The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Undani Kuhusu Mtanzania Aliyefariki Nchini Ukraine. Familia Yazungumza

Nemes Tarimo aliuwawa Ukraine akiipigania Urusi, familia inasubiri mwili wake

subscribe to our newsletter!

Dar es salaam. Familia ya Mtanzania aliyeuwawa nchini Ukraine akipigana upande wa Urusi chini ya kampuni binafsi ya Wagner inasubiri kusikia kutoka kwa serikali, ni lini hasa wataweza kupokea mwili wa mpendwa wao kwa ajili ya maziko.

Nemes Tarimo alieyezaliwa Novemba 11 mwaka 1990, aliuwawa Oktoba 24,2022, katika mji wa Bakhmut huko nchini Ukraine, sehemu ambapo kuna mapigano makali zaidi kati ya Urusi na Ukraine toka mwishoni mwa mwaka jana.

Ndugu wa Tarimo wameiambia The Chanzo kwamba wanawasiliana kwa ukaribu na serikali katika juhudi za kuufuatilia mwili wa ndugu yao huku wakitumaini majibu yatapatikana muda si mrefu.

“Kama familia tunasubiri tamko la serikali ndio litatuambia ndugu yetu amekufa kwa kitu gani na pia mwili wake utarudi lini” anaelezea Salome kisale, dada wa Tarimo katika mahojiano na The Chanzo.

Hema kwa ajili ya waombolezaji katika nyumba ya familia Mbezi Msuguri

“Yanaongelewa mengi, ni vitu vingi vimezushwa kuhusu huu msiba lakini kama familia tunasubiri tamko rasmi la serikali”, Kisale aliongeza wakati akiongea na The Chanzo katika nyumba ya familia ya Nemes huko Mbezi Msuguri.

Jitihada zetu kupata ufafanuzi wa serikali hazikufua dafu, hata hivyo Msemaji wa Serikali Ndugu Gerson Msigwa alieleza kuwa halifahamu suala hilo kwa sasa na kuahidi atalifuatilia.

Mr. Andrew Edward Mwandenuka mjomba wa Tarimo na Salome Kisale wanafamilia

Kwa mujibu wa mjomba wa Nemes, Mr Andrew Edward Mwandenuka familia imekuwa ikipokea ushirikiano wa kutosha kutoka serikalini hasa katika kuhakikisha mwili wa Nemes unarudi nchini Tanzania.

“Japo bado [serikali] hawajatupa taarifa rasmi mwili utafika lini, tarehe ngapi lakini tunaendelea kuwasiliana nao, wanafanya jitihada kubwa ili kuwasilisha mwili wa mpendwa wetu” aliongeza Mr Mwandenuka katika mazungumzo na The Chanzo.

Waombolezaji katika makazi ya familia ya Tarimo

Maisha akiwa Urusi

Nemes alisoma katika shule ya Makongo na baada ya elimu ya sekondari alijiunga na Chuo cha Elimu ya Biashara ambapo alimaliza mwaka 2016. Baada ya kumaliza chuo alikaa nyumbani kwa muda mpaka alivyopata ufadhili kwenda kusoma chuo nchini Urusi. Alijiunga na Chuo cha Teknologia cha Urusi-MIREA.

Marafiki zake wa karibu wanaelezea kuwa akiwa masomoni Urusi  Nemes alikua pia akijishughulisha na shughuli za kufungasha mizigo katika kukabiliana na changamoto ya ukali wa maisha mjini Moscow.

Nemes Tarimo akiwa Urusi

Alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na familia yake na marafiki wa karibu muda wote aliokuwa Urusi. Mwaka 2020, Nemes alirudi Tanzania wakati huu akijaribu kutimiza moja ya ndoto yake ya kugombea uongozi. “Alipenda sana masuala ya uongozi”, rafiki yake wa karibu anaiambia The Chanzo.

Wakati huo aliorudi ilikuwa ni kipindi cha uchaguzi mkuu Tanzania. Nemes alishiriki chaguzi za ndani za CHADEMA akiomba ridhaa ya kugombea Ubunge kupitia chama cha CHADEMA katika jimbo la Kibamba. Hata hivyo hakufanikiwa kwani alikuwa wa pili katika kura za maoni za chama.

Nemes akiwa amevalia jezi ya Tanzania

Nemes ambaye anaelezwa na marafiki na majirani kama mtu mpole, anayeongea taratibu na rafiki kwa kila mtu alirudi nchini Urusi mwishoni mwa mwaka 2020. Lakini baada ya muda mfupi toka arudi Urusi mawasiliano yakawa magumu, hakuwa anapatikana tena.

Kukamatwa Urusi

Utafiti wetu baada ya kuangalia nyaraka mbalimbali kutoka Mahakama ya Wilaya ya Moscow, Tarimo alikamatwa majira ya saa kumi na mbili na dakika arobaini jioni Januari 14 mwaka 2021, katika mitaa ya Bekhtereva, Moscow. [Unaweza ukaona nyaraka tulizozipakua hapa na hapa]

Inasemekana kuwa baada ya ukaguzi wa Polisi alikutwa na gramu 5.29 za madawa ya kulevya aina ya methylephedron katika mfuko wake wa koti, madawa yaliyopigwa marufuku nchini Urusi.

Kesi yake ilisajiliwa kama kesi ya jinai kwa namba 12101450081000009 na Tarimo akapelekwa katika mahakama ya wilaya Nagatinskiy Moscow Januari 16,2021, wapelelezi wakitaka wamueke rumande huku upelelezi ukiendelea. Mahakama iliruhusu akae rumande kwa miezi miwili mpaka Machi 15,2021.

Tovuti ya Mahakama ya Moscow ikionyesha kesi ya Nemes

Alirudishwa mahakamani tena machi 10,2021, ambapo wapelelezi waliiomba Mahakama iongeze muda wa kuendelea kumshikilia kwani upelelezi haukukamilika, Mahakama iliridhia ambapo alirudishwa rumande mpaka April 15.Baadae mahakama ikaridhia aendelee kukaa rumande mpaka Juni 15 ikiwa ni miezi mitano bila kesi kuendelea.

Juni 10,2021, Tarimo alirudishwa tena Mahakamani mbele ya Jaji Krutovskaya Larisa Adamovna ambapo Jaji aliridhia aendelee kukaa rumande mpaka Julai 15,2021, upelelezi ukiendelea.

Jaji alieleza kuwa kwa kuwa hana makazi ya kudumu Urusi na hana kazi rasmi kama sababu za kuendelea kuwekwa mahabusu na kutokupewa dhamana. Alirudishwa tena Mahakamani na Mahakama ikaridhia aendelee kukaa mahabusu mpaka Septemba 15,2021.

Picha ya mwisho aliyopost Nemes katika ukurasa wake wa Facebook mnamo Januari 8,2021, siku sita kabla ya kukamatwa

Oktoba 14,2021, Tarimo alifikishwa tena Mahakamani mbele ya jaji Shikareva S.A ambaye aliridhia aendelee kukaa mahabausu mpaka Novemba 15,2021, upelelezi ukiendelea. Hii ikifanya yeye kukaa mahabusu kwa muda wa miezi kumi bila kesi kuendelea.

Kwa mujibu wa sheria za Urusi gramu 5.29 za madawa ya N-methylephedron inahesabika kama ni kiasi kikubwa cha madawa hii ikimaanisha kama angekutwa na hatia angetumikia kifungu cha mpaka miaka 13 gerezani.

Wakati The Chanzo haikuweza kuthibitisha kama Tarimo aliwahi kukutwa na hatia au bado alikuwa mahabusu, taarifa mbalimbali zineleza kuwa akiwa katika kushikiliwa alichukuliwa na kampuni binafsi ya kijeshi ya Wagner.

Nemes katika tukio la kimataifa la vijana nchini Urusi

Kwa mujibu wa ripoti ya BBC, Kampuni ya Kirusi ya Wagner inachangia takribani asilimia 10 ya majeshi ya Urusi yanayopigana nchini Ukraine, maelfu wakiwa ni wafungwa. Wafungwa huchukuliwa wakiahidiwa kupewa msamaha wa vifungo vyao kama wakiipigania Urusi kwa walau miezi sita katika vita nchini Ukraine.

Wapiganaji wa Wagner huwekwa katika sehemu ngumu zenye mapigano makali zaidi ya kivita nchini Ukraine, huku wengi wao hasa wafungwa wakiwa na mafunzo kidogo.

Ripoti Kinzani

Katika hali ya kustaajabisha, taarifa iliyochapishwa Januari 18,2023, na RIA Novosti, chombo cha habari cha serikali ya Urusi, inadai kuwa Nemes alikuwa kifungoni kwa mauaji ambapo Nemes  alisema hana hatia.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa Nemes alizikwa mwanzoni mwa Disemba 2022, katika makaburi ya Goryachiy Klyuch, huku ripoti ikieleza zaidi kuwa ndugu wa Nemes waliridhia azikwe katika nchi ambayo ameipenda na kuifia.

Ripoti hiyo inamtaja Nemes kama shujaa aliyejaribu kumuokoa mwanajeshi mwingine katikati ya makombora makali ndipo umauti ulipomfika. Taarifa hiyo imeendelea kusambaa katika vyombo mbalimbali nchini Urusi.

Nemes katika shughuli za kilimo nchini Tanzania

Mwafrika wa pili anayejulikana kuuwawa Ukraine

Tarimo anakuwa ni Mwafrika wa pili anayejulikana kuuwawa nchini Ukraine akiipigania Urusi.

Mwezi Septemba 2022, taarifa zilisambaa kuwa raia wa Zambia Lemekhani Nathan Nyirenda, 23, alifariki nchini Ukraine akiipigania Urusi. Ripoti zinaonyesha kuwa Nyirenda alikuwa akisoma masuala ya nishati ya Nyuklia katika Chuo cha Fizikia cha Moscow.

Alifungwa April 2020 kwa muda wa miaka 9 na miezi sita kwa makosa ya kukutwa na madawa ya kulevya na alikuwa akitumikia kufungo chake mjini Moscow kabla ya kuchukuliwa na Wagner kwa kuahidiwa msamaha.

Hata hivyo jitihada za Serikali ya Zambia ziliwezesha mwili wa Nyirenda kurudishwa Zambia Disemba 12,2022, ambapo aliagwa na ndugu na jamaa.

Kwa upande wa Nemes, familia yake, marafiki zake, watu waliosoma nae wanaamini haiwezekani akawa anahusika na makosa yeyote yanayohusiana na uhalifu hasa hasa madawa ya kulevya, kwani historia yake na tabia yake inaonyesha hakuwa mtu wa namna hiyo, “hakuwa mtu wa mambo kama hayo, ni vigumu kuhusika” walisema marafiki zake.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *