Dar es Salaam. Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imekosolewa kwa kushindwa kutenga fungu la kufadhili mageuzi ya msingi ya kisiasa nchini Tanzania, ikiwemo ufufuaji wa mchakato wa kuandika Katiba Mpya na mazungumzo yanayoendelea ya kutafuta maridhiano ya kisiasa nchini.
Wakiwasilisha uchambuzi wao wa bajeti hiyo hapo Jumapili kwa nyakati tofauti, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba walihitimisha kwa kusema kwamba bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni Juni 14, 2022, haina sifa hata moja ya kuitwa “Bajeti ya Wananchi.”
Uchambuzi wa bajeti kutoka vyama hivyo vya upinzani unafuatia ule uliofanywa na chama kingine cha upinzani cha ACT-Wazalendo ambacho kililalamika kwamba bajeti hiyo inawaacha wananchi wa Tanzania njia panda kwa “kushindwa kutoa mweleko thabiti” wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwenye bajeti hiyo ambayo utekelezaji wake utaanza Julai 1, 2022, Serikali imepanga kutumia jumla ya Shilingi trilioni 41.48 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo ya Serikali.
Utekelezaji wa bajeti hiyo utaambatana na kufutwa kwa ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita; kupunguzwa kwa tozo zinazotokana na miamala ya simu kwa asilimia 43; kubadilisha mfumo wa manunuzi ya umma; na kudhibiti matumizi ya vyombo vya moto vya Serikali.
Bajeti hiyo pia itaambatana na utozwaji kodi kwenye mikopo inayotolewa nje ya mfumo wa mabenki; Sh1,000 mpaka Sh3,000 kuwekwa kama ada ya king’amuzi; kuongezwa kwa ushuru wa nywele bandia pamoja na hatua zingine kama hizo.
“Huwezi kusema bajeti hii ni bajeti ya wananchi wakati wananchi wanataka Katiba Mpya na Katiba Mpya haipo kama kipaumbele kwenye bajeti ya nchi,” Mnyika aliwaeleza waandishi wa habari hapo Juni 19, 2022, katika makao makuu ya chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam.
CHADEMA wamekuwa wakiendesha kampeni mbalimbali za kudai Katiba Mpya, wakisema kwamba mchakato wa kuandika nyaraka hiyo muhimu unapaswa kuanza mara moja ili kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 Tanzania iwe na Katiba Mpya.
“Kuna kipande kikubwa cha wananchi wanataka Katiba Mpya kama nyenzo ya msingi na Katiba Mpya haijaingizwa kwenye bajeti ya Serikali,” aliongeza Mnyika. “Kwa muktadha huo peke yake hii bajeti siyo bajeti ya wananchi kwa sababu haikamilishi mchakato wa Katiba ya wananchi.”
Katika uchambuzi wake, Mnyika pia amedokeza haja ya kuwepo kwa mikakati ya kupunguza matumizi ya Serikali ili kuokoa fedha zitakazotumika kwa ajili ya wananchi.
“Ukubwa wa Serikali yetu unachangia vilevile ukubwa wa gharama za uendeshaji wa Serikali,” alisema Mnyika. “Katika mazingira ambayo taifa linapitia katika hali ngumu, na wananchi wanapita katika mazingira ya kufunga mkanda, wakati umefika sasa kwa Serikali kutekeleza mapendekezo yetu ya muda mrefu ya kupunguza ukubwa wa Serikali ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.”
Naye Profesa Lipumba, wakati akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni, Dar es Salaam, mnamo Juni 19, 2022, alieleza masikitiko yake juu ya kushindwa kwa bajeti hiyo katika kuonesha nia ya kuhitaji mabadiliko ya kidemokrasia kutokana na kutotenga fedha kwa ajili ya michakato ya Katiba Mpya na Tume huru ya Uhaguzi.
“Ukisikiliza ile hotuba haya mabadiliko ya ujenzi wa demokrasia hayakuguswa kabisa,” alisema Profesa Lipumba ambaye ni mchumi kitaaluma. “Hakuna mwelekeo wowote kwamba kuna fungu limetengwa kuweza kushughulikia suala suala zima la ujenzi wa demokrasia.”
CUF pia imekosoa mpango wa Serikali wa kuunganisha vitambulisho vya taifa na mchakato wa ulipaji kodi, ikisema kwamba hatua hiyo itapunguza ari ya wananchi kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho vya taifa. Profesa Lipumba amesema hatua hiyo ikitekelezwa ni sawa na kurejesha kodi ya kichwa kinyemela.
“Usivihusishe vitambulisho vya taifa na kodi kwa hivi sasa wakati ambapo watu hawajapata hivyo vitambulisho,” anaonya Profesa Lipumba. “Mwishoni hata watu watakuwa hawaendi tena kujisajili, kwamba mtu atatafsiri kwenda kujisajili kupata kupata kitambulisho [cha utaifa] ni kwenda kujisajili kupata namba ya usajili wa mlipa kodi (TIN).”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.