Mtwara. Mwaka wa 2022 umeshuhudia Watanzania kadhaa wakitambulika katika ngazi za kitaifa na kimataifa kwa mchango ambao wameendelea kuutoa kwenye tasnia zao husika na hivyo kuwapa hamasa zaidi kwenye kufanya vile ambavyo wamekuwa wakivifanya.
Zikiwa ni siku chache zimebaki kabla ya mwaka huu kwenda kuisha, The Chanzo inakuletea orodha ya Watanzania 10 ambao wametambulika kwa sababu mbalimbali.
Kwenye orodha hiyo, wapo wanasiasa, wanamuziki, wanamichezo na watu walipo kwenye tasnia nyengine:
- Rais Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani hapo Machi 19, 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.
Mnamo Novemba 30, 2022, Rais huyo wa kwanza mwanamke kwa taifa la Tanzania alitunukiwa shahada ya udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Hatua hiyo ilikuja baada ya Baraza Kuu la chuo hicho, katika kikao chake cha 876 lilimpendekeza Rais Samia kutunukiwa digrii hiyo ya juu ya heshima ya falsafa kwa kile walichoeleza kuwa ni kutokana na mchango wake katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kielimu nchini.
Akimtunuku Rais Samia shahada hiyo ya heshima, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Jakaya Kikwete alisema ni watu wa tatu tu ndiyo wamewahi kutunukiwa shahda hiyo ya heshima na chuo hicho, hatua inayomfanya Rais Samia awe wa nne.
- Florens Luoga
Profesa Florens Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, aliibuka mshindi wa tuzo ya Central Banker of the Year for Africa for 2022 Award inayotolewa na jarida la The Banker ambayo hutambua maafisa waandamizi wanaochochea ukuaji uchumi na ustahamilivu kwenye nchi zao husika.
The Banker linamilikiwa na gazeti la nchini Uingereza la Financial Times. Tuzo yake kwa Profesa Luoga, aliyeteuliwa kwenye nafasi hiyo hapo mwaka 2018, ilikuwa na lengo la kutambua mchango wake katika kusisitiza nidhamu miongoni mwa wakopeshaji wa ndani ya Tanzania.
- Mohammed “Mo” Dewji
Akiwa kama rais wa kampuni ya MeTL Group, Mo Dewji alichukua nafasi ya 15 kwenye orodha ya mabilionea wachanga wa Kiafrika kwa kigezo cha Doza za Kimarekani iliyotolewa na jarida la Marekani la Forbes.
Akiwa na umri wa miaka 46 tu, Dewji anatambulika kama tajiri mchanga kabisa barani Afrika, akiwa na utajiri wa Dola za Kimarekani bilioni 1.5. Dewji aliirithi kampuni ya MeTL Group kutoka kwa wazazi na kufanikiwa kuisimamia na kuiendeleza hadi sasa.
Dewji aliliambia gazeti la The Citizen hapo Aprili 3, 2022, kwamba siku zote alikuwa anataka kuwa mtu tajiri lakini kadiri alivyokuwa anakuwa aligundua kwamba pesa siyo kitu muhimu kuliko vitu vyote ulimwenguni.
- Ally Awadh
The African Leadership Magazine, jarida linalochapisha habari za watu wanaofanya vizuri kutoka barani Afrika, lilimtaja bilionea Ally Awadh, mwanzilishi wa kampuni ya Lake Oil Group, kama kama mshindi wake wa the 2022 Young Business Leader of the Year.
Tuzo hiyo hutambua wafanyabiashara wakubwa waliochini ya umri wa miaka 40 kutoka barani Afrika kutokana na mafanikio yao ya kibiashara na mifano wanayoiweka kwenye jamii zao husika.
- Noelah Godfrey Msuya
Msuya, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali liitwalo Child Support Tanzania alishinda the Franco-German Human Rights Prize kutokana na mchango wake wa kutetea haki za watoto wenye ulemavu nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Mataifa, watu takriban bilioni moja huishi na aina fulani ya ulemavy duniani kote. Kwa Tanzania, takwimu zinaonesha kwamba angalau watu milioni 4.2 huishi na aina fulani ya ulemavu.
- Consolata Lubuva
Mtanzania Consolata Lubuva aliongoza kitaifa kwenye matokeo ya Kidato cha IV ya mwaka 2021 kati ya wanafunzi 483,820 waliofanya mtihani huo.
Mwanafunzi huyo wa Shule ya Sekomdari ya wasichana ya St. Francis ya mkoani Mbeya aliliambia gazeti la Mwananchi hapo Januari 15, 2022, kwamba ana ndoto ya kuwa daktari wa watoto.
“Nitakwenda kusoma PCB ili niwe daktari niweze kuwasaidia watoto wadogo,” Mwananchi ilimnukuu Consolata akisema. “Napenda sana kuwasaidia watoto wadogo ili wakue vizuri.”
- Fortunatus Bundala
Mtanzania Fortunatus Bundala aliibuka mshindi katika shindano la uandishi wa insha linalojulikana kama The Queen’s Commonwealth Essay Competition 2022, taji la Silver, baada ya hotuba yake aliyoibuni kama kiongozi mkuu wa nchi juu ya namna bora ya kutatua matatizo ya kielimu kukonga nyoyo za majaji wa shindano hilo.
Akiandika hotuba hiyo kama mwanafunzi wa Kidato cha VI katika Shule ya MT. Augustine-TAGASTE iliyopo Kimara, jijini Dar es Salaam, Bundala alijenga hoja kwamba mfumo wa elimu unaotumika hivi sasa nchini Tanzania haumpi mwanafunzi nafasi na fursa ya kujifunza na kuwa mbunifu.
Jumla ya wanafunzi 26,300 kutoka nchi 60 za Jumuiya ya Madola walishiriki shindano hilo lililokuwa na lengo la kuwatia moyo wanafunzi vijana kutoka nchi za jumuiya ya madola ili kuwajengea uwezo wa kujiamini katika kupaza sauti zao ili kuendeleza vipaji vyao.
- Majaliwa Jackson
Akiwa ziwani kuendelea na shughuli zake za kila siku za uvuvi, kijana Majaliwa Jackson alikabiliwa na mtihani wa kuokoa maisha ya watu kufuatia ajali mbaya ya ndege ya Precision iliyotokea katika Ziwa Victoria hapo Novemba 6, 2022, na kuuwa watu 19.
Jackson, 20, ametambulika kuwa miongoni mwa watu wa kwanza waliofika katika eneo la tukio ndani ya takriban dakika tano na, kwa kushirikiana na mhudumu wa ndege na abiria, alifanikiwa kufungua mlango wa ndege na hivyo kufanikisha uokozi wa watu wapatao 23.
Kufuatia ujasiri wake huo, iliamuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwamba Jackson aingizwe kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili aweze kutoa mchango stahiki kwa taifa. Pia, Jackson alitambulika kitaifa kutokana na ushujaa wake huo na kualikwa mpaka bungeni.
- Ramadhani Brothers
Ramadhan Brothers, kundi linalojihusisha na sanaa ya maonyesho na sarakasi, linaloundwa na ndugu wawili Ibrahim Ramadhani and Fadi Ramadhan lilikonga nyoyo za wafuatiliaji wengi wa michezo hiyo Tanzania na kwengineko baada ya kufanya vizuri sana kwenye mashindano ya kutafuta vipaji ya Australia’s Got Talent (AGT).
Licha ya kwamba ndugu hao wawili hawakuweza kuibuka washindi kwenye mashindano hayo, umahiri wao katika kuucheza mchezo huo uliwafurahisha wengi ulimwenguni, hali iliyopelekea mpaka Rais Samia Suluhu Hassan awapongeze vijana hao.
Ushiriki wao kwenye AGT pia uliwafanya ndugu hao wawili waalikwe na vyombo kadhaa vya habari baada ya kurejea nchini Tanzania.
- Karim “Mandonga” Said
Bondia huyo wa Kitanzania amejizolea sifa kwa uwezo wake wa kuhamasisha mchezo wa ndondi nchini na kuufanya ufuatiliwe na watu waliowengi.
Licha ya ukweli kwamba amekuwa akipoteza kwenye mechi nyingi alizokuwa akishiriki, Mandonga, kama anavyojulikana amejizolea mashabiki mengi kwa majigambo yake, hali iliyopelekea mpaka kupewa ubalozi wa kutangaza bidhaa za kampuni mbalimbali.
Mandogo pia amejizolea umaarufu kwa mtindo wake wa kubuni aina za ngumi, akija na majina ya ngumi kama vile “ndoige” na “PelosoPeloso.”
Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.