The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uchakavu wa Madarasa Shule ya Msingi Nanjihi Wawakwaza Wana Nachingwea

Serikali yasema inalitambua tatizo na tayari iko mbioni kulitatua.

subscribe to our newsletter!

Lindi. Wakazi wa kijiji cha Nanjihi, kata ya Kilimarondo, wilayani Nachingwea, mkoani Lindi wameiomba Serikali na wandau wengine wa maendeleo kusaidia ukarabati wa miundombinu ya madarasa katika Shule ya Msingi ya Nanjihi.

Wakizungumza na The Chanzo hivi karibuni, wanakijiji hao wamedai kwamba kumekuwa na uchakavu wa miundombinu ya madarasa kwa muda mrefu katika shule hiyo, hali inayotishia usalama wa wanafunzi.

Wananchi hao walidai kuwa kati ya madarasa manne yanayotumika kwa sasa, madarasa mawili ndiyo yako salama, mawili yaliyobaki ni machakavu lakini bado wanafunzi wanalazimika kuyatumia kwa kusomea.

Nasma Mfikilwa, mkazi wa Nanjihi, aliiambia The Chanzo kwamba hali hiyo inawafanya wazazi wasiwe na amani kuhusu usalama wa watoto wao wanapokuwa shuleni.

“Mzazi anapokuwa nyumbani anawaza kwamba mwanangu atarudi salama kwa sababu madarasa yamejenga nyufa na hizo kenchi za juu zilikuwa zimeshuka kabisa,” alisema Mfikilwa. 

SOMA ZAIDI: Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?

Adrea Ng’ombo, mwanakijiji mwengine, alibainisha kwamba changamoto ya uchakavu wa madarasa kwenye shule hiyo ni ya muda mrefu, hali inayowafanya wanafunzi kupunguza hamu ya kutaka kwenda shule.

“Hii hali ya uchakavu imetuathiri kiasi kwamba hata watoto wengine hawajisikii kuja darasani kutokana na uchakavu wa madarasa jinsi ulivyo, hata raha ya kusoma wao hawajisikii tu,” alisema Ng’ombo.

Kijiji cha Nanjihi kipo pembezoni mwa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea. Kwa mujibu wa wanachi, Shule ya Msingi ya Nanjihi ilijengwa mwaka 1977 na tangu muda huo kijiji kilipata mradi wa kuongeza madarasa mawili ambayo kwa sasa ndiyo yanaonekana kuwa salama na mazuri ukilinganisha na mengine ambayo yalijengwa tangu mwaka huo.

Shule hiyo kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 200 wa kuanzia Darasa la Awali mpaka Darasa la Saba, huku ikiwa na walimu sita.

Wanakijiji wameiomba Serikali iwasaidie kuboresha shule hiyo wakisema mvua zinazoendelea kunyesha zinaifanya hali kuwa mbaya zaidi.

Hamisi Ally Pindepinde ni mzazi wa watoto wawili, mmoja anasoma Darasa la Tano na mwingine akiwa Darasa la Saba katika shule hiyo, ameiomba Serikali iitazame changamoto hiyo kwani imekuwa ni ya muda mrefu sana.

“Serikali itutazame kwa sababu changamoto hii ni ya muda mrefu sana na hatujabahatika kupata majengo,” alisema Pindepinde ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya maendeleo ya elimu kijijini hapo.

“Kutokana na uchakavu huu wa majengo inapelekea mpaka watoto wanakuwa na woga kuishi katika mazingira haya kama hivi tunavyoona kwa macho,” aliongeza.

SOMA ZAIDI: Mpaka Sasa Serikali ya Awamu Ya Sita Imefanya Nini Kwenye Elimu?

Mansed Muni ni Afisa Elimu Maalum wilaya ya Nachingwea aliyeiambia The Chanzo kwamba halmashauri kupitia kitengo cha elimu imepanga bajeti ya Shilingi milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili kwa hatua za mwanzo katika kutatua changamoto hiyo.

“Kwenye changamoto ya miundombinu kwenye Shule ya Msingi Nanjihi, kwenye bajeti zetu tumetenga Shilingi milioni 40 kwa ajili ya madarasa mawili na Shilingi milioni sita kwa ajili ya vyoo vya wanafunzi kwa kuanzia kwa bajeti hii mwaka 2023/2024,” alisema Muni. 

“Lakini tunafahamu kwamba mahitaji ni madarasa manne, ni mategemeo ya idara pia bajeti ijayo ya 2024/2025 tutakamilisha madarasa mengine mawili,” aliongeza afisa huyo.

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Tukiona serikali inatuchelewesha basi tupambane wenyewe kuchangishana michango ili wadogo zetu wapate elimu iliyo bora. Lakini kwa ninavyo wajua wananchi wa nanjihi sijui!!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts