawasongi mbele na ndicho kilichotokea, wengine wakaamua hili suala tumeshindwa kuelewana tunaondoka. Je, hapo baada ya kuondoka kuna muafaka? Mpaka sasa hivi tuko hapa tunaongea, tunajadiliana, tunafanya nini, kile kilichopo sasa hivi mezani kina muafaka wa aina gani?
Kwa hiyo, tukiwa tunaangalia ni jinsi gani tumekwama haya ndio mambo ya msingi ya kuangalia. Nakupa mfano mwingine. Katika hali ya kawaida, Katiba ikiwa inabadilishwa tunasema kuwe kuna uwiano sawa wa Zanzibar na Tanzania Bara katika yale maoni ya mwisho. Lakini angalia tu kipengele ni aina gani ya Serikali iliyopo Tanzania na ndio hiyo ni kiini kabisa ni jambo la Muungano kabisa. Angalia zile takwimu za watu waliosema kutoka Bara na watu waliosema kutoka Zanzibar na tulichoamua mwisho tuwe na Serikali ya aina gani.
Kwa hiyo, itakupa kabisa picha kwamba katika kutoa maoni kwetu au kuyachakata yale maoni, kuyapata ni kitu kingine, kuyachakata na kufikia mahali nalo pia ni suala jingine. Je, watu wamejinasibu na hii Katiba tunayoingelea kwa kiasi gani wanajinasibu na Katiba yao? Angalia pia, leo hii tunapokuwa tunadai Katiba Mpya ni vitu gani tunavitilia mkazo? Mara nyingi sana ni masuala ya kisiasa, [ikiwemo] Tume [ya Taifa ya Uchaguzi] ambayo ni mazuri sana. [Mambo ya] Muungano ni mazuri sana na yanafaa. Lakini hayo ni katika asilimia kumi.
Kuna mambo ya haki za binadamu tunazoziongelea ilikuwa ni asilimia kumi na tatu utawala bora, sisi tunatoka mahakamani kama maafisa wa mahakama ilikuwa ni asilimia sita, watu walikuwa na hoja zao nyingi sana nyingine. Je, tunapokuwa tunasema leo hii tunawahabarisha kwamba hili suala la Katiba Mpya tunawahabarisha pia na hivi vitu vingine?
Ni msingi wa muhimu sana kwa sababu mtu akivisikia atajua ndio, haya ndio yalikuwa maoni yetu na suala la kwamba tuwe na Katiba Mpya sasa halitakuwa tena la wanasiasa litakuwa la wananchi na likifika kwa wananchi tutakapo sema kwamba ndio sasa hili ni suala letu sisi kwa hiyo tulifanyie kazi.
Jane Magigita: Kwa hiyo, hapo tunajikwamuaje? Nadhani sio wewe pekee wa kutoa majibu. Leo tuna wadau wote wa huu mchakato kama wananchi na kama raia nadhani umesisitiza kwamba kama kuna umuhimu wa kuwa na mjadala mpana na ushiriki mpana ambao kwenye juzuu [ya tatu ya Rai ya Jenerali] ameuongelea vizuri sana Jenerali Ulimwengu. Lakini sio tu mjadala mpana na ushiriki mpana hata uchakataji wa yale yanayokusanywa na lenyewe ni suala muhimu sana la kuibua huo unaosemwa muafaka wa kitaifa.
Kwenye juzuu sikumbuki ni ukurasa namba ngapi lakini kuna sehemu ambayo Jenerali umefanya pia kwa lugha nyepesi nimempenda. Umeona jinsi gani wananchi wanaweza kutoa wazo likaja pana na likatengeneza muafaka halafu lile likachukuliwa. Umetoa mifano kama maeneo matatu, manne kwenye madini, nadhani umetoa sijui na kwenye rasilimali na kwenye kitu kingine kama vitu vinne au vitatu na ambavyo vinaweza vikachukuliwa sasa na sekta maalumu kama ni ya viwanda sekta ya madini wao wakatengeneza vipengele muafaka vya kikatiba lakini muafaka ukaanza kwa wananchi. Kwa hiyo, unafikiri tunaweza tukajikwamuaje hapo?
Gloria Kalabamu: Kwa mtazamo wangu, kama ulivyosema, ushiriki wa watu ni muhimu na hapo sasa ndio linakuja jukumu la taasisi kama Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwamba watu wapelekewe hizi taarifa sahihi kwamba tunaposema Katiba Mpya tunamaanisha kwa upande wa uchumi. Tunamaanisha upande wa upatikanaji wa haki zako. Tunamaanisha upande wa elimu. Tunamaanisha upande wa afya. Ili kusudi watu tuweze kujinasibu na hiyo Katiba Mpya badala ya kuwaachia sasa wanasiasa.
Lakini pia tusibanwe sana na muda. Tusiwaze sana lazima tuwe na kiwango hiki cha muda cha kufikia mahali pale tusibanwe sana na muda. Lakini tujue kwamba hiki tunachokitaka hiki kiwe ni bora na kiwe kimemgusa kila mtu.
Kuwekewa tarehe ya mwisho ni mbaya sana na hilo la kusema kwamba msijadili, vyote viwili ni vitu vibaya sana. Halafu jambo jengine lazima tuwe wakweli kuna gharama. Kwa hiyo, tunapouendea mchakato huo tujiulize tunataka tufanye gharama gani na hiyo gharama inakuja kwa sababu gani? Kuna machaguo matatu.
Moja, tuanzie tulioishia twende kwenye kura ya maoni kwa kubadilisha sheria ya kura ya maoni? Mbili, turudi tena tuanze kule kwenye mchakato? Na tatu ambapo mimi kwa upande wangu ningeona ni bora zaidi ni kutafuta wataalamu ama wa ndani au wa nje ambao sasa wanaweza wakachakata vizuri ili kusudi tunapokuja kusema kwamba kumbe tunaipigia kura hiki kitu iwe ni kitu ambacho watu wote wanaona tumepata muafaka nacho sasa hivi tulipo kuna vitu vingine ambavyo watu wanasema kwamba bora iende vivyo hivyo kwa sababu angalau mambo fulani yamekamilika, lakini haikuwa muafaka.
Jane Magigita: Kwa hiyo, unasema kwamba maoni yaliyokusanywa wapatikane wataalamu wakayachakate halafu hatutarudi kwenye mfumo kama wa Bunge au Mkutano wa Taifa wa kikatiba. Itaenda moja kwa moja kwenye kupitishwa, hayo ndio maoni yako?
Gloria Kalabamu: Hayo ni maoni yangu.
Jane Magigita: Kwa sababu una wasiwasi na gharama au ni kwa sababu ya nini?
Gloria Kalabamu: Gharama ipo lakini sio sana. Wasiwasi wangu ni kwamba mwisho wa siku Katiba ni andiko la kisheria. Ni nyaraka inayohusu mambo ya sheria. Kwa hiyo, hatuwezi tukawaacha wataalamu kabisa.
Ni lazima na wataalamu wawepo kwa sababu Katiba ni sheria. Hata ukiangalia sehemu nyingine itapita itaenda itafanya nini lakini mwisho wa siku lazima watu wenye taaluma hizo wabobezi ndugu zetu kama kina Jenerali Ulimwengu na wengine, wengine walioko sehemu zote ama watu kutoka nje. Kwa sababu lengo ni kwamba yale yaliyotolewa na wananchi sasa yakae katika namna nzuri ya kisheria.
Lakini kama nilivyosema, jambo la tatu na la nne la msingi kabisa kwangu mimi ni kwamba utu na heshima ni muhimu. Kitu hata kikiwa kizuri vipi kama hakina nia njema ya thabiti basi hakitatekelezeka. Kwa hiyo, tunapokuwa tunasukuma tujikumbushe utu na heshima na kuheshimiana. Kwamba katika hili hatutakubaliana katika kila jambo, mambo mengi sana tutaenda tukiwa tofauti.