The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

John Heche: Ugonjwa Unaoitesa Tanzania ni Uongozi M’bovu

Ataka mifumo na taasisi ziwekwe ambazo zitahakikisha watawala wanawajibika kwa wananchi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kiongozi mwandamizi wa chama cha upinzani CHADEMA John Heche ameeleza kwamba tatizo kubwa linaloizuia Tanzania isipige hatua za maendeleo ni uongozi ambao amesema hauwajibiki kwa wananchi.

Heche, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, alitoa tathmini hiyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika hapo Octoba 3, 2022, katika ofisi za The Chanzo zilizopo Msasani, Dar es Salaam.

Heche anashauri kwamba ili Watanzania waweze kupata maendeleo wanayostahiki ni lazima mifumo na taasisi ziwekwe ambazo zitahakikisha watawala wanawajibika kwa wananchi hao.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo kati ya The Chanzo na John Heche:

The Chanzo: Ni nini kilikusukuma kuibua hoja hii ya madeni na pesa ambayo Tanzania inaitumia kurejesha haya madeni?

John Heche: Kwanza, kumekuwa na uelewa mdogo sana wa watu wetu kuhusu masuala ya deni la taifa. Mtu wa kawaida, Mtanzania ambaye anauza miwa, au anauza nyanya, au machinga, au nani kwenye nchi hii, hawajajua kabisa jinsi ambavyo deni la taifa linahusiana na maisha yao ya kila siku.

Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikitumia mwanya huo kukopa na kukopa na kukopa. Kwa sababu kuna kisingizio kimoja ambacho siku moja Waziri wa Fedha [Mwigulu Nchemba] alisema kwamba hakuna mtu ataenda kukugongea, wewe Khalifa [Said, mwandishi The Chanzo] kama wewe nyumbani kwako kukudai deni la taifa.

Kwa hiyo, watu wamekuwa wanafikiri kwamba hilo deni sisi halituhusu, [kwamba] linaihusu Serikali [kwani] ndiyo inayokwenda kukopa. Lakini deni haliwagusi wao. Kwa hiyo, kumekuwa na uelewa mdogo na elimu ndogo sana kuhusu masuala ya deni la taifa na namna ambavyo linavyoathiri maisha ya wananchi wa kawaida.

Na kwa sababu hizo, ni muhimu sana tukaanza kuwaelewesha wananchi namna ambavyo ukopaji, au madeni haya, yanavyoumiza maisha yao kila siku. Wewe mwenyewe umesema tunalipa asilimia 40 ya kile tunachokusanya. Asilimia 40 ya kile tunachokikusanya.

Ukiangalia mapato ya Tanzania kwa mwezi, kiuhalisia, sijui hiyo asilimia 40 wewe umeiangalia vipi. Kwa sababu, ukisoma bajeti ya mwaka huu, kwanza deni letu la taifa limefikia Shilingi trilioni 69. Kuna deni la ndani na kuna madeni ya nje.

Hapo ni kabla ya haya mamikopo ambayo Rais [Samia Suluhu Hassan] amekopa halafu akasema mama nimeenda kuzunguka zunguka huko [nje ya nchi], nimerudi na kitu, alitumia hiyo kwamba nimeenda kutembea tembea huko sijarudi mikono mitupu na siku hizi wakienda huko [nje ya nchi] wanarudi wanapongezana. Hiyo ni kabla.

Kwa hiyo, deni la taifa inawezekana limefika karibia-, kwa sababu mwezi Aprili wakati Mwigulu anazungumza lilikuwa Shilingi trilioni 69 kama nilivyokwambia. Na ukiangalia, ukisoma bajeti ya mwaka huu ya fedha, Serikali imetenga kama Shilingi trilioni 9.8 kulipa deni la taifa. Sasa ukigawa kwa mwezi ni kama bilioni 600 na kitu, 700 mpaka 800 ambazo tunalipa deni la taifa.

Na ukichukua makusanyo ya nchi, ukichukua makusanyo yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mwezi, TRA inasema tumekusanya trilioni 1.2, trilioni 1.3. Kama [TRA] wanakusanya trilioni 1.3 au trilioni 1.2, bilioni 800 au 700 na kitu zinatumika kulipa deni la taifa.

Kwa hiyo, Serikali inakusanya Shilingi trilioni 1.3, Shilingi bilioni 800 inalipa deni la taifa, inabaki kama bilioni mia tano na kitu na mia sita, siyo? Ukitoa elimu bure ambayo tunaambiwa kwamba wanatumia Shilingi bilioni 30 kwa mwezi, inabaki bilioni 500 na kitu. Ukichukua mishahara ya walimu, askari na nini kila kitu kimeisha. Sasa unaendeshaje uchumi sasa hapo?

Ndiyo tunakuja sasa kwenye jinsi ambavyo hili deni [linavyoiathiri] nchi yetu. Yaani unakuwa kwenye ufukara na unakuwa kwenye hiyo hiyo mizunguko ya ufukara. Huwezi kujitoa humo. Kwa sababu kama unakusanya pesa na zote zinaingia kwenye matumizi huwezi kutunza, huwezi kuanzisha mradi mpya.

Ili Serikali ianzishe mradi, ni lazima tena ikakope ili ije ianzishe mradi, ianziishe barabara, iweke maji, ifanye nini. Kwa sababu fedha zingine zote wanazokusanya [zinalipa madeni]. Na hapo hatujazungumzia mafuta [watu wa Serikali] wanayotumia kwa mwezi. Hatujazungumzia za maofisi. Hatujazungumzia magari.

Ukiangalia bajeti ya mwaka huu Mwigulu amesema Serikali inatumia kwa mwaka Shilingi bilioni 558 za kununua magari ya viongozi, V8 hizi wananunua mpaka wilayani. Kwa hiyo, ndiyo maana sasa, leo tunahitaji walimu kwenye shule. Vijana wapo wamemaliza shule. Wapo mtaani, siyo kwamba hawapo. Wapo. Hata tukisema leo hii shule zote zijae walimu kama tuna fedha wanajaa.

Hatuna upungufu wa walimu. Watu wamemaliza kuanzia mwaka-, [Rais wa awamu ya tano John] Magufuli aliingia [madarakani] mwaka 2015, hakuajiri [walimu]. Tangu mwaka 2015, acha wale ambao [Rais wa awamu ya nne Jakaya] Kikwete alikuwa anaajiri wanabaki kidogo.

Magufuli hajaajiri tangu mwaka 2016, 2017, 2018 aliajiri kidogo, kidogo sana na mwaka huu ndiyo Serikali ikatangaza ajira. Ilikuwa mwezi wa ngapi? [Serikali] ilitangaza ajira kama 11,000. Maombi, watu walioomba, walikuwa watu 600,000 mpaka wakafunga mfumo, yaani umezidiwa. [Wanatakiwa] watu 11,000, wameomba 600,000.

Sasa tangu kipindi hicho Serikali haijaajiri kwa sababu Serikali hawana fedha za kuajiri. Kwa sababu hii mishahara ya walimu, watumishi wa nini ndiyo hiyo deni la taifa, ndiyo hiyo elimu bure ndiyo hiyo. Sasa nini kinachobaki kwenye kuajiri?

Hatuwezi kuajiri manesi wa kutosha. Hatuwezi kuajiri madaktari. Hatuwezi kujenga madarasa. Tunasubiri tutoze tozo. Hatuwezi kujenga madarasa tunasubiri pesa za UVIKO-19. Wengine walizipeleka pesa za UVIKO-19 ambazo walipewa na Benki ya Dunia wengi walizipeleka kwenye kujenga uchumi wao uanze kukua.

Kenya waliweka kwenye maviwanda watu wenye viwanda ndiyo walioenda kukopa ili uchumi uanze kukua ajira ziwepo. Sisi tulipeleka kujenga madarasa kwa sababu hatuna fedha. Fedha nyingi zinakwenda kwenye kulipa [na] kupunguza deni. Kwa sababu usipowalipa hawa wazungu wanakufungia mikopo na wewe huwezi kujiendesha. Sasa wakikufungia huwezi kupeleka bakuli uwe omba omba huko wakishakufungia umeisha.

Kwa hiyo, kitu cha kwanza ambacho watu wa Serikali ambacho wanahakikisha wamefanya ni hela ya wazungu wakawalipe madeni waliyokopa. Ndivyo hivyo deni la taifa linavyoathiri mwananchi wa kawaida.

Huwezi kujenga barabara mpya. Huwezi kupelekea watu maji. Watoto wako walioko mitaani hawawezi kuajiriwa kwa sababu fedha nyingi zinatumika kulipa deni la taifa. Kama tungekuwa tunakusanya hizi fedha zote na zipo zingekuwa zinabaki Tanzania kwenye mzunguko wetu tungeweza kufanya haya mambo.

Lakini watu waliopo madarakani hawana upeo. Wao ni kukopa na kuongeza deni na deni linaongezeka kuwa kubwa zaidi.

The Chanzo: Lakini sasa tunakopa kufanya nini? Kwa sababu, kwa mfano, kama mimi nikiwa nakopa unakuja kuanzisha biashara, biashara inaendelea, hakuna ubaya kurejesha mkopo wa watu kwa sababu hivyo ndivyo maisha yalivyo. Si kila mtu anajitosheleza. Sasa sisi, kwa mfano, kama nchi, tunakopa kufanya nini na hivo vitu vipo?

John Heche: Swali zuri sana. Hapo sasa ndiyo tatizo linapokuja. Nimekwambia kwa sababu wananchi hawafuatilii hizi pesa zinazokopwa, na kwa sababu hizi pesa zinakuja kwa pamoja, watu walioko serikalini wanaziona kama ni pesa wamepewa hisani.

Ndiyo hapo sasa kwamba-’. Mimi juzi nilikuwa Italia. Waziri wa Italia anakuja kwenye kufungua mkutano, anakuja na baiskeli, anakuja anaendesha baiskeli, halafu wewe unamkopa, wewe unatumia [gari aina ya] VXR ya mwaka 2022.

Mwananchi wa kawaida Tanzania, wafanyabiashara wakubwa hawa, hawawezi kununua magari hayo mapya. Lakini waziri na wakuu wa wilaya na wakuu wa idara, unakwenda kwenye wizara kuna mtu anaitwa Katibu Mkuu ana gari VXR. Kuna wakurugenzi, wakuu wa idara, nani, waziri wake, manaibu waziri.

Njoo mpaka wilayani, mkuu wa wilaya ambaye kiuhalisia ukiniuliza mimi hana kazi yeyote, anatembelea VXR. Huduma ya hii gari ni balaa. Kwa hiyo, unakopa kwenye kufanyia kazi ambayo siyo ya uzalishaji.

Na nataka nifafanue hili jambo kwa sababu limekuwa linaleta maswali mengi sana kwa watu wasiojua. Suala la magari mimi nimekuwa nikiandika sana kuwauliza watu wa Serikali kuhusu matumizi ya umma.

Sasa kuna watu wasiojua, wengine wanajua lakini wanapotosha, wanatumiwa na watawala au wanajipendekeza waonekane, mtu anakuandikia anasema, “Mbona wewe ulipokuwa mbunge hukupinga kutumia magari ya VX?”

Kuna tofauti kubwa kati ya gari inayotumiwa na mbunge na gari inayotumiwa na Waziri. Unapokwenda bungeni unakopeshwa pesa wewe kununua gari unayotaka wewe. Lakini kuna ukomo. Wakati sisi tunaenda ukomo ulikuwa Shilingi milioni 90. Ndiyo pesa ya ukomo, milioni 90, huwezi kukopa zaidi ya hapo.

[Hii ni] ya gari na hiyo hela unakatwa kwenye mshahara wako, unalipia lile gari, lile gari likiharibika Serikali hailitengenezi, unatengeneza wewe. Ndiyo maana pale bungeni kuna wabunge wengine wanatumia gari za kawaida kabisa, kuna wengine hawatumii kwa sababu hiyo mizigo, huo mzigo kwanza wa deni. Pili wa kuendesha hilo gari, huduma, vipuli, tairi kila kitu inakuwa ni hela yako mwenyewe.

Gari la waziri, gari la mkuu wa wilaya, gari la nani la viongozi wa Serikali yote kuanzia tairi, dereva huduma yake ya kila mwezi inatumika pesa ya mlipa kodi maskini. Kwa hiyo, narudi pale uliposema kwamba tunakopa pesa nyingi lakini hazionekani ziko wapi na zimefanya nini.

Kwa sababu tukijiuliza kuacha madeni ambayo tumelipa yote kwa mwaka ni kama bajeti ya mwaka huu ilikuwa ni kama trilioni 30 na kitu, sasa tunadaiwa mara mbili, yaani deni tulilonalo ni bajeti yetu ya miaka miwili ikiwa imejumuisha kila kitu.

Nikisema inajumuisha kila kitu maana yake ni kwamba unajua sisi kwa bajeti yetu tunapanga maoteo, tofauti na ulaya au Marekani. Marekani wanapanga bajeti tayari wana fedha. Wakisema tutajenga barabara kutoka Sinza mpaka hapa ofisini pesa inakuwa imeshapelekwa.

Sisi, unaotea. Unasema tutajenga barabara kutoka Sinza mpaka hapa Kinondoni, tutajenga hospitali Sinza, tutafanya nini, tutafanya nini halafu baadaye unaenda kuomba mkopo kwa wazungu. Yaani, una bajeti halafu huna mia, halafu unaenda kuomba mzungu.

Mzungu akikunyima, [umekwama]. Kwa mfano, sasa hivi [Ulaya] wana ugomvi, wazungu wanapigana kule na [Rais wa Urusi, Vladmir] Putin. [Putin] amevuruga dunia. Kwa hiyo, wanakwambia sisi hatuna hela, hela zote tunaelekeza kwenye vita.

Kwa hiyo, mpango wako uliopanga hautekelezeki. Ndiyo maana ukiangalia vitu vingi ambavyo Serikali inapanga vya kibajeti havitekelezeki, wanatekeleza tu labda asilimia 40, asilimia 30 kwa mwaka.

Kwa hiyo, hoja ni kwamba kukopa siyo tatizo tungekuwa tunakopa na tunajiwekeza sehemu sahihi, kwenye miradi sahihi, ambayo baada ya muda hiyo miradi ingeanza kuzalisha, kwa sababu hupaswi kuwa kwenye mizunguko ya kukopa, na kukopa na kukopa.

Kwa sababu hata unavyokopa kwenye mabenki, unapofanya biasahara, unatakiwa unakopa huku unakua siyo deni linaongezeka. Kwa mfano, Mwigulu anasema mwezi Aprili alipokuwa anahutubia Bunge anasema deni liliongezeka kwa asilimia 14.

Kwa hiyo, deni la taifa lilikuwa kwa miezi mingapi, kwa mwaka wa bajeti mwaka jana 2021, deni lilikuwa trilioni 60, mwaka huu lipo trilioni 69. Bajeti itakayosomwa mwaka huu litakuwa kubwa zaidi kwa sababu Mama [Samia Suluhu] kila siku anakopa tunaambiwa.

Mama sijui yuko wapi amepewa sijui trilioni ngapi watu wanapiga makofi. Siyo za bure. Ni pesa za mikopo. Sasa zinawekezwa kwenye nini ndiyo hizo sasa zinatumiwa kwenye vitu visivyoileweka.

Ukiaangalia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka huu inasema kuna upotevu wa pesa zaidi ya trilioni tano, yaani hazikuwa zimehesabiwa, yaani matumizi yalifanyika lakini hakuna risiti. Hakuna.

Kwa mfano, wanasema tulichimba kisima. Hicho kisima hakionekani. Wanasema labda tulifanyia huduma ya gari, risiti za hiyo huduma hazipo. Kwa hiyo, ndiyo hizo sasa tunakopa zinaingia kwenye mifuko ya watu na matokeo yake ni athari kubwa zaidi.

The Chanzo: Mkopeshaji huwa hajali, yaani hajali kwamba pesa unayomkopa unaenda kuifanyia nini? Kwa mfano, tuchukulie mtu kama Benki ya Dunia, au taasisi nyingine za ukopeshaji, au mataifa mengine tajiri ambayo yanaikopesha Tanzania, huwa hayajali Tanzania inakopa kwenda kufanya nini, na pengine kuna ufuatiliaji wowote labda kuhakikisha kwamba kile ambacho Tanzania imesema imekopea inaenda kukitekeleza?

John Heche: Wazungu, nikitaka kutumia neno sahihi, wazungu wangependa Waafrika waendelee kuwa masikini ili watumie umasikini wao wa Waafrika kujiendeleza zaidi wao. Ujinga mwingi sana unaofanywa na viongozi wa Afrika, wanafanya ufisadi mkubwa, wananunua majumba kule wanafanya nini, wanajenga mahoteli Ulaya na nini, inawafaidisha wao [Wazungu].

Mabenki, Benki ya Dunia, kwa mfano, benki kama IMF, IMF ni benki ambayo inamilikiwa na nchi tajiri, wamewekeza mtaji wao. Wewe Khalifa unaenda, unakopa kwa masharti mnayokubaliana na unarudisha na riba. Sasa wewe kama unanikopa mimi, unarudisha na riba mimi nafuatilia nini? Unacho wewe, tumia vibaya kwa sababu ukitumia vizuri utakuwa na uchumi hutakuja kukopa.

Kwa hiyo, ukitumia vibaya unabaki kwenye mzunguko wa umasikini, unaendelea kukopa. Lakini wao wanaweka masharti, kwa mfano, chanzo cha haya mambo yanayoitwa tozo ni Serikali yetu kupewa mashariti na IMF kwamba ione namna ya kuchaji watu tozo kwenye miamala, kwenye vifaa vya umeme, hizi nini na nini. Yaani ni maelekezo yalishushwa Serikali ikachukua kutoka kwa wao wazungu, kwa sababu mtengeneze hela ya kulipa madeni yetu.

Kwa hiyo, kama mkopeshaji wewe unakopa na mimi nina uchumi naweza kukukopesha leo ulikuwa na viatu, unauza unanipa, unabaki bila viatu. Kesho unakopa unauza nguo yako unabaki na shati. Kesho kutwa ukikopa utauza na figo, yeye anaendelea tu kwa sababu hakuna huruma kutoka kwa bepari, hakuna huruma kutoka kwenye dunia ya kibepari.

Hii ni dunia ya ushindani. Nini unachopeleka? Watu wako wana akili kiasi gani? Watu walioko serikalini wanasaini mikataba ya aina gani? Ndiyo hivyo. Na ukweli wa Mungu mimi nimewaambia Watanzania na narudia tena leo, nimejiridhisha bila shaka yoyote [kuwa] hatutaondoka kwenye matatizo haya, kiuhalisia tutazidi kudumbukia kwenye matatizo zaidi, kwa uongozi wa Chama cha Mapinduzi [CCM].

Kwa miaka 62 wamejaribu, wameshindwa. Hawana uwezo. Ukitaka kujua hawana uwezo, kaka, CCM wanafanya chaguzi za wilaya si ndiyo? Ngazi ya wilaya si ni viongozi wakubwa? Ni wilaya gani umesika mwenyekiti anasema, mimi naomba nichaguliwe nikawe mwenyekiti wa wilaya niende kwenye kikao cha kitaifa, nikaishauri Serikali ishughulike na deni la taifa lisizidi kuwaumiza wananchi? Umesikia nani amesema hivyo?

Wanasema mimi mnichague nikapiganie chama chetu. Hawana kabisa mawazo yoyote kuhusu masuala ya nchi. Ndiyo hao wanaokuja kukutana, kwa mfano, CCM wanapenda sana kuwa na kitu kinaitwa ukuu wa chama, chama kiongoze Serikali.

Sasa kama chama kinachoongoza Serikali na ambacho kinajifanya kwamba kinaongoza Serikali hicho chama kinapaswa kuwa na watu wenye akili kwenye chama kuliko walioko Serikalini.

[Chama] ambacho kina uwezo wa kutambua kwamba kuna makosa kuliko ungetegemea kuona viongozi wa CCM wanaogombea kutoka hata kwenye wilaya wanazungumza deni la taifa, wanazungumza ufisadi, wanazungumza kuhusu maendeleo, kukwama wanazungumza vitu vinavyogusa maisha ya wananchi lakini nani umesikia anazungumzia jambo hili?

Wanafurahia kuvaa nguo za kijani na kujirundika kwenye ukumbi, kugawana rushwa kwa sababu ni chanzo cha rushwa. Kwa hiyo, hawana kitu chochote wanachozungumza kuhusu masuala ya nchi na nchi inazidi kwenda kwenye matatizo.

The Chanzo: Nilitaka kukuuliza kuhusiana na kitu kinaitwa deni himilivu, au uhimilivu, tumekuwa tukisikia hata bungeni wanazungumza deni linaongezeka lakini deni letu ni himilivu. Himilivu ni nini kinaamua au nini tunaweza kukitumia kusema kuwa hili deni ni himilivu, hili deni siyo himilivu? Na, kwa mfano, ni kweli kwamba deni letu la taifa kwa kiwango ambacho wewe umekizungumzia ni kweli ni himilivu kama ambavyo Serikali inasema?

John Heche: Kaka, nimekwambia kwanza tuna watu wasio na uwezo kabisa. Unakuwa na Waziri wa Fedha na Mipango ambaye amepata hicho cheo kwa sababu ya kuvaa nguo na mabendera ya taifa na nini. Hana uzalendo. Hana uwezo. Hawezi kututoa hapa kwa sababu hana mipango.

Ukisema deni ni himilivu maana yake nini? Kama makusanyo yako asilimia 100, asilimia 40 kabla hujaanza chochote umeshalipa deni unabaki na asilimia 60 unanielewa vizuri? Ukibaki na asilimia 60 unalipa mishahara ya watumishi na wafanya kazi zaidi ya asilimia 40 jumla, unanielewa vizuri? Hujaingia kwenye OC.

The Chanzo: OC ni nini?

John Heche: [OC ni] pesa za matumizi za kuendesha ofisi, zile ambazo, kwa mfano, kama ulisikia juzi wanazungumza watapunguza chai kwenye maofisi, chai, sijui vitumbua, kununua magari, kuweka mafuta ya magari, huduma za magari. Yale matumizi ya kawaida ya ofisi, yale ya kuendeshea ofisi, kununua rimu na vitu kama hivyo.

Kuna kitu kinaitwa elimu bure ya bilioni 30. Sasa uhimilivu wake uko wapi? Kwa sababu kama lingekuwa himilivu si zingebaki pesa za maendeleo? Sasa kwa ajili ya maendeleo kwamba tumetumia kwa sababu hata wewe nyumbani kwako, bajeti tu ya kawaida ya nyumbani kwako, huhitaji kutambua hili jambo kwa kutumia mfano wa Serikali.

Kama wewe Khalifa mshahara wako unautumia kwenye kulipa madeni na kwenye matumizi ya anasa, huwezi hata kununua tofali, watoto wako wanakuona wewe ni baba wa aina gani?

Kwa sababu kwenye mshahara wako unapaswa ufanye mambo mengine yote lakini uwe na uwezo wa kubakiza ununue kakiwanja leo, kesho kutwa ununue tofali, siku nyingine ununue simenti, uweke vyumba viwili kama hivi za watoto wako kukaa hapo, [hayo] ndiyo maendeleo.

[Mwanazuoni wa Kiafrika] Walter Rodney anasema maendeleo ni mchakato wa pande nyingi. Umetoka kwenye hatua moja umeenda kwenye hatua ile. Lakini mtu anakwambia deni ni himilivu, na bungeni una wabunge kama Jah People, yule sijui wa Njombe, una watu kama kina Munde Tambwe, ndiyo wamejaa kule.

Asilimia 90 [ya wabunge waliopo bungeni] hawawezi hata kusoma kitu kilichoandikwa kwenye karatasi. Kwa hiyo, wanakuja wanaambiwa kwamba deni ni himilivu, [wabunge] wanapiga makofi. Hawaelewi maana ya mambo haya kwenye maisha ya mwananchi wa kawaida ni mabaya zaidi.

Athari ya deni la taifa ni kuwanyima vijana wetu ajira. Ni kuinyima nchi yetu maendeleo. Ni kushindwa kufikia ndoto zetu kama nchi kwa sababu kila kitu tunachokusanya asilimia arobaini kinakwenda kwenye kulipa deni ambalo watu wamekopa na wakatumia vibaya na wanazidi kukopa.

The Chanzo: Mtu anaweza kujiuliza, unajua hata mimi najiuliza, iliwezekana vipi yaani kwa Tanzania ikajikuta ipo kwenye mzigo huo mkubwa wa madeni. Yaani, imewezekana vipi yaani tuna watu, wananchi wapo, vyama vya upinzani mpo, Asasi za Kiraia zinazohusika na masuala ya uwajibikaji zipo. Inawezekana vipi-, Chama cha Mapinduzi kipo ambacho umesema ndiyo chama kikuu kinaiongoza Serikali. Iliwezekana vipi unakuta kwamba Serikali inajikopea, inajikopea tu na sisi sote tupo mpaka inafikia hatua hii madeni haya yanaathiri maisha yetu?

John Heche: Inawezekana kwa sababu wananchi, Watanzania, wamekubali. Wamekubali kuingia kwenye uongozi wa hovyo. Watu wanajiteua. Kwa mfano, uchaguzi uliopita, kuanzia uchaguzi wa Serikali za vijiji, Magufuli alipora uchaguzi na Serikali yake yeye ndiyo aliamua Khalifa akawe mwenyekiti wa mtaa huu, wewe fulani kawe mwenyekiti wa mtaa ule. Watu ambao wananchi walitaka wawaongoze hawakuingia madarakani.

Kaja kwenye ubunge, akafuta wabunge wote ambao wananchi waliwataka, madiwani wote na Rais waliyemtaka. Kwa hiyo, hii nchi imegeuka mali ya mtu. Kwa mfano, kuna mfano leo [Oktoba 3, 2022], umejitokeza mzuri sana wiki iliyopita.

[Rais wa Kenya] William Ruto alipochaguliwa, amechaguliwa kuwa Rais, hakuapishwa siku ile, wakaenda mahakamani, ukafanyika mchakato, Mahakama ikachukua muda kama wa wiki mbili, tatu, Mahakama ikamaliza kesi, ndiyo William Ruto akaja akaapishwa.

Juzi ametangaza baraza lake la mawaziri yeye ana mamlaka ya kukuteua, kukupendekeza, kwamba Khalifa [napendekeza awe wa waziri wa kitu fulani]. Baadaye unaenda bungeni kwa sababu wanaamini Bunge ni chombo cha wananchi, kimechagua mtu sasa, unakuja wewe mwenyewe pale bungeni.

Bwana Khalifa njoo, waziri mteule, Rais amekupendekeza uwe Waziri wa Fedha. Lakini sisi wabunge, mimi nasimama, kutoka Tarime, huyu anasimama kutoka wapi wapi. Wewe Khalifa tunakujua wewe ni mwizi. Ulipokuwa mkurugenzi kwenye ofisi fulani, ofisi yako lilitokea tatizo hili ripoti ya CAG hii hapa unasemaje? Unajieleza.

Wewe bwana umewahi kufanya hivi. Wewe bwana uadilifu wako upo kwenye matatizo. Wewe bwana Rais amekuteua kwa sababu wewe ni mjomba wake, huna uwezo wa kuwa Waziri wa Fedha kwa sababu Waziri wa Fedha kazi zake ni hizi.

Au wewe tuambie malengo yako na mpango wako kama Waziri wa Fedha ni yapi, kwa sababu Waziri wa Fedha ndiyo waziri wa tatu, yaani baada ya Rais anafuata Makamu wa Rais, anafuata Waziri Mkuu halafu anafuata Waziri wa Fedha, ndiyo Waziri wajuu kabisa, ndiyo ana mipango yote ya nchi, ndiyo anamatumizi yote ya nchi.

Anapaswa kuwa na uwezo mkubwa na mipango kwamba mimi bwana, kwa mfano, bandari ya Dar es Salaam haitumiki sawasawa, nikiwa Waziri wa Fedha-’. Leo ukiangalia bandari ya Dar es Salaam, kwa mfano, huu ni mfano halisi kabisa natoa, imepitisha mizigo tani milioni 17 mwaka 2021, tani milioni 17.

Bandari ya Mombasa imepitisha tani milioni 34.5, kumbuka sisi tupo karibu na Kongo kuliko Mombasa. Sisi tuko karibu na Zambia kuliko Mombasa. Hizi ni nchi ambazo tunaziduhumia. Sisi tuko karibu na Malawi kuliko Mombasa. Sisi tuko karibu na Rwanda kuliko Mombasa. Sisi tuko karibu na Zambia, Rwanda, Burundi, Kongo zote tuko karibu nazo kuliko Mombasa.

Inakuwaje bandari ya Mombasa ipitishe mzigo mara mbili zaidi ya bandari yetu sisi? Au, kwa mfano, sisi tuna bandari Tanga [na] Mtwara. Inakuwaje Khalifa, mafuta yanakuja yanafika bandari ya Dar es Salaam yanasafirishwa kwa magari kwenda Tanga, kwenda Kaskazini mikoa ya Kaskazini, Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara?

Wanaenda kununua mafuta kwa bei ya juu wakati mafuta yangesafirishwa kupitia bandari ya Tanga, magari ya Arusha yangechukulia mafuta Tanga?

Tumefika hapa kwa sababu ya watu wanaoteuliwa hata kama hana uwezo, akiwa mjomba wa Rais, Rais amevutiwa na yeye, akiwa mototo wa dada yake, akiwa binamu yake, hata kama hana uwezo wa kuwa kitu chochote [Rais] akishakuteua ndiyo unaenda kukaa pale.

Lakini wenzetu Kenya nimekuambia wiki mbili zilizopita Rais ameteua mawaziri, watapita bungeni wiki hii, watahojiwa kama kuna mtu Bunge litamkataa itabidi Rais apendekeze mtu mwingine.

Lakini jana [Oktoba 3, 2022], sisi Rais hapa kateua mtu siyo mbunge, yaani kamteua kamfanya kuwa mbunge, leo kamuapisha. Yaani, jana hiyo hiyo kamteua nafasi mbili, yaani kamteua ubunge na kamteua na uwaziri halafu leo kamuapisha ni Waziri. Sasa katika mazingira hayo tunashindwaje kufika hapa?

Pili, angalia usawa wa malipo. Sisi tunazalisha nini na tunauza nini nje ya nchi. Ukilinganisha na tunachoingiza, kwa sababu hapa ndipo penye mchezo wote. Kama wewe Khalifa una nchi kama ya kwetu, Mungu ametujalia kila kitu, ardhi tuliyonayo, ardhi, tuna ardhi ekari milioni 29.5 inayolimika, sisi tunauwezo wa kulisha nchi zote za Kusini mwa Jangwa la Sahara tukilima vizuri.

Tuna uwezo wa kulisha nchi zote hizo. Sisi wenye ardhi kama hiyo, sisi ambao tuna nguvu kazi kubwa kama nchi, vijana wazuri, tuna lugha moja kama ya Kiswahili ambayo inatuunganisha na watu wote, nchi nyingine unakuta watu wanaongea, kama Cameroon, wanapigana baadhi ya sehemu wanaongea Kiingereza, eneo lingine wanaongea Kifaransa wanapigana kwa sababu ya lugha hiyo lakini sisi tuna lugha moja inayotuunganisha.

Tuna hekta milioni 29, tunaagiza ngano kutoka nje ya nchi asilimia 90, kiuhalisia kuna mzee mmoja wa CCM aliniambia juzi, sitamtaja, kwamba nchi moja wapo tunayoagiza ngano ni kutoka Saudia Arabia. Yaani sisi Tanzania tunaagiza ngano kutoka jangwani, yaani ukimuuliza Bakhresa atakwambia anakwenda kuchukua ngano Saudia Arabia.

Asilimia 70, nimekwambia tunaagiza ngano asilimia 90, asilimia 70 kati ya hiyo ngano tunaagiza kutoka kwenye nchi ya Ukraine na Urusi. Kwa hiyo, kwa mfano, sasa hivi Urusi wanapigana na Ukraine wananchi wetu wataanza kufa njaa.

Sasa katika mazingira hayo unashindwaje kufika hapa? Lazima tuwe na uwezo wa nchi kuzalisha, kuwekeza kwenye uzalishaji hasa kilimo, ili tuweze kuweka mizania. Pesa nyingi ambazo tunatumia kwenye kuagiza vitu kama ngano ambayo tunaweza kujilimia, hiyo pesa ibaki kwenye mzunguko hapa. Mafuta ya kula mikoa hii ya Singida, Dodoma tuwekeze kwenye mafuta ya kula.

Ukimsikiliza [Waziri wa Kilimo] Hussein Bashe [anaonekana] ni mtu ambaye ana ari ya kutaka kufanya kitu. Lakini sasa yuko kwenye kundi ambalo hawezi kufanya vitu anavyofikiria kufanya. Hawezi kuwekeza kwenye kilimo kwa sababu kusema tu ni kusema lakini tunakuja kwenye uhalisia sasa kwamba bajeti yake ni kiasi gani?

Umempa bajeti kiasi gani? Tangu vita ya pili ya dunia bidhaa pekee ambayo haijawai kushuka bei ni bidhaa ya nyama. Sisi Tanzania, nchi kama Botswana inasafirisha nyama kuliko sisi, Botswana nusu ya nchi hiyo ni jangwa.

Namibia kwenye jangwa la Kalahari pale wanasafirisha nyama kuliko sisi. Wana watu milioni 2.5. Namibia wana ng’ombe zaidi ya milioni 10. Yaani ng’ombe ni mara nne ya watu waliopo Namibia. Ndiyo nchi pekee Afrika ambayo imeruhusiwa kuuza nyama moja kwa moja kwenye soko la Marekani kwa kufikia vigezo vyao.

Namibia sisi mwalimu aliacha kiwanda kama cha Tanganyika Packers leo kimegeuka kuwa eneo la mtu kusalia. Badala ya kuwa eneo la uzalishaji pale kungekuwa na vijana 20,000 wameajiriwa. Kungekuwa na ngozi zinarekebishwa pale, zinasafirishwa kwenda kutengeneza mikanda, nyama ukienda kwenye maduka makubwa ya Uingereza unakuta bidhaa ya Tanzania ya nyama.

Ni eneo kuna mtu yule anaitwa nani vile? Boniface Mwamposa. Yule anayemwagia watu wanunue maji wataenda mbinguni. Mwaposa ndiye anayesalisha pale. Ukienda kiwanda cha nyama alichoacha Mwalimu [Julius Kambarage Nyerere] Shinyanga vyote ni maghala.

Katika mazingira kama hayo unatengenezaji uwiano wa malipo kwenye nchi yako? Ukimuuliza Rais, Rais Samia nini, nini mwelekeo wako, unataka kupata nini baada ya miaka yako serikalini? Haki ya Mungu mimi nafikiria Rais yupo amalize muda wake.

Sidhani kama ana kitu cha wazi kabisa ambacho kinajitambulisha kwamba mimi baada ya miaka mitano nimekuta watu milioni ngapi ni masikini, nataka nikitoka kuna ile malengo ya jumla na malengo mahususi.

Nataka niwe nimepata hiki, nataka niwe na vijana kadhaa ambao wametoka kwenye umasikini. Nataka niwe na vijana kadhaa, niwe nasafirisha labda ng’ombe, nyama ya ng’ombe. Niwe nasafirisha madini kwa kiwango hiki. Sidhani kama hiyo Serikali, hii Serikali [ya Rais Samia Suluhu] inacho hicho kitu.

The Chanzo: Ana R nne. Rais ana R nne.

John Heche: Hiyo tu ya maridhiano ni tatizo kwake, maridhiano tu. Unaridhiana vipi na watu, kwa mfano, sisi unatuzuia kufanya mikutano ya hadhara ambayo ipo kisheria. Sheria namba 5 ya mwaka 1992 inasema tufanye mikutano ya hadhara lakini mpaka sasa tunazuiliwa na polisi, unaridhiana na nani?

The Chanzo: Ulisema hivi karibuni kwamba mataifa yaliyoendelea na taasisi za kimataifa hazina budi kuisamehe Tanzania madeni wanayoidai kama kweli wangependa kuiona Tanzania ikipiga hatua za kimaendeleo. Unadhani kwa nini hatua hiyo ni muhimu?

John Heche: Mimi ninavutiwa sana na masuala ya mazingira na naumizwa sana na nchi hii kwa sababu pamoja na umaskini tulionao nchi yetu itaingia kwenye matatizo makubwa zaidi kwa kadri mazingira yanavyozidi kuharibiwa.

Mabadiliko ya tabia ya nchi yanazidi kuwa makubwa, yameathiri sana Ulaya. Ukifuatilia jinsi ambavyo dunia inaenda, hewa ya ukaa ambayo inatolewa na viwanda, kwa sababu Afrika nzima inatoa asilimia mbili tu. Kuchangia kwenye uchafuzi wa mazingira huko angani na kutoa ile hewa ya ukaa inayoenda kusababisha theluji ya milima kuyeyuka, kwa mfano, Mlima Kilimanjaro kuna theluji, theluji inakaribia kuisha.

Maeneo ambayo yalikuwa na majani kipindi kilichokuwa huko nyuma leo hayaoti majani, mvua wakati mwingine zinakuwepo mvua hazitabiriki. Zamani, kwa mfano, mimi wakati nakua Tarime tulikuwa tunajua kabisa misimu ya mvua ni miwili na sisi tulikuwa tunalima misimu miwili. Unajua kabisa mvua inaanza muda fulani mpaka muda fulani.

Kwa mfano, mvua ilikuwa inaanza Agosti, Septemba, Oktoba watu wanapanda wanavuna Novemba. Wanaanza tena wanalima tena Februari panakuwa na mvua hapo. Kwa hiyo, Tarime mvua zilikuwa hazinyeshi miezi miwili. Lakini sasa hivi huwezi kukadiria tena. Kuna mwaka zinanyesha sana, kuna mwaka hazinyeshi. Sehemu nyingine ni balaa zaidi.

Ukiangalia maji yanazidi kupungua wakati mwingine sehemu nyingine ambazo zilikuwa visiwa zimemezwa na maji. Ukipita, kwa mfano, nikupe mfano halisi. Miaka sita nyuma ulikuwa ukivuka Morogoro mjini unaenda Dodoma ukivuka Mvomero umeanza maeneo hayo ni pori, miti mizuri. Leo miti yote imeangushwa imekua mkaa.

Ukipanda, ukienda, kwa mfano, ukiwa unaenda Iringa, ukiiacha Mikumi, ukiacha pori la Mikumi, ulikuwa ukiacha katikati ya Mikumi yenyewe unaianza hiyo mlima hiyo ilikuwa na miti mizuri unashuka mpaka kule Ruaha, Mbuyuni kule chini yote ni miti mpaka unaenda kuikaribia Kilolo.

Leo pale lile eneo linaelekea kuwa jangwa, miti inazidi kuisha. Nenda Kusini [mwa Tanzania]. Vivyo hivyo. Nenda kila sehemu hivyo hivyo. Kwa hiyo, mimi nipo na tahadhari na mabadiliko ya tabia ya nchi yatakavyoipiga hii nchi. Mito itakauka. Watu hawatapa maji. Hali itakuwa mbaya zaidi.

Watu hawatakuwa na nishati ya kupikia kwa sababu leo tuna umeme ambao tumepelekea watu chini ya watu asilimia 20 na kiuhalisia watu waliopata umeme hawana uwezo wa kuutumia kuupikia, wanauwezo wa kutumia kuangalizia na labda na kunyooshea [nguo] kwa kutumia umeme kwenye kupika ni gharama sana, hata watu wenye fedha wanatumia mambo ya kuni na mkaa.

Kwa hiyo, mimi nilipendekeza kwamba kwa sababu nchi zilizoendelea [kama vile] Ujerumani, Marekani, Uingereza na nchi nyingine zimeona athari ya mabadiliko ya tabia ya nchi na imewaathiri wao sawa na inavyowaathirika Waafrika.

Kwa hiyo, mimi nikaomba na nikatoa wito kwamba kwa sababu hizo nchi zinatudai, zinatudai madeni na huwa tunakopa kwao na wao wanataka sisi tusitumie nishati kwa mfano ya gesi, wanataka tutumie nishati jadidifu, kwa mfano sola, umeme wa upepo [nishati] ambazo haziathiri mazingira.

Tukitumia gesi au mkaa wa mawe ambao tunao pale Mchuchuma na Liganga katika kuanzisha viwanda vyetu tutazidi kuchafua anga, tutazidi kusababisha matatizo kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi.

Kwa hiyo, mimi nikawaambia kama Wazungu wanataka sisi tuende kwenye nishati jadidifu wakati wao viwanda vyao vinatumia nishati nafuu kama makaa ya mawe na gesi katika kujijenga na wamekua na maendeleo makubwa wakubali kusamehe madeni wanayotudai.

Lakini hayo madeni yakisamehewa yaende mahususi kwenye kuzalisha nishati ambayo itaokoa ukataji wa miti.

Kuna zile tunaita NBCs kila nchi inaweka malengo yake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Kupatia watu maji, kujenga vituo vya kimafunzo vya kutoa labda mbegu ambazo ni bora, ambazo zitahimili mabadiliko ya tabia ya nchi. Kutengeneza mazingira ya kukabiliana na hali tuliyonayo na kulinda nchi isiendelee kuharibika.

Kwa hiyo, [hayo] ndiyo mambo mahususi ambayo nilikuwa napendekeza kwamba madeni yanaposamehewa, yakisamehewa siyo tusichukue fedha tupeleke tena kwenye sijui madarasa, sijui nini. Ziende kwenye mambo mahususi ambayo ni hayo sasa.

Ya kuzalisha nishati ili tusaidie na watu wanaotumia mkaa, wasitumie mkaa, watumie nishati ambayo tutawapa ili watu wanaotumia kuni, wasitumie kuni. Watu wanaotumia mafuta ya dizeli na petroli katika kupikia au kuzalisha umeme tuwasaidie. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hoja yangu imejikita hapo.

The Chanzo: Sasa, kwa mfano, unadhani leo, kwa mfano, mataifa ambayo ulisema yafanye hivyo, yakaamua kufanya, unaamini kwamba Serikali yetu inaweza kuzielekeza hizo pesa kwenye maeneo unayotaka wewe?

John Heche: Hapana kwa sababu hizo hela ni za Wazungu, ukikusanya unawapelekea wao.

Wao wanaenda kuzipangilia bajeti na ili fedha ziingie kwenye mzunguko wenu mkatoa na wataalamu wenu, wao kwa sababu hizi fedha zilipaswa kuwa zao, yaani Ujerumani anavyotudai akisema labda nimetoa trilioni mbili kwenda kwenye chanzo cha kutengeneza umeme Ziwa Ngosi pale wa joto ardhi, Tanzania iweke wataalamu halafu sisi tutawalipa watengeneze huo umeme halafu Ujerumani inaenda wanaandikia kule kwamba lile deni Tanzania imelilipa kwa kupitia kutengeneza ule mradi.

Kwa hiyo, tunakuwa kama sisi tumemlipa yeye, yeye kumbe ametusamehe kwa hiyo lile deni lake linaonekana kule kuliko wao wanapotoa hela nyingine kuleta huku kwa ajili ya kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi.

Kwa sababu kuna wito kwa nchi za Afrika kwamba mataifa yaliyochafua zaidi dunia ndiyo yatoe fedha, ndiyo ile kulikuwa na ahadi ya dola bilioni 100 kwa nchi za Afrika. Sasa mimi mapendekezo yangu wasitoe hata hela nyingine na kuzileta huku, hizo wafanyiebiashara.

Wao watusamehe tu haya madeni, sisi tufanyie kazi kwa sababu sisi tutakusanya wenyewe na zitakwenda kwenye kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Kwa hiyo, tunachohitaji ni usimamizi na uadilifu kwenye hiyo miradi.

The Chanzo: Lakini tukienda mbele wewe unaamini uhitaji wa kuwa na mifumo ambayo inailazimisha Serikali kuwajibika kwa wananchi wake bila ya kuwepo Mzungu ni muhimu sana?

John Heche: Ni sahihi kabisa. Ni kubadilisha uongozi. CCM hawawezi kututoa. Jambo la kwanza ni kuondoa CCM madarakani na kuleta Katiba Mpya, Katiba ambayo-’. Leo mathalani Katiba yetu inasema Rais hashtakiwi.

Leo Jacob Zuma ameshtakiwa yuko nje kwa dhamana pale Afrika Kusini, anajua balaa alilokutana nalo gerezani. Kwa hiyo, mtu yeyote anayeingia kwenye madaraka Afrika Kusini anajua ukicheza na wananchi, ukitoka tu madarakani wanaruka na wewe shingoni kwa sababu Katiba ipo.

Lakini Rais wa Tanzania hata akisema sisi wote tuuawe hawezi kushtakiwa popote. Mzee Mkapa aliwai kuniambia kuwa Rais wa Tanzania ana mamlaka ya kusema kijiji fulani kifutwe, yaani watu wauawe wote halafu hakuna utakapo mhoji. Yaani wamejipa mamlaka, Rais wa Tanzania amejipa mamlaka ya kukaribiana na Mungu.

Sasa Rais anakinga, akajitunga kinga na Jaji Mkuu. Hebu fikiria, Jaji Mkuu unajipa kinga hata, Kongo ya Mobutu haikuwai kutokea hivyo? Jaji Mkuu wa Tanzania ana kinga dhidi ya mambo atakakayoyafanya akiwa madarakani. Jaji Mkuu ni mtu wa haki wewe unafanya mambo gani ambayo yanahitaji kinga?

Spika wa Bunge ana kinga kwenye nchi hii. Sasa kwa msingi huu nani atawajibika? Kwa sababu binadamu alivyoumbwa bwana Khalifa ni kiumbe mwenye tamaa, mwenye uroho, mwenye ni nini.

Kinacho mdhibiti binadamu ni sheria, tusingetunga sheria binadamu angezaliwa na mama halafu angetembea na mama yake. Kinachozuia hayo mambo yasitokee ni sheria na makuzi ya watu: usifanye usifanye, fanya, fanya fanya. Unanielewa vizuri? Sheria ziwepo zinazokataza.

Kwa hiyo, binadamu ukimuwekea mali, ukaweka pesa katika maamuzi yake na usimdhibiti, atachukua hizo pesa. Lakini ukitunga mfumo ambao anajua ukipeleka mkono kuchukua pesa sisizo kuwa za kwako vidole vitabaki pale hawezi kupeleka pale mkono.

Nchi ya Tanzania, kwa sheria zilizopo, na chama kilichopo madarani, kinapalilia kutokuwepo kwa umoja, kiuhalisia unapeleka mtu mzuri CCM kesho anakuwa nyang’au kwa sababu asipoiba wanamshangaa.

Kwa sababu kila kitu kipo pale cha kuiba, ndiyo maana nchi hii miaka 60 unaniuliza deni linazidi kupanda. Tunaagiza ngano sisi Tanzania. Haiwezekani katika mazingira ya kawaida, tuna kila kitu. Kaka hii nchi inaweza kuwa nchi imara ya Afrika na maandishi yapo.

Ukifungua hii bandari tu ya Dar es Salaam, [Rais wa Rwanda Paul] Kagame alisema akipewa bandari ya Dar es Salaam tu analisha ukanda wa Afrika Mashariki na Kati yote kwa kutumia hii bandari.

The Chanzo: Pale umesema kuna haja ya kubadilisha uongozi, ukimaanisha kwamba CHADEMA inabidi muwepo madarakani?

John Heche: Kabisa!

The Chanzo: Nini kinakupa matumaini kwamba, kwa mfano, CHADEMA ikichukua uongozi wa nchi mambo yanaweza kuwa tofauti, nini kinakupa imani hiyo?

John Heche: Jambo la kwanza tutatengeneza Katiba ambayo itaunda taasisi ambazo hata mtu yeyote wa CHADEMA akitaka kudokoa tutashughulika naye.

The Chanzo: Rais Samia anasema anaenda kuwapa Katiba.

John Heche: Hawezi. Hana dhamira hiyo. Angekuwa na dhamira hiyo rafiki yangu haya mambo tungeona yameshaanza kufanywa. Vitendo vya Samia, Samia anatamani kuwa yeye, anatamani kuwa kama Magufuli ndiyo maana nimesema Rais ameshindwa kujitambulisha yeye ni mtu wa namna gani, nini haswa anachotaka, nini anataka kufanikiwa kiuchumi iwe wazi hata kwa mtoto mdogo akiamka ajue.

Mimi Heche, kwa mfano, nikiwa Rais wa nchi hii watu wanajua nitawekeza kwenye kilimo, nitawekeza kwenye ufugaji na uvuvi baada ya miaka mitano ya kwanza, vijana watakuwa matajiri wanaendesha magari, wana nyumba nzuri kwa sababu inawezekana.

Tutasimamia sheria. Kwa mfano, tulitunga sheria ya ulinzi wa rasiliamali za umma kwamba mkataba wowote ambao Serikali yetu inaingia na makampuni ya kimataifa kwenye gesi, kwenye uvuvi, kwenye madini, kwenye nini ndani ya siku sita za mwanzo za Bunge linalofuata mikataba ipelekwe bungeni.

Ile ajenda ikishakuwa imejadiliwa bungeni inakuwa ni ya umma na wewe unaweza kuitumia ukahoji, sijui kama unanielewa? Wakati mwingine watu wanashindwa kuelewa tunaposema kitu kipelekwe bungeni, wengine wanasema mbona Bunge mnasema siyo mbunge sijui nini? Halafu mnasema vitu vipelekwe?

Hapana. Ukipeleka kitu bungeni na taarifa ikajadiliwa kwenye meza ya Spika wa Bunge inakuwa ni taarifa ya umma. Kwa hiyo, unaweza kuitumia hata wewe. Lakini kama haipo pale huwezi kuitumia.

Kwa hiyo, wakati mwingine tunasema taarifa ziende bungeni siyo kwa sababu tunaamini hili Bunge lililoiba uchaguzi kwamba linaweza kufanya chochote lakini kitu kikiingia pale kitakuwa kwenye matumizi yetu tunaweza kukipata na kukihoji kupitia hapo.

[Serikalini] hawafuti sheria, sheria ipo ya ulinzi wa rasiliamali, sheria ya 2017 kifungu cha 6 kimeelezwa wazi kabisa, hawafanyi hivyo. Sasa watu kama hao hawawezi kusaidia hii nchi kusonga mbele kwenye uchumi nini tunataka kukipata, kwenye siasa, demokrasia nini tunataka kupata kwenye utamaduni na mazingira.

Hivyo vitu vikiwa wazi tutaendesha nchi kiurahisi kwa sababu una malengo umejiwekea kwamba nikifika pale ninunue baiskeli, nikifika pale nitanunua pikipiki, nikifika pale na njia za kwenda unaziweka na zinaonekana. Sasa ukiwa nchi inajiendea tu.

Haya juzi Magufuli alikuwa anatuambia hivi leo tumegeuka Rais haeleweki, yuko vuguvugu, anataka demokrasia, hataki demokrasia, anasema mimi nitaruhusu mikutano. Mikutano huhitaji hata kuruhusu. Zuio la Magufuli lilikuwa batili.

Rais Samia unatakiwa ujitofautishe na Magufuli, uiambie dunia nimeikuta mikutano imefungiwa kuanzia leo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) watu wafanye mikutano. Waiweke Serikali yako kwenye taa iwajibike.

Kwa nini mnaogopa watu wasiwahoji, kwa sababu hamtaki kuwajibika. Wanajua Heche akifanya mkutano Kinondoni hapa atawaambia watu mnavyokopa deni, tuwazibe, na wananchi siyo wajinga, kuna njia nyingi tu za kuwasiliana.

Kesho tukienda Tarime tutahoji kuhusu namna madini hayatumiki kwa watu. Kesho tukienda Mwanza tutahoji namna wanavyoshindwa kuwekeza kwenye uvuvi. Kwa hiyo, hayo ndiyo mambo ambayo Serikali inayaogopa.

Lakini kama wangeruhusu mikutano ya hadhara kiuhalisia tungewasaidia, tungekuwa tunaongea jambo ambalo wangeweza kulichukua, wakaliweka kwenye vitendo.

Lakini leo Magufuli alijidanganya hivi hivi miaka mitano akafungia mikutano, [Mgombea wa Urais mwaka 2020 kupitia CHADEMA Tundu] Lissu alipoanza mikutano, ilibidi apore uchaguzi.

Rais Samia atakuja kushangazwa na Watanzania kwenye uchaguzi na najua anahitaji kugombea. Lakini Watanzania watamshangaza sana. Ni bora angeacha mikutano aanze kujipima mapema licha ya CCM kimekwisha kufa lakini aanze kujipima mapema wananchi wanamchukulije.

Ni hatari sana kufungia watu kwenye boksi na wakaja kuchomoka wakati wa kampeni ni muda mfupi sana kwao kujibu hoja hizo.

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Asifiwe Mbembela na kuhaririwa na Lukelo Francis. Shafii Hamisi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts