Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ameeleza kwamba Serikali ya awamu ya sita inapanga kuendeleza juhudi zake za kutatua changamoto kubwa zinazowakabili waandishi wa habari pamoja na tasnia nzima kwa ujumla ili kutengeneza mazingira wezeshi ya utoaji wa habari zenye tija nchini.
Nnauye amebainisha hayo leo Juni 29, 2022, wakati akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) iliyopo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) iliyolenga kujadili ushiriki wa SJMC katika tasnia ya habari nchini.
“Serikali imefungua milango kwa ajili ya mijadala na mjadala hasa wa wadau hasa kuhusu maboresho ya sheria za huduma ya habari na vyombo vya habari ya mwaka 2016 na pia kuweka mzingira bora ya utendaji kazi wa vyombo vya habari kwa ajili ya huduma kwa wananchi na maendeleo ya taifa,” alisema Nnauye.
Nnaye, ambaye pia ni Mbunge wa Mtama (Chama cha Mapinduzi – CCM), alisema kwamba Serikali itaendelea na mikakati ya kuhakikisha kuwa inaweka wazi fursa ya watu kutoa habari na maoni ambapo suala hili limeshaanza kutekelezwa baada ya Serikali kuvifungulia baadhi ya vombo vya habari ambavyo vilikuwa vimefungiwa kuendesha shughuli za kutoa habari.
“Mnakumbuka Serikali imefungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa,” anaeleza Waziri Nnauye. “Serikali inafanya juhudi za kufungua fursa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha zaidi tasnia hii katika kuhakikisha unakuwepo uhuru zaidi wa habari na kutoa maoni.”
Nnauye ametaja baadhi ya changamoto zinazoikabili tasnia ya habari nchini ambazo ni pamoja na taaluma ya habari kutokuwa na hadhi na heshima kama ambavyo ipo kwenye taaluma nyingine; ujira mdogo kwa wafanyakazi wa tansia ya habari pamoja na kufanya kazi bila mikataba; pamoja na kuendelea kupungua kwa kasi ufanyikaji wa habari za kiuchunguzi.
“Bado hatujafanikiwa sana kuifanya tasnia ya habari ionekane ni taaluma yenye hadhi na heshima kama zilivyo taaluma nyingine nchini, bado kwa mfano tupo kwenye hali ambayo kosa la mwandishi mmoja linaweza kuhesabiwa ni kosa la chombo kizima cha habari,” alisema Nnauye.
Akizungumza katika mjadala ulioandaliwa katika kongamano hilo Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Joyce Shebe amebainisha kuwa kwa sasa tansia ya habari inakabiliwa na upungufu wa wanawake wanaoshiriki kuzalisha maudhui licha ya uwepo wa wanafunzi wengi wa kike wanaosomea taaluma hiyo.
“Kiukweli ushiriki wa wanawake kwenye vyombo vya habari hauridhishi,” alisema Shebe ambaye pia ni mhariri wa Clouds Media Group. “Ila tukirudi kwenye madarasa ambayo yanatufundisha vyombo vya habari, idadi inaridhisha lakini huku sasa kwenye utendaji hatuwaoni kwa idadi ile ambayo tunawaona kwenye madarasa au kwenye vyuo.”
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji nchini (TBC) Dk Ayub Rioba alisema kwenye kongamano hilo kwamba kwa sasa habari za uchunguzi hazifanyiki kutokana na hatari kubwa waandishi wanazoweza kukabiliana, akisema jambo hilo linashusha thamani na mchango wa vyombo vya habari kwa wananchi na jamii nzima kwa ujumla.
“Ni kweli kabisa tunaona kwamba habari za uchunguzi hazifanyiki,” alisema Dk Rioba. “Lakini kama ukitaka vyombo vya habari vionekane kwamba vinathamani, vina mchango muhimu kwa maisha ya watu, naamini kabisa kwamba [habari za uchunguzi] zinapaswa kupewa uzito.”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.