The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wazazi Watakiwa Kuacha Kuwaficha Watoto Wenye Ulemavu

Wanashauriwa kwamba kuendelea kufanya hivyo ni kukiuka haki za msingi za watoto wao, ikiwemo ile ya kupata elimu.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Wito umetolewa kwa wazazi wa watoto wenye ulemavu nchini kuacha kuwaficha watoto hao kwani kuendelea kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao za msingi za kibinadamu, ikiwemo haki yao ya kupata elimu.

Wito huo ulitolewa jijini hapa hapo Disemba 12, 2022, wakati wa Kongamano la Wadau wa Elimu Jumuishi nchini Tanzania.

Kongamano hilo lililolenga kujadili Maendeleo ya Elimu Jumuishi, liliandaliwa na Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania na Kituo cha Taarifa kwa Ulemavu (ICD) wanaotekeleza Mradi wa Elimu Jumuishi.

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Justus Ng’wantalima alisema kwamba wazazi wenye watoto wenye ulemavu huwaficha kwa kudhani kwamba wanawapenda kumbe wanawaangamiza.

“Wakati mwingine wazazi wanasema huyu mtoto mimi sitaki asumbuke, kwa hiyo anamuweka ndani, hampeleki shule,” alisema Ng’wantalima.

“Lakini maisha yajayo yanabadilika,” anabainisha Ng’wantalima. “Leo una uwezo kama mzazi, kesho huo uwezo hautakuwanao. Huyu mtoto atabaki na nini? Hana kitu cha kumsaidia.”

Aisha Msantu ni Mkurugenzi wa Glaring Future Foundation, shirika lisilo la kiserikali linalowajengea uwezo watu wenye ulemavu, alisema kwenye kongamano hilo kwamba umasikini huchangia wazazi kuficha watoto wao wenye ulemavu.

Msantu alisema kwamba ni muhimu jitihada zikaongezwa kwenye kupunguza umasikini kwenye kaya za watoto wenye ulemavu, akisema kwamba kadiri familia inavyokuwa kwenye umasikini ndivyo uwezekano wa watoto wenye ulemavu kufichwa huongezeka.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Afisa Elimu Maalum Jiji la Dodoma Issa Kambi, mpaka sasa jiji la Dodoma limebainisha watoto wenye ulemavu zaidi ya 400.

Watoto 96 wameonekana kuwa na aina ya ulemavu ambao wanahitaji huduma ya kielimu kwa maana ya afua stahiki.

Watoto hao wanatarajiwa kusajiliwa mwezi Januari 2023 kuanza na masomo ya elimu ya msingi.

“Tunatoa wito kwa wazazi wote wa watoto wenye ulemavu katika jiji la Dodoma, popote ulipo mzazi, ukigundua kuna mtoto amefichwa, taarifa itolewe ili kusudi tuweze kufuatilia kwa kina,” Kambi alitoa wito huo wakati wa mazungumzo yake na The Chanzo.

“Ndiyo maana hata hawa watano waliofichwa namuelekeza kiongozi wetu kituo cha upimaji [Nkuhungu] aende afuatilie na anipe ripoti tunamsaidiaje, kama ni ‘home-base’ wakapewe huduma kama ni wa kusajiliwa shule wakasajiliwe shuleni,” aliongeza Kambi.

Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Nkuhungu, ambaye pia ni Msimamizi wa Kituo cha Upimaji kwa watoto wenye ulemavu, Awadhi Mbogo, amesema ili kuwaondoa wazazi katika hali ya kutamani kuwaficha watoto wao wenye ulemavu wamekuwa wakiwashauri namna bora ya kuishi na watoto hao.

“Huwa hawakubali kama mtoto huyo amezaliwa na chagamoto hiyo ya ulemavu. Kuwaondoa kwenye hali hiyo huwa tunawapa mifano watoto wengine ambao walikuwa na ulemavu zaidi ya watoto wao na sasa hivi wako vizuri,” alisema Mbogo.

“Vilevile, tunafanya ufuatiliaji kuangalia maelekezo kama mzazi ameyafuata au la. Kwa ile kufuatilia mara kwa mara inamsaidia yeye mara kwa mara kujua kwamba inawezekana. Wakati mwingine wazazi wanakosa elimu juu ya masuala ya watoto wenye ulemavu,” aliongeza mtaalamu huyo.

Huku kukosa elimu kumeungwa mkono na baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu ambao kabla ya kupata elimu wao wenyewe walikuwa wanawaficha watoto hao.

Mmoja kati ya wazazi hao ni Marry Eliud, mama wa mtoto mmoja wa kiume mwenye ulemavu, mwenye umri wa miaka 13, ambaye amekiri kwamba kama isingekuwa elimu aliyoipata, mtoto wake bado angeendelea kubaki mafichoni.

“Tuwaibue watoto waliofichwa nyumbani ili waweze kupata haki ya elimu kama watoto wengine,” alisema mama huyo. “[Watoto hawa] wanatakiwa kujumika na watoto ambao ni wazima ili wajione wako sawa na watoto wengine, wasijione kuwa wametengwa.”

Jackline Kuwanda ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma . Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts