The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wanaharakati Watilia Mashaka Mpango wa Serikali Kuwahamisha Wamaasai Ngorongoro ‘Kwa Hiari’

Wanaharakati siyo tu wanadai kwamba Majaliwa hakukutana na viongozi halisi wa kimila wa Kimaasai bali hata eneo analosema kuwatengea Wamaasai waliotayari kuhama Ngorongoro la kilomita za mradi 400,000 huko Handeni, Tanga, halina uhalisia.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mvutano mkali unaendelea baina ya Serikali na wanaharakati wa haki za binadamu kufuatia kauli ya Serikali kwamba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tayari amepokea orodha ya kaya za awali 86 zenye watu wapato 453 ambao wamekubali kuondoka “kwa hiari yao” kwenye Hifadhi ya Ngorongoro huku wengine wakiendelea kujiandikisha.

Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuwahamisha Wamaasai wapatao 70,000 kutoka Ngorongoro kufuatia madai ya Serikali kwamba hifadhi hiyo ambayo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linaitambua kama moja ya urithi wa dunia kuwa katika hatari ya kupotea kutokana na shughuli za binadamu.

“Zamani watu waliweza kuishi na wanyama [ndani ya hifadhi] bila tatizo kwa sababu kulikuwa na wakazi 8,000 tu wenye ng’ombe 20 hadi 30,” Majaliwa alisema baada ya kumaliza kikao na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimaasai wanajulikana kama Malaigwanan. “Leo hii, kuna wakazi 110,000 na mifugo zaidi ya 813,000, wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo.”

Majaliwa aliwaeleza viongozi hao wa kimila kwamba Serikali imetenga eneo la kilomita za mraba 400, 000 wilayani Handeni, mkoani Tanga, ambapo kati ya hizo, kilomita za mraba 220,000 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, kupima viwanja na kutenga maeneo ya malisho.

Lakini kwa mujibu wa wanaharakati wanaopigania haki za Wamaasai kuendelea kubaki kwenye hifadhi hiyo, Serikali inatumia “mbinu chafu” kufanikisha zoezi lake hilo kwa kutumia watu wasiokuwa Wamasaai wanaoishi Ngorongoro na kuwafanya wawakilishi wa wananchi hao.

Joseph Oleshangay ni mwanaharakati wa haki za binadamu anayefanya kazi na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na ambaye ni mmoja kati ya watu waliomstari wa mbele kupinga juhudi za Serikali kuwahamisha Wamaasai kutoka Ngororo.

Wamaasai wa Ngorongoro wakwepwa

Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter kufuatia tangazo hilo la Alhamisi la Serikali, Oleshangay, ambaye amezaliwa na kukulia Ngorongoro, alisema tofauti na kile Serikali inauaminisha umma wa Watanzania, mamlaka husika hazijawahi kukaa chini na Wamaasai halisi wanaoishi Ngorongoro tangu Aprili 6, 2021, pale Rais Samia Suluhu Hassan alipoagiza watu hao wahamishwe ili wasiharibu urithi wa dunia.

“Badala ya kukutana na jamii yenyewe ambayo imekuwa ikitengwa kwenye sera za Serikali kwa miaka 43 iliyopita, Rais [Samia] ameona ni bora atumie madalali wanaojifanya kuwa ni wananchi wa Ngorongoro,” aliandika Oleshangay. “Watanzania wasidanganywe kwamba jambo hili linafanywa kwa maslahi ya umma. Tunajua linafanywa kwa maslahi ya wawindaji.”

Akizungumzia suala la uhalisia wa watu ambao Majaliwa amekutana nao hapo Alhamisi, eneo la Oretei Loongaik-Marya, kwenye Chuo cha Ufundi, jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Traditional Ecosystems Survival Tanzania (TEST) Yannick Ndoinyo alisema kwamba ana mashaka watu ambao Waziri Mkuu Majaliwa amekutana nao ni Wamaasai.

TEST ni shirika lisilo la kiserikali (NGO) linalojihusisha na utatuzi wa migogoro, utunzaji wa maliasili na kuendeleza maendelezo endelevu ya watu, wanyama na mifugo katika eneo la Serengeti Mashariki.

“Katika maisha yangu yote kama Mmaasai mtu mzima sijawahi kuwaona viongozi wa kimila wakicheza mbele ya mtu yoyote,” aliandika Ndoinyo kwenye ukurasa wake wa Twitter huku akionesha watu wanaosadikika kuwa viongozi wa kimila wa Kimaasai wakicheza mbele ya Majaliwa. “Hitimisho langu la haraka, na pengine sahihi, ni kwamba hawa siyo viongozi halisi wa kimila, hususan siyo wale wanaotoka Ngorongoro.”

Hitimisho la Ndoinyo linaweza kuwa sahihi, hususan ukizingatia kauli ya Kiongozi wa Malaigwanani Ngorongoro Metui Oleshaudo ambaye amenukuliwa akisema kwamba amesikitishwa na hatua ya Serikali kuwaita Wamaasai wasioishi Ngorongoro na kupitisha azimio kuwa wamekubali kuhama, huku wakazi halisi wakiwa hawana taarifa ya kikao husika.

Kilomita za mraba 400,00 ni kubwa kiasi gani?

Utata mwengine ulioibuliwa na tangazo la Serikali unahusu ule mpango wa Serikali kuwatengea Wamaasai waliokuwa tayari kuhama kwa hiari yao eneo la kilomita za mraba 400,000 wilayani Handeni, mkoani Tanga, eneo ambalo wanaharakati wanasema ni kubwa kuliko Tanga yenyewe yenye kilomita za mraba 26,677.

“Mkoa wa Tanga una kilomita za mraba 26,677,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Edward Porokwa, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa PINGOS Forum, ambao ni mtandao wa mashirika yanayoendeshwa na watu asilia. “Imekuwaje [Mheshimiwa] Waziri Mkuu akapata kilomita za mraba 400,000 wilaya ya Handeni kuwapatia wafugaji wanaotakiwa kuhamishwa Ngorongoro?

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu hapo Alhamisi, tayari Serikali imepima kutoka kwenye eneo lililotengwa jumla ya viwanja 2,406, ambapo kati ya hivyo 2,070 Serikali imeandaa kwa ajili ya makazi na kila kiwanja kina ukubwa wa ekari tatu.

“Tumeanza na nyumba za kuanzia 101 za vyumba vitatu vya kulala kwa wale wanaotaka,” taarifa hiyo imemnukuu Waziri Mkuu Majaliwa akisema. “Tuna viwanja 336 kwa ajili ya huduma kama shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya. Ujenzi wa mifumo ya maji unaendelea. Umeme wa REA pia utakuwepo.”

Kuna uwezekano mkubwa taarifa hiyo kuhusu eneo la kilomita za mraba 400,000 ina makosa ya uandishi kwani eneo zima la Tanzania lina kilomita za mraba 945,087.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts