Morogoro. Serikali imetakiwa kushirikiana kwa ukaribu na wananchi katika jitihada za kulinda vyanzo vya maji huku wadau wa huduma hiyo muhimu ya kijamii wakieleza kwamba hakutakuwa na usalama wa nchi kama hakutakuwa na usalama wa maji nchini.
Hayo yalidhihirika hivi karibuni wakati wa warsha maalum ya siku mbili iliyoandaliwa na Shahidi wa Maji, shirika lisilo la kiserikali linalopigania usalama wa maji, kutoka Februari 22 mpaka Februari 23, 2023, mkoani hapa.
Shahidi wa Maji iliwakutanisha wadau wanaohusika na utetezi wa usalama wa maji kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kujadili kwa pamoja namna bora wananchi wanaweza kushiriki kikamilifu katika kulinda vyanzo mbalimbali vya maji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Shahidi wa Maji Abel Dugange alisema ni muhimu kwa wadau wote kuunganisha nguvu na kuhakikisha usalama wa maji nchini.
“Watafiti wanasema kwamba vita itakayokuja ya dunia, kama tusipojipanga vizuri, itakuwa ni vita juu ya maji,” Dugange alitahadharisha. “Sijui kama kuna sekta unaweza kutaja ambayo haitegemei maji. Kwa hiyo, “usalama wa maji ni usalama wa nchi”
Dugange alisema kwamba kwa sasa nchini Tanzania kuna uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji, hali aliyosema inatokana na watendaji wa Serikali pamoja na wananchi kutotimiza wajibu wao, akisema ni lazima watu wapaze sauti kukomesha hali hiyo.
Kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Ulinzi wa Mazingira (NEMC), nchini Tanzania kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji kutokana na kuwepo kwa shughuli za binadamu zinazofanyika pasipo kuzingatia sheria zinazosimamia mazingira na rasilimali maji.
Shughuli zinazochangia uharibifu wa vyanzo vya maji ni pamoja na ukataji wa miti kwa ajili ya kujipatia kuni, mkaa au mahitaji ya ujenzi; mifugo; uchimbaji mchanga na madini; ujenzi usiozingatia taratibu taratibu za mipango miji; na kilimo kisicho endelevu.
Uzembe
Gemma Akilimali ni mwanaharakati wa masuala ya maji na huduma za jamii na Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambaye amehusisha uharibifu huu wa vyanzo vya maji na “uzembe” wa wananchi na watendaji wa Serikali.
“Sisi ni wazembe. Angalia tunavyoachia watu wanaenda kujenga majumba kwenye vyanzo vya maji. Miti inakatwa, miti ambayo ndiyo hii ilikuwa inatusaidia,” Akilimali aliiambia The Chanzo pembezoni mwa warsha hiyo.
“Kwa hiyo, tuna suala kubwa la kutafakari kama taifa,” aliongeza. “Kama kweli tunataka kuja kuliokoa taifa hili, ni lazima tukae chini tuanze kuangalia upya matumizi ya ardhi.”
Akizungumzia suala la ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali ya nchi, Akilimali alishauri kwamba ni muhimu kwa Serikali na idara zinazohusika na maji kuanza kufikiria wapi maji yanapatikana kabla ya kufikiria usambazaji.
“Ni lazima uanze kuangalia chanzo cha maji, kwamba wapi nitapata maji ambayo nitaweza kusambaza,” alisema mdau huyo.
“Kuweka mabomba siyo suluhisho kwa sababu mabomba yalikuwepo na mengine hayana maji, yamekauka,” aliongeza. “Kwa hiyo, unaona kabisa uwekaji wa mabomba siyo suluhisho. Weka mabomba sawa, lakini vyanzo vya maji viko wapi?”
Afisa Programu wa Shirika la Shahidi wa Maji John Muma alisema jitihada zozote zinazolenga ulinzi wa vyanzo vya maji nchini zitashindwa kuzaa matunda kama makundi ya wanawake na vijana yatakuwa hayashirikishwi ipasavyo.
Muma alisema kwamba kwa mujibu wa tathmini yao wao kama shirika, makundi hayo yamekuwa hayashirikishwi ipasavyo kwenye jitihada hizo, kitu ambacho anasema ndiyo kilichowashawishi kuandaa mafunzo hayo ya siku mbili mjini Morogoro.
“Kwa hiyo, mafunzo haya ambayo tumeyatoa yamelenga kuwajengea uwezo vijana na akina mama kuona umuhimu wa kushiriki na kupaza sauti ili kuhakikisha kila kundi linatoa mchango wake pasipo ubaguzi katika utunzaji wa usimamizi wa rasilimali za maji,” alisema John wakati wa mahojiano na The Chanzo.
Ulinzi wa vyanzo vya maji nchini Tanzania unasimamiwa na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Hata hivyo, wadau wamebainisha kwamba suala la utunzaji wa vyanzo vya maji ni la kila mwanajamii na hivyo kutoa wito kwa kila mwananchi kuwa balozi mzuri wa kuona namna ya kuvilinda na kuvitunza vyanzo vya maji.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.