Tanga. Jumla ya shilingi bilioni 429.1 zimetumika katika mradi wa maboresho ya Bandari ya Tanga ulioanza Agosti 2019 kwa lengo la kuiwezesha bandari hiyo kuhudumia meli kubwa ambazo awali hazikuweza kushusha mizigo moja kwa moja bandarini hapo.
Haya yamelezwa na Meneja wa Bandari Tanga, Masoud Athuman siku ya Jumatano Disemba 28, 2022 jijini Tanga wakati akitoa taarifa juu ya utendaji kazi wa bandari na mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Tanga kwa waandishi wa habari wanawake kutoka mikoa mbalimbali walipotembelea bandari hiyo.
“Gharama za Mradi huu kwa awamu ya kwanza uligharimu kiasi cha shilingi Bilioni 172.4″ Masoud alisema wakati akitoa taarifa yake ” Na lengo la mradi huu ilikuwa ni kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 hadi mita 13 na upana wa mita 73 kwenye njia ya kuingiza [na] kutokea meli [1.7 km]” alifafanua zaidi.
Bandari ya Tanga ni miongoni mwa bandari kuu tatu za mwambao za Tanzania bara ambapo kwa mwaka 2021 ilihudumia asilimia 4.7 tu ya shehena zote za mizigo tani 18,082,400 zilizohudumiwa na bandari kuu za mwambao. Huku bandari ya Dar es salaam ikihudumia asilimia 94.2 ya shehena zote na kiasi kilichobaki kilihudumiwa na bandari ya Mtwara.
Awamu ya pili ya maboresho ya bandari ya Tanga ambayo yamefikia asilimia 83 sasa, yalianza Septemba 2020 na yanatarajiwa kukamilika Aprili 2023,takribani bilioni 256.8 zitatumika.
‘’Lengo la mradi huu pia ni kuboresha magati mawili yenye urefu wa mita 450,” Masoud aliongeza kwenye taarifa hiyo kuhusu Bandari ya Tanga, ambayo ndio bandari kongwe zaidi ya kisasa kwenye mwambao wa bahari ya Hindi.
Baada ya maboresho, gati hizo mbili za Bandari ya Tanga zilizojengwa mwaka 1914 na 1958, zitaongezwa mita 50 upande wa Mashariki na mita 92 upande wa Magharibi kuelekea Baharini ikiwa ni pamoja na kuongeza kina cha maji [Draft] Kutoka mita 3 hadi mita 13.
Fursa kwa biashara kimataifa
Bandari ya Tanga mahali ilipo kijiografia ina fursa ya kuhudumia mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara pamoja na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Maboresho yanayoendelea katika bandari ya Tanga yatakapokamilika kwa asilimia 100 yataiwezesha kuwa na uwezo wa kuhudumia shehena mpaka tani za uzito 3,000,000 kutoka uwezo wa kuhudumia shehena za uzito tani 750,000 kabla ya mradi wa upanuzi.
Katibu tawala wa mkoa wa Tanga Pili Hassan Mnyema amesema faida zimeanza kuonekana katika mradi wa maboresho ya bandari ya Tanga yanayoendelea kwani hivi sasa nchi jirani zimeanza kutumia bandari hiyo.
“Faida ambazo zimeanza kupatikana ni pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Rwanda na Burundi kuanza kuitumia bandari yetu ya Tanga kwa sababu inakuwa rahisi tofauti na sehemu nyingine” alisema Mnyema.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ongezeko la shehena katika bandari ya Tanga limekuwa kwa wastani wa asilimia 20 kutoka shehena tani 502,426 mwaka 2017/18 hadi kufikia tani 986,308 mwaka 2021/22 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na bandari hiyo.
Fursa za ajira
Bandari ya Tanga imetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 254 ambapo kati yao, 199 ni wanaume na wanawake ni 55 tu sawa na asilimia 22.
Mwanahamis Salim ni mmoja wa wafanyakazi wa kutwa bandarini hapo ambaye alianza kazi mwanzoni mwa mwaka 2022, anasema fursa ya kazi aliyopata bandarini hapo imemuwezesha kujipatia kipato kinachomsaidia kuendesha maisha yake tofauti na hapo awali.
“Nashukuru nimepata kazi hii. Maana kuna watu wengine wamekaa nyumbani hajui akapate wapi lakini tunashukuru bandari inatusaidia” alisema Mwanahamis.” Hii kutwa ambayo tunaingia inatusaidia kusomesha watoto na kulipa kodi.”
Katika mradi wa maboresho bandari ya Tanga pia inapanua wigo wa sehemu ya kuhifadhia makontena kutoka uwezo wa kuhifadhi makontena 1,000 hadi kufikia uwezo wa kuhifadhi makontena 12,000.
Afisa Masoko bandari ya Tanga, Rose Tandiko anashauri uli kuwe na tija katika uwekezaji unaoendelea ni muhimu baadhi ya bidhaa toka mikoa jirani zikatiliwa mkazo kupitia katika bandari ya Tanga. “Ninachoiomba Serikali yetu katika suala hili, inaweza kuweka maagizo kwamba mazao ya kimakakati yanayozalishwa labda Kilimanjaro, Arusha kama Kahawa,Mkonge yote yapite katika Bandari ya Tanga hii itatuongezea shehena katika Bandari yetu.” alishauri Rose.
Jackline Kuwanda ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com