The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

CHADEMA, ACT-Wazalendo Washauriwa Kumaliza Tofauti Zao

Wadau wa siasa nchini wanabainisha kwamba mnufaika mkubwa wa mtifuano kati ya vyama hivyo viwili vya upinzani nchini ni yule kila mmoja wao analenga kuitoa madarakani – CCM.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wachambuzi na wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wameelezea kusikitishwa kwao na mzozo unaoendelea kuvikumba vyama viwili vya upinzani vya ACT-Wazalendo na CHADEMA, wakisema hali hiyo si afya kwenye siasa za mabadiliko ambazo Watanzania wanazitegemea kutoka kwa vyama vya upinzani.

Wachambuzi hao wamebainisha hilo licha ya kukiri kwamba ukinzani wa mawazo miongoni mwa wananchi ni afya kwenye jamii ya kidemokrasia na tofauti za kisera miongoni mwa vyama vya siasa ni msingi wa siasa za vyama vingi.

Hata hivyo, wachambuzi hao wanakubaliana kwamba tofauti inayoendelea kujidhihirisha kati ya vyama hivyo vikuu vya upinzani nchini si aina ya tofauti inayoweza kuendekezwa kwani inaashiria hatari ya kuzuia mchakato wa mabadiliko badala ya kuuharakisha.

“Nadhani hata kama siyo kwa minajili ya kujipanga na kuiondoa [Chama cha Mapinduzi] CCM madarakani lakini kuboresha mahusiano kati ya viongozi wa vyama hivi vya siasa ni muhimu sana,” mhadhiri wa siasa na utawala wa umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Richard Mbunda anaieleza The Chanzo.

“Kwa sababu baadhi yao wanaimba wimbo wa maridhiano tena kwa kutaka maridhiano na CCM,” anaongeza mwanazuoni huyo na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Tanzania. “Basi ni dhahiri wangeanzia kwanza katika upinzani, waanze kujenga hayo maridhiano mazuri ili baadae hata wanapoyaita katika muktadha wa kitaifa maridhiano na chama tawala ilete mantiki zaidi.”

Msingi wa mvutano

Angalau mambo manne yametajwa kama msingi wa sintofahamu kati ya vyama vya ACT-Wazalendo na CHADEMA, sintofahamu ambayo mara nyingi imekuwa ikishuhudia baadhi ya wanachama wa vyama hivyo wakishutumiana, kukebehiana, kudhihakiana na muda mwengine hata kurushiana matusi kwenye mitandao ya kijamii.

Mambo haya yanajumuisha hatua ya ACT-Wazalendo kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar licha ya mwanzoni kuweka msimamo kwamba isingechukua uamuzi huo baada ya kuita kile kilichofanyika mnamo Octoba 28, 2020, kama “uchafuzi” badala ya uchaguzi.

CHADEMA na ACT-Wazalendo pia wamekuwa wakitofautiana juu ya suala zima la namna ya kukabiliana na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, hususan linapokuja suala la kuchukua juhudi za kurekebisha taasisi za kidemokrasia kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025. Wakati ACT-Wazalendo ikionesha utayari wa kujishirikisha na Serikali katika hili, CHADEMA imekuwa ikigoma kujiweka karibu na Serikali.

Ni katika muktadha huu ndipo moja kati ya vipindi vibaya katika mahusiano kati ya vyama hivi kilijidhihirisha pale ACT-Wazalendo ilipoamua kushiriki kikao kilichoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Francis Mutungi kujadili kile kilichoitwa hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini na kupendekeza namna za kuiboresha. CHADEMA, pomoja na NCCR-Mageuzi, walisusia kikao hichi kilichofanyika Dodoma.

Katika suala hili hili la kuufanyia mageuzi mfumo wa demokrasia ya vyama vingi Tanzania ndipo tofauti nyingine kubwa inapoonekana kati ya vyama hivi viwili. Wakati ACT-Wazalendo ikisema kipaumbele kwa sasa ni Tume Huru ya Uchaguzi, CHADEMA wanasema hapana, kipaumbele ni Katiba Mpya.

ACT-Wazalendo inadai Tanzania haiwezi kufufua mchakato wa Katiba Mpya kwa Bunge lililopo hivi sasa ambalo kwa kiasi kikubwa limetawaliwa na wabunge wa CCM, CHADEMA, kwa upande wake, inasema Katiba Mpya ni muhimu kwani upatikanaji wake utahakakisha upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Kuna suala la hatma ya Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe ambaye yuko gerezani akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na ugaidi. Wakati ACT-Wazalendo ikiamini kwamba Mbowe anaweza kuwa huru kwa viongozi wa upinzani kufanya mazungumzo ya karibu na Serikali, CHADEMA haioni umuhimu wa kufanya hivyo kwani wanaamini Mbowe hana hatia na Serikali inapaswa kumuachia bila masharti yoyote.

Rashid Abdallah ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya siasa za Tanzania ambaye ameuelezea mvutano unaoendelea kati ya CHADEMA na ACT-Wazalendo kama “vita vya panzi” na katika mazingira kama hayo si vigumu kumjua mnufaikaji wa vita ya aina hiyo.

“Hapa atakayenufaika ni yule aliye katika dola,” ni mtazamo wa Abdallah. “Ikiwa wanaweza kukubaliana kwamba tunatumia mbinu tofauti za kisiasa kuondoa matatizo lakini lengo letu ni moja, basi sioni sababu ya kwa nini washambuliane kwa maneno na kuvutana. Lengo ni moja, njia ndiyo tofauti.”

Nini kinaweza kuwa kinachochea sintofahamu hii?

Markus Mpangala ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anayeamini kwamba ni vigumu sana kwa vyama hivi kuweza kukaa meza moja, akitaja hatua ya ACT-Wazalendo kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama kizuizi kikuu cha ufanikishaji wa maelewano kati ya vyama hivyo vikuu vya upinzani.

“ACT-Wazalendo ni sehemu ya utawala wa 2020-2025,” anabainisha Mpangala. “Kwa hiyo, tofauti hii inatengeneza ukuta baina ya vyama hivi viwili. CHADEMA wanaiona [ACT-Wazalendo] kama mnufaika wa siasa za CCM wakati chenyewe kinajiona ni mhanga wa siasa za CCM.”

Wakati ni ukweli kwamba hakuna kiongozi wa CHADEMA aliyejitokeza hadharani na kutamka kauli hizi, si mara moja wala mbili imekuwa ikishuhudiwa watu wanaojinasibisha na CHADEMA kuielezea ACT-Wazalendo kama “CCM B” na majina kama hayo yanayolenga kukifutia chama hicho hadhi ya upinzani.

Dk Mbunda anadhani kwamba mvutano huu kati ya vyama hivi viwili si tu ni wa kihistoria bali pia ni wa kibinafsi. Mwanazuoni huyo anaeleza kwamba wana-CHADEMA wanaonekana bado hawaja msamehe Zitto Kabwe tangu watofautiane naye ndani ya chama hicho na kupelekea Zitto kuondoka kwenye chama hicho.

“Uhusiano kati ya CHADEMA na ACT-Wazalendo haukuwahi kurekebishwa,” anaeleza Dk Mbunda. “Na hiyo ni tangu kipindi baadhi ya viongozi kama Zitto Kabwe walipoondolewa CHADEMA kutokana na tuhuma za uhaini kabla ya kujiunga na ACT-Wazalendo ili kuendeleza maisha yao ya kisiasa.”

Kwa mujibu wa Mbunda, ni vigumu kwa vyama hivyo kuelewana wakati Zitto akiwa Kiongozi wa ACT-Wazalendo. Lakini hoja hii inapingwa na mmoja wa viongozi waandamizi na mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo ambaye anaamini kwamba Zitto siyo msingi wa mvutano huo.

“Hivi ndivyo CHADEMA walivyokuwa wakishughulika na [Chama cha Wananchi] CUF kabla ya kuibuka kwa ACT-Wazalendo,” anasema mwanasiasa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe mtandaoni.

Anaongeza kwa kusema kwamba ni mkakati wa CHADEMA kwamba siasa za Tanzania Bara ziwe kama vile za Zanzibar ambapo kuna kuwa na chama tawala na chama kimoja madhubuti cha upinzani.

“Chama chochote kitachoibuka kutikisa himaya yake,” anafafanua, “ni lazima kikabiliane na hali ambayo ACT-Wazalendo inakabiliana nayo.”

Vyama vyenyewe vinasemaje?

The Chanzo ilimuuliza Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika ana mtazamo gani kuhusiana na mvutano huu kati ya chama chake na ACT-Wazalendo ambapo alijibu kwa kuonesha kwamba yeye haoni kama kuna mvutano.

“Ili nijibu hilo swali,” aliagiza Mnyika, “nahitaji unitumie uthibitisho wa picha kutoka kwenye mitandao ya kijamii zinazoashiria tofauti za vyama hivyo. Nahitaji kupata uelewa wa jambo hilo ndipo nikupatie majibu husika.” The Chanzo, hata hivyo, haikufanya kama Mnyika alivyoagiza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Ado Shaibu aliieleza The Chanzo kwamba anatambua uwepo wa hali hiyo na kwamba inamsikitisha sana huku akiitaja hali hiyo kuwa siyo nzuri kwani vyama vyote hivyo viwili vina lengo moja la kushika na kuiongoza dola kwa kuiondoa CCM madarakani.

“Mimi sifurahii mivutano baina ya wapinzani,” anasema Shaibu. “Utofauti wa kisiasa sio vita. Watu wanaweza kupishana kimawazo. Lakini kupishana ni lazima kuwe juu ya masuala. Pia, ni lazima watu wapishane kwa uungwana.”

Ni yapi madhara ya muda mrefu ya hali hii?

Wachambuzi wanatofautiana kuhusiana na yapi yanaweza kuwa ni madhara ya muda mrefu ya hali hii kama hatua stahiki za kuirekebisha hazitachukuliwa kwa haraka. Abdallah, kwa mfano, anasema hawezi kutabiri kitu kwani, kama msemo mashuhuri unavyosema, “kwenye siasa hakuna adui wa kudumu.”

“Na hata sasa kusema kwamba upinzani hautashirikiana [kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka] 2025 au utashirikiana yote mawili yanawezekana kwa kweli,” anabainisha. “Lakini, lililo muhimu kwa wao kama wapinzani ni kushirikiana kwa sababu hapo ndiyo watakuwa na zile nguvu za pamoja za kupambana na chama tawala.”

Lakini Dk Mbunda anaiona hatari inayoweza kutokana na mivutano hii ambayo anaihusisha na vyama hivyo kutokukuwa kitaasisi. Na hatari hii ni wapiga kura kuona vyama hivi haviko makini na hivyo kuacha kuvifuatilia na kupigia kura wagombea wake wakati wa uchaguzi.

“Hiyo mikwaruzano kati ya viongozi na wafuasi wa vyama kama walivyoiendeleza kwa kubezana na kudharauliana inapunguza nafasi ya upinzani kuaminika,” anaonya Dk Mbunda. “Na hata fursa na uwezekano wa wao kuweza kushika dola kwa kupitia sanduku la kura zitazidi kuwa nyembamba kadiri hali hii itakavyozidi kuendelea.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts