Dodoma. Wabunge wa Bunge la Tanzania wamebainisha kwamba sheria na kanuni kandamizi zinazozuia vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru zinapaswa kurekebishwa ili waandishi waweze kutimiza wajibu wao kama mhimili wa nne wa dola.
Watunga sheria hao walitoa wito huo wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan) yaliyofanyika mnamo Februari 12, 2022, yaliyolenga kuwafahamisha wawakilishi hao wa wananchi vifungu vya sheria na kanuni vinavyominya uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Kauli za wawakilishi hao zinakuja siku chache tu baada ya Serikali kuyafungulia magazeti manne ya MwanaHalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima huku Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akibainisha nia na utayari wa Serikali wa kuyafanyia kazi maoni na mapendekezo ya wadau yanayolenga kuboresha sheria na kanuni zinazoongoza uandishi wa habari Tanzania.
“Nikiri kwamba yapo mambo yamezungumzwa hapa [kwenye mafunzo] ambayo yanahitaji maboresho,” alisema Mbunge wa Mlalo (Chama cha Mapinduzi – CCM) Rashid Abdallah Shangazi wakati akichangia. “[Marekebisho ya sheria na kanuni] ni hoja za msingi ambazo tunapaswa kuzitazama kwa mawanda mapana.”
Baadhi ya sheria na kanuni zinazolalamikiwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari nchini ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo, pamoja na mambo mengine, inaruhusu Serikali kufungia magazeti.
Sheria hiyo pia inaweka sharti kwa gazeti kuwa na leseni ambayo inapaswa ihuishwe kila mwaka. Pia, inaweka sharti kwamba ili mtu afanye uandishi wa habari Tanzania ni lazima awe na elimu ya kiwango cha stashada au shahada ya uandishi wa habari au taaluma inazohusiana nazo.
Kingine kinacholalamikiwa ni Kanuni za Mawasiliano na Kielektroniki na Posta, Maudhui ya Mtandaoni za 2020 ambazo pamoja na kuipa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kufungia redio, runinga na vyombo vya habari vya mtandaoni kwa kukiuka vitu kama vile “maadili ya taifa” pia zinaweka sharti kwa vyombo vya mtandaoni kuwa leseni inayohuishwa kila mwaka ambayo gharama yake imekuwa ikilalamikiwa na wadau.
Halima Mdee ni Mbunge wa Viti Maalum ambaye anaamini kwamba sheria na kanuni “zilizotungwa kwa makusudi, na siyo kwa bahati mbaya” zinapaswa kubatilishwa kwani “zimekuwa zikiipa Serikali mamlaka ambayo imekuwa ikiitumia vibaya.”
Mdee anaamini kwamba ni muhimu kwa wadau kutumia mwanya huu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya kutaka kuweka mazingira safi kwa kazi za waandishi wa habari nchini kufanikisha mabadiliko ya sheria hizi.
Mnamo Aprili 6, 2021, ikiwa ni siku 18 tu baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kufunguliwa kwa vyombo vyote vya habari vilivyokuwa vimefungiwa, akisema: “Tusiwape mdomo mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa habari na nataka kanuni ziwe wazi, ili mtu akifungiwa ajue kosa na adhabu yake. Tusifungie tu kibabe.”
Mbunge wa Momba Condester Michael (CCM) alieleza kwamba wao kama watunga sheria na watu wanaoisimamia Serikali wanatambua mchangao wa vyombo vya habari, akisema wanaifanya jamii kujua kinacho endelea na hivyo wataunga mkono juhudi za kufanya maboresho ya sheria na kanuni zitakazowawezesha waandishi kufanya kazi kwa uhuru zaidi.
Akizungumzia nafasi waliyonayo wabunge kufanikisha juhudi hizi za waandishi wa habari na wanaharakati wa uhuru wa kujieleza, mwenyekiti wa Misa-Tan Salome Kitomari aliwaita wabunge “vinara wa mabadiliko” na hivyo ni muhimu kuwashirikisha kwenye juhudi hizo.
“Tukiwa na wabunge wenye uelewa, maana yake hata muswada ukipita bungeni itatusaidia kusukuma yale mambo ambayo tunafikiri yana kwaza kazi yetu ya uandishi wa habari,” anaamini Kitomari ambaye ni moja kati ya waandishi wa habari mahiri nchini Tanzania
Jackline kuwanda ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.