Mara. Damas Wilson na Richard Kayanda, vijana wa hamasa wa CHADEMA waliokuwa kwenye timu ya kampeni ya aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kupitia chama hicho cha upinzani Esther Matiko kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020, waliripotiwa kutoweka kwenye mazingira ya kutatanisha mnamo Oktoba 26, 2020.
Mpaka wakati wa kuandika habari hii, vijana hao bado walikuwa hawajapatikana.
Kutokupatikana kwa Wilson, mkazi wa mtaa wa Byambwi, kata ya Bomani na Kayanda, mkazi wa mtaa wa Byambwi kata ya Nyandoto, kumeacha siyo majonzi tu kwa wapendwa wao bali pia dhiki, maisha duni na hali ya kukata tamaa kwa wategemezi wao, ambao wanajumuisha wake na watoto wanaopaswa kupambana na changamoto za maisha bila ya uwepo wa waume na baba zao hao.
Juhudi za kumtafuta Wilson, aliyekuwa akifanya kazi kama kinyozi kujiingizia kipato, na Kayanda ambaye shughuli yake ni kupaka rangi, zimeendelea kwa muda sasa, huku ndugu na wanachama wa CHADEMA wakishirikiana kuwasaka wapendwa wao hao huku na kule, wakienda kwa mamlaka hii ya Serikali kabla ya kwenda kwa ile, bila mafanikio yoyote.
Akichangia kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi mnamo Machi 3, 2021, Mbunge wa Viti Maalum Esther Matiko alimtaka waziri aliyekuwa anahusika na wizara hiyo George Simbachawene kuuleza umma wa Watanzania juu ya hatma ya vijana hao wawili, akibainisha kwamba mamlaka zote zinazohusika na ulinzi na usalama nchini zinafahamu taarifa hiyo.
Wako hai au wamekufa?
“Tungependa kufahamu hatma ya hawa ndugu [zetu],” alisema Matiko ambaye kwa sasa amefukuzwa uwanachama wa CHADEMA. “Kama wamekufa tuambiwe ili tuweke matanga. Na kama wako gerezani, [tuambiwe ili] tuweze kuwatembelea na kuwaona.”
Hata hivyo, Serikali haikueleza chochote kuhusiana na vijana hao.
Akijibu swali la mwandishi wa habari hii juu ya hatua ambayo uchunguzi wa kupotea kwa vijana hawa umefikia, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime Rorya William Mkonda alisema: “Ndugu zao kama wapo, ambao wametoa taarifa, waje tutawataarifu. Kama wametoa taarifa, waje wamwone [Mkuu wa Kituo] wataambiwa kama wanaendelea kutafutwa au vipi.”
Wakiongea na The Chanzo kwa nyakati tofauti, wake wa vijana hao wanabainisha kwamba hali ya kutokuwa pamoja nao kunawafanya waishi maisha magumu yaliyojawa na hofu, wasiwasi na dhiki, huku wakiziangukia mamlaka za nchi kuwasaidia kuwatatulia kitendawili kinachozunguka maisha ya Wilson na Kayanda.
Tulijua ni uchaguzi tu kumbe …
“Tulikuwa tunaenda kwa Esther Matiko [ambaye alikuwa] anatuambia labda wamekamatwa tu kwa sababu ya kampeni ili kupunguza kura. Baada ya kura basi watarudi,” anasema Jael Kayanda, mke wa Richard Kayanda, wakati alipotembelewa na The Chanzo nyumbani kwake. “Basi, ikafika muda waliachiliwa ambao walikuwa wamekamatwa. Lakini hatukupata waume zetu.”
Jael, mama wa watoto watatu, anasema hakujipanga kuendesha familia peke yake, akilalamikia changamoto nyingi za malezi na maisha zinazoikumba familia yake ambazo anaamini zisingekuwa na uzito kama ulizo nazo kwa sasa endapo kama mume wake Richard Kayanda angekuwepo nao.
“Mimi nilikuwa nauza vitenge lakini kwa sasa nimekaa tu kwani mtaji umekata baada ya kuutumia kumtibia mtoto,” anasema Jael. “Mimi bado nina matumaini kwamba mume wangu atarudi na kuja kujumuika na sisi. Naiomba Serikali inisaidie kutimiza matumaini yangu hayo.”
Naye Esther Wansatu, mke wa Damas Wilson, ameiambia The Chanzo kwamba amelazimika kurudi nyumbani kwao baada ya kumsubiri mume wake bila mafanikio. Gharama za maisha, pamoja na mahitaji ya mtoto mmoja ambaye walibahatika kumpata na Damas, ndiyo chanzo cha yeye kurudi kwa mama na baba yake.
“Pale nilipokuwa nakaa nilikuwa nimepanga, na tulikuwa tunadaiwa pesa ya miezi ya nyuma ambayo tulikuwa hatujalipa takribani Sh170,000,” anasema Esther ambaye anajishughulisha na vibarua vya ujenzi kukidhi mahitaji yake ya msingi. “Kwa hiyo, nikaona siyo vyema niendelee kukaa pale na hamna mtu anayenisaidia kulipa hiyo kodi wala kupunguza. Nikaona ni vyema nirudi nyumbani.”
Vyombo vya ulinzi viwajibike
Bashiri Abdallah ni mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Tarime ambaye amebainisha kwamba mbali na chama hicho cha upinzani kuendelea na juhudi za kuwatafuta Damas Wilson na Richard Kayanda pia kimekuwa kikizisaidia pale inapobidi familia za vijana hao.
Abdallah alieleza kwamba mara baada ya watu vijana hao kutoonekana kwa muda mrefu, CHADEMA ilifanya jitihada za kuwawezesha wake zao na kiasi cha fedha kama mtaji wa biashara ili waweze kutatua changamoto zao za kimaisha. Hata hivyo, biashara hizo zimeshindwa kuendelea kwa sababu mbalimbali.
“Wito wetu kwa Serikali na vyombo vya dola vyote ni kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwatafuta vijana hawa kwa sababu watu hawa wanategemewa na familia zao na watu hawa ni muhimu sana ndani ya jamii yetu,” alisema Abdallah. “Kwa hiyo, Serikali na vyombo vya dola vyote tunawaomba watekeleze wajibu wao ambao ni kuwalinda raia na mali zao.”
The Chanzo ilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni ili kufahamu kama Serikali inachukua mkakati wowote wa kusaidia vijana hawa kupatikana lakini ilishindikana kupata majibu kutoka kwake baada ya simu zake kutokupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakuweza kujibu.
Hali hii ya vyombo vya ulinzi na usalama kushindwa kulipatia ufumbuzi jambo limemfanya Esther Matiko kupunguza juhudi za kuwasemea vijana hawa baada ya kushutumiwa kwamba anatumia sakata la vijana hao kama mtaji wa kufanikisha malengo yake ya kisiasa.
Nini kinapasa kufuata?
“Nimewashauri ndugu [wa hawa vijana] kuitisha hata mkutano na waandishi wa habari na hata kujaribu kumfikia Rais [Samia Suluhu Hassan],” Matiko anaieleza The Chanzo. “Sisi tukizungumza [Serikali] inadai ni siasa tu. Wanauliza mbona ndugu zao hawazungumzi?”
Bonny Matto ni mwanaharakati kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mkoani mara ambaye licha ya kulaani kupotea kwa vijana hao, amezishauri familia wafikirie kulipeleka Jeshi la Polisi mahakamani kulishinikiza litoe majibu ya walipo wapendwa wao.
“Mahakama ndio chombo pekee cha kutoa haki katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema Matto wakati wa mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya simu. “Kwa hiyo, wanaweza kwenda kuhoji kwamba watu wetu wamepotea, tumetoa taarifa polisi na hakuna kitu kinachofanyika. Wanaweza kutoa taarifa na kufungua faili mahakamani.”
Jofrey Cosmas ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza, Tanzania. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni cosmasjofrey54@gmail.com.