Ajali ya ndege ya shirika la Precision Air iliyotokea Bukoba, Novemba 6, 2022, imeibua mjadala kuhusu kasumba ya ajira Tanzania kwa namna ya kipekee kabisa.
Katika ajali hiyo ambayo ilitokea asubuhi, siku ya Jumapili, kijana shujaa Majaliwa Jackson alikuwa mtu wa kwanza kufika kwenye tukio, ambapo alivunya mlango wa ndege kwa kasia lake na kuwawezesha baadhi ya abiria kutoka wakiwa hai.
Jumla ya abiria 26 waliokolewa na 19 waliosalia walifariki dunia.
Kutokana na ujasiri wa Majaliwa, Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa mkutanoni huko nchini Misri, aliagiza kijana huyo aandikishwe Jeshi la Zimamoto na Ukoaji kwa mafunzo zaidi kuhusu uokoaji kama zawadi kwa kitendo chake cha ujasiri.
SOMA ZAIDI: Sekretarieti ya Ajira Ifanye Haya Kuepusha Usumbufu kwa Waombaji Kazi za Serikali
Na kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Majaliwa tayari ameshapokelewa jeshini ambako atajifunza na kutumika kuokoa maisha ya watu na mali zao katika kituo atakacho pangiwa baada ya mafunzo.
Hili la kumpeleka Majaliwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limezua jambo. Kwanza, ni kuhusu umuhimu na utofauti kati ya ujasiriamali na ajira.
Pamoja na kuwa Majaliwa ameishukuru Serikali kwa kumpa nafasi jeshini, baadhi ya watu wanadhani kwamba kwa namna fulani kumpeleka kijana huyo jeshini hakutamfaa sana.
Majaliwa hakuulizwa
Hakuna dalili zinazooenesha kuwa Majaliwa aliulizwa anataka Serikali imfanyie nini au impe zawadi gani. Ni kama vile amri ilitoka juu kijana apelekwe jeshini.
Akiwa kijana mtiifu na kwa kasi ambayo matukio yote yaliyovyoteka ilikuwa vigumu kwa Majaliwa kupata nafasi ya kutafakari na kuamua kwenda au kutokwenda jeshini.
Itachukua muda kwake kuanza kuyapitia matukio yote yaliyotekea yaliyomfanya awe shujaa wa ghafla.
Watu wanashangaa kwa nini Serikali imekimbilia kumpa Majaliwa ajira serikalini badala ya kumuwezesha katika shughuli zake za uvuvi kwa kumuongezea mtaji na kumpa vifaa vya kisasa ili aweze kuwa mvuvi bora zaidi.
Wengi katika mtazamo huu wanadhani kwa ujasiri wake Majaliwa angefaa zaidi kama angebaki ziwani kuliko kupelekwa kufanya kazi katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Idara hii inajulikana kwa kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha, yenye ufanisi mdogo na ambayo ni chanzo cha malalamiko kila yanapotokea majanga makubwa nchini. Mazingira haya ya kazi ni kama vile kupoteza kipaji cha Majaliwa.
SOMA ZAIDI: Mfumo Wetu Wa Uchumi Na Dhana Ya Ukosefu Wa Ajira
Kama angebaki ziwani, Serikali ingeweza kuunda vikundi vya uokoaji vitakavyo muhusisha Majaliwa na wavuvi wengine.
Vikundi hivi vingepata mafunzo na vifaa vya mawasiliano vya kisasa, pamoja na vifaa vya kisasa vya uvuvi. Ziwa Victoria pia linahitaji uokoaji wa uhakika kwa sababu ya ajali za majini za mara kwa mara zinazopoteza maisha ya wavuvi na abiria.
Dhana potofu kuhusu ajira
Kwa kuharakisha kumpeleka Majaliwa jeshini, viongozi wa Serikali wameonesha udhaifu kwa kudhani kuwa ajira ndiyo zawadi bora zaidi ambayo wangeweza kumpatia Majaliwa.
Hii inatokana na dhana potofu iliyoshamiri nchini inayoipa ajira umuhimu uliopitiliza.
Dhana hii ndiyo imefanya maelfu ya vijana waliomaliza shule na vyuo waranderande mitaani wakisubiri ajira, wakati fursa za kujiajiri ziko tele.
Tukio la ajali ya ndege ya Bukoba limeonesha kuwa Serikali inachangia si tu kulea dhana hii ya ajira bali pia kuichochea.
Labda ndiyo maana hata uboreshaji wa mitaala shuleni na vyuoni ili kuwawezesha vijana kujiajiri badala ya kusubiri ajira umekuwa ni wa kusuasua.
Mitaala ya Tanzania ina muktadha wa tangu enzi za uhuru, ikisisitiza zaidi kuzalisha watumishi serikalini kuliko wajasiriamali.
Ni matumaini ya wengi kuwa Serikali italiona hili na kumuondoa Majaliwa jeshini na kumrudisha ziwani akiwa na mtaji mkubwa zaidi na zana bora za uvuvi.
Fursa kwa vijana
Tanzania ni nchi iliyojaaliwa rasilimali ambazo bado wananchi hawajazitumia vya kutosha kujiongezea kipatao.
Nchi hii ina eneo kubwa sana la bahari, maziwa makubwa matatu, maziwa madogo kadhaa, mito na mabwawa lakini bado kitoweo cha samaki hakipatikani kwa urahisi, na kikipatikana ni ghali sana.
Yote haya ni kwa sababu wavuvi wana mitaji midogo na zana za kizamani. Vijana wengi hawajishughulishi na uvuvi, labda kama ni shughuli ya kifamilia. Watu wazima ndiyo wengi katika shughuli hizi.
Kumuwezesha Majaliwa kuwa mvuvi bora na muokoaji mzuri zaidi wa siku zo usoni ingekuwa ni ujumbe ambao Serikali ingepeleka kwa vijana kuhusu kuchagua kujiajiri na kutokusibiri ajira. Kwa bahati mbaya, Serikali imekosa fursa hiyo.
Na kwa kweli fursa kwa vijana hazipo katika uvuvi tu. Tanzania ni nchi yenye eneo kubwa sana la kilimo, kwa mfano, ambalo halijatumika vya kutosha. Vijana wengi wanakimbilia mijini wakiacha watu wazima mashambani.
Ifike wakati viongozi wa Serikali wabadilishe mtazamo na waachane na dhana kuwa ajira ndiyo kila kitu.
Wakiweza kufanya hivi basi itakuwa rahisi kwa mitaala shuleni kubadilishwa na kwa wananchi kuanza kuona na kuzichangamika fursa bwerere za kujiajiri zilizopo nchini!
Damas Kanyabwoya ni mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi. Anuwani yake ya barua pepe ni dkanyabwoya@gmail.com. Anapatikana pia Twitter kama @DKanyabwoya. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.