The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali, Wataalam Wachambua Hali ya Ukame na Upungufu wa Chakula Tanzania

Watanzania takriban 437,000 kutoka maeneo mbali mbali ya nchi wanahisiwa kukabiliana na tishio la upungufu wa chakula.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Serikali imesema kwamba Watanzania hawana sababu ya kuwa na hofu ya upungufu wa chakula nchini unaoweza kusababishwa na hali ya ukame ambao umekuwa ukiripotiwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, ikisema kwamba hali hiyo imeathiri mifugo tu na siyo binadamu.

Hayo yameelezwa mnamo Februari 15, 2022, na Charles Msangi, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Uratibu wa Menejimenti ya Maafa iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu alipokuwa akijibu swali la The Chanzo endapo kama Serikali imepokea taarifa zozote kuhusiana na uhaba wa chakula nchini.

“Ukosefu wa maji umeathiri mifugo tu,” alijibu Msangi kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu kupitia Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Augustino Tendwa. “Mpaka sasa hakuna madhara kwa binadamu upande wa usalama wa chakula.”

Kauli hiyo ya Serikali hata hivyo inakuja wakati ambapo Watanzania takriban 437,000 kutoka maeneo mbali mbali ya nchi wanahisiwa kukabiliana na tishio kali la upungufu wa chakula, kwa mujibu wa shirika linalojihusisha na uangalizi wa usalama wa chakula nchini la Integrated Food Security (IPC).

Kati ya halmashauri 14 ambazo IPC ilifanya utafiti wake ukijumuisha watu milioni 3.4, halmashauri nne za Handeni, Longido, Mkinga, na Monduli ziliripotiwa kukabiliwa na hali ya juu ya tishio la upungufu wa chakula.

“Mavuno hafifu ya hivi karibuni yamepelekea kupungua kwa upatikanaji wa chakula na kupunguza shughuli za kiuchumi zilizokuwa zikifanywa awali baada ya mavuno,” inasema sehemu ya taarifa ya IPC ambao ni sehemu ya Mfumo wa Taifa wa Usalama wa Chakula na Lishe (MUCHALI).

Mnamo Januari 29, 2022, shirika la misaada la Msalaba Mwekundu liliripoti kwamba zaidi ya watu milioni 2 kutoka mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga wanakabiliwa na athari zitokanazo na hali ya ukame ulioripotiwa kuathiri maeneo hayo, hususan mifugo ambayo imeripotiwa kufa kwa wingi.

Shirika hilo lilionya kwamba upungufu wa chakula umeripotiwa kwenye maeneo yote ya nchi yenye viwango vidogo vya mvua na kwamba watu wamekuwa wakiuza hifadhi yao ya chakula ili kukidhi mahitaji mengine muhimu ya nyumbani. Msalaba Mwekundu pia iliripoti kupanda kwa bei za vyakula kutokana na kuongezeka kwa uhitaji miongoni mwa wananchi.

“Mpaka kufikia Januari 18, 2022, tumekuwa tukipokea simu kutoka kwa madiwani wakiomba msaada wa haraka,” shirika hilo lilikiri kwenye taarifa yake.

The Chanzo ilimuuliza Felician Mtehengerwa ambaye ni Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania kama taarifa zao pia wameishirikisha Serikali ambapo alijibu kwamba hicho ndicho walichofanya na hata kugharamikia safari za maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Kiteto, Manyara na kuona mifugo kiasi gani imefariki.

“Kwa haraka haraka ninachoweza kusema [ni kwamba] mifugo zaidi ya 60,000 imekufa, anasema Mtehengerwa. Familia hazina chakula. Wafugaji kuishi kwao wanategemea mifugo. Akiwa na mifugo maana yake ana chakula, anaweza akauza mfugo wake akapata chakula. Sasa kama mifugo yake mingi imekufa maana yake hata hali ya njaa inakuwa ni kubwa kwao.”

Dk Ronald Ndesanjo ni mwanaikolojia na mtaalamu wa mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayehusisha masuala haya ya ukame na upungufu wa chakula na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia ya nchi na kubainisha kwamba hali hii si ngeni kwa wafugaji wengi kutoka kwenye maeneo yanayoripotiwa.

Mtafiti huyo anabainisha kwamba wafugaji kihistoria wamekuwa wakiishi maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa hayana mvua za kutosha na ukame unakuwepo. Hata hivyo, wafugaji hao siku zote wamekuwa wakikabiliana na hali hiyo kwa namna bora  na kwa uwezo mzuri zaidi.

Dk Ndesanjo ana mawazo kwamba tofauti pekee kati ya zamani na sasa ni kwamba maeneo mengi ambayo kwa asili yalikuwa yakitumiwa na wafugaji kwa ajili ya malisho yamechukuliwa na kutumika katika shughuli nyingine, huku mifugo ya wafugaji ikiendelea kuongezeka.

“Tuliangalie hili suala katika muktadha mpana,” anashauri Dk Ndesanjo wakati akiongea na The Chanzo. “Kwamba je, kwa asili, maeneo yaliyokuwa ya wafugaji yamekwenda wapi na kwa namna gani wanaweza wakarudishiwa ili hawa [wafugaji] wawe na uwanda mpana wa kupata malisho?”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts