Leo hii [Oktoba 30, 2022], mimi mwenyewe binafsi na viongozi wenzangu wa ACT-Wazalendo, bila shaka na wanachama pamoja na wapenzi wetu popote walipo duniani, tuna furaha kubwa sana, furaha isiyo na kifani kuona tunafungua ofisi yetu wenyewe hapa Magomeni, Dar es Salaam.
Tangu chama kilipoanzishwa kilikuwa na ofisi katika eneo la Kijitonyama lakini kwa hakika haikuwa na hadhi ya ofisi ya chama cha siasa chenye ndoto ya kushika dola na kuongoza Serikali.
Hiki ni chama kilichokuwa kinadharauliwa na kuonekana cha kinyonge. Washindani wetu walikuwa wakitutania kwa ofisi yetu ndogo na kusema ACT-Wazalendo ina bendera nyingi kuliko wanachama. Leo, hawatucheki tena!
Pamoja na kudharauliwa na kubezwa, tulikuwa na ndoto kuwa itafika siku moja ACT-Wazalendo itakuwa na ofisi yake yenyewe, na si ofisi tu bali ya kisasa kwa haiba yake lakini pia kwa samani na vifaa mbalimbali kwa matumizi ya ofisi. Ndoto hii leo tumeitimiza leo nanyi ni mashahidi wa hili.
Tuna furaha siyo kwa sababu tumepata jengo tu bali kwa sababu ofisi yenyewe inawakilisha taswira ya chama chetu – cha vijana, cha kisasa, wabunifu na wachapa kazi.
Chama cha watu wenye maarifa na wenye uwezo mkubwa wa kustahmili misukosuko. Muhimu zaidi, chama kiongozi kinachotazama mbele. Ofisi yetu hii si tu ni jengo, kuna majengo mengi mazuri nchini, bali ni alama ya sisi ni nani na tuna dhamira gani.
Ni alama ya uwezo wa wanachama wetu kujikusanya wenyewe na kuamua kufanya jambo ambalo katika hali ya kawaida hudhani haliwezekani. Ni alama ya uwezo wa viongozi wetu kuwafikia watu wa makundi mbalimbali na kuwashawishi waamini katika ndoto yetu.
Ukubwa wa ndoto zetu
Jengo hili tunalofungua leo ni kielelezo cha kuonyesha ukubwa wa ndoto zetu. Kama hatuwezi kujenga ofisi yetu wenyewe, tutaweza kujenga miundombinu mikubwa ya umwagiliaji?
Tutaweza kujenga shule ya watoto wetu kusoma na vituo vya afya vya akina mama zetu kujifungua kwa stara? Tutaweza kupambana na janga la umasikini wa watu wetu na kutengeneza uchumi unaozalisha ajira kwa vijana wetu?
Ofisi hii ni ishara ya ndoto zetu. Tutaijenga Tanzania na Zanzibar kwa ukubwa huu wa ndoto zetu. Ndoto kubwa ndiyo siri iliyojificha kwenye ujenzi huu wa ofisi yetu ambayo leo tunaifungua rasmi.
Sisi ACT-Wazalendo tunaamini kuwa shabaha kuu ya chama chochote cha siasa inapaswa kuwa ni kuunda sera zitakazowezesha kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi. Kutatua shida za Watanzania kunahitaji viongozi wenye muda wa kutulia na kufikiria.
Kunahitaji viongozi wenye ofisi zenye mazingira ya kutafakari na usiri wa vikao. Wanachama wa ACT-Wazalendo wametuwekea sisi viongozi mazingira hayo ya kufanya kazi na kutafakari vizuri ili kuimarisha chama chetu na kubuni sera mbadala za kuliongoza taifa letu.
Kwa mnasaba huu basi, sinabudi kutoa shukrani zangu za dhati kwa viongozi wenzangu ndani ya ACT-Wazalendo kwa kuwa na dira ya pamoja katika ujenzi wa chama chetu.
Aidha, wanachama wetu na wapenzi pamoja na wahisani wetu, wa ndani na nje ya nchi, ambao tumekuwa tukishakana mikono kwa hali na mali kukiendesha chama chetu.
Kupitia kwenu ndani ya kipindi cha miaka miwili tumefanikisha kufanya mikutano mikuu mitatu kwa gharama zenu. Na leo hii tunazindua jengo letu linalotokana na michango yenu. Tunawashukuru sana!
Nisiwe mwizi wa fadhila kama sitowashukuru pia mafundi kuanzia mhandisi mwenyewe na vibarua ambao wamejitolea kwa nguvu zao zote kukamilisha ujenzi wa ofisi hii.
Najua, husuan wiki tatu hizi za mwisho, kazi haikusita hata saa moja, siyo usiku, siyo mchana, muda wote watu wamekuwa kazini. Ahsanteni sana.
Tulibezwa
Mara nyingi nimekuwa nikitumia msemo huu – Kwanza wanakubeza, pili wanapambana na wewe, tatu unawashinda. Huko tulikotoka, tulichekwa kwa kuwa na bendera nyingi bila ofisi wala wanachama. Tulibezwa.
Kama mnasoma magazeti na mitandao ya kijamii, sasa waliotubeza wameamua kupambana nasi. Hii ni hatua ya pili tayari. Sina shaka kwamba hatua ya tatu – ya kuwashinda – haiko mbali kutoka sasa.
Jengo hili ni sehemu ya mipango mingi tuliyonayo katika ujenzi wa chama chetu. Tunakusudia kufanya mabadiliko makubwa katika kila eneo. Kuanzia ofisi zetu za chama, uongozi na sera zetu.
Tulianza mapema mwaka huu kwa kuzindua mfumo wa kuandikisha wanachama wetu kidigitali tuliouita ACT Kiganjani.
Hivi sasa maelfu ya wanachama wetu wanajisajili katika mfumo huo na tunaendelea na kampeni maalumu za kuhakikisha kuwa kila mwanachama wetu anasajiliwa katika mfumo wa ACT Kiganjani.
Vilevile, mwanzoni mwa mwaka huu tulizindua Baraza Kivuli la Mawaziri kama Idara Maalumu ya Chama ya Wasemaji wa Kisekta.
Mawaziri wetu, na hapa niseme kwa ufakhari kabisa, asilimia 52 ni wanawake na asilimia 45 ni vijana chini ya umri wa miaka 35 wakiongozwa na Waziri Mkuu Kivuli Bi Dorothy Semu, wanafanya kazi nzuri sana.
Hivi sasa kila siku unaisikia ACT-Wazalendo ikipaza sauti kuibua masuala ya wananchi. Hili ndiyo jukumu la chama cha siasa – muda wote kuiwajibisha Serikali kwa masuala ya wananchi na kupendekeza majawabu. Sisi tulikataa kuwa chama cha kulalamika tu.
Tulikataa kushikwa mateka na madhila ya mwaka 2020. Tumeamua kuhakikisha yaliyotokea 2020 hayatokei tena kwa kupigania mageuzi ya kisheria na kikatiba na siyo kwa kuwa walalamikaji.
Mapitio ya sera
Katika mwendelezo wa kukijenga chama chetu kimkakati tumefanya mapitio ya sera zetu na mapema mwaka 2023 tutazizindua rasmi. Tangu Aprili 2022, tumekuwa tukifanya kazi kubwa ya ujenzi wa chama chetu na kazi hiyo tunaendelea nayo.
Tumedhamiria kufikia malengo yetu ya kuwa chama kinachoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar na kujenga taifa la wote kwa maslahi ya Watazania wote. Yote haya ni katika mageuzi tuliyoamua kuyafanya.
Tunayafanya haya kwa sababu ACT-Wazalendo ni chama kinachoamini kuwa nchi yetu inahitaji mageuzi ya kweli kweli ambayo yatawanufanisha Watanzania wote. Sisi tunaamini ACT-Wazalendo ni chama kinachoweza kutimiza matarajio hayo ya wananchi.
Hivyo, niwaambie basi katika mpango wetu huu mara baada ya kumalizika kwa ujenzi huu, sasa nguvu zetu zinaelekea kujenga ofisi ya kisasa kule Zanzibar. Baada ya hapo tunahamia kwenye ujenzi wa ofisi zetu za mikioa na baadaye ofisi za majimbo.
Na hatutoishia kwenye majengo tu, ni ofisi za kisiasa pamoja na vifaa vyake ikiwa na pamoja na vitendea kazi na usafiri kwa watendaji wetu.
Muhimu ni kuwa tunataka viongozi wanaowajibika kujenga chama, mageuzi haya hayatomuacha pia kiongozi goigoi. Kwa hiyo, wito wangu kwa viongozi na wanachama ni tuongoze juhudi za ujenzi wa chama.
Nichukue nafasi hii kuwaeleza Watanzania kuwa tumedhamiria kujenga chama cha siasa cha kisasa, kinachoshughulika na masuala yao, kinachowajibika kwao na kinachoongoza harakati za mageuzi hapa nchini.
Tunajenga chama cha siasa kinachofanya siasa. Kwa wale Watanzania walio kwenye vyama mbalimbali na wanaoona kuwa hawapati nafasi ya kufanya haswa kazi ya siasa wanayokusudia, jukwaa la kufanya siasa lipo ACT-Wazalendo.
Hii ni nchi ya kidemokrasia inayotoa uhuru kwa kila mtu kujiunga na chama cha siasa kinachoweza kufanikisha malengo yake.
Ewe mwanasiasa ambaye unataka kufanya siasa lakini chama chako hakikupi nafasi ya kufanya hivyo, njoo ACT-Wazalendo tufanye siasa!
Zitto Kabwe ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo. Hii ni sehemu ya hotuba aliyoitoa kwa wanachama wa chama hicho cha upinzani wakati wa uzinduzi wa Makoa Makuu mpya ya chama hicho yaliyopo Magomeni, Dar es Salaam. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.