The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Maji Yanavyoinyima Raha Makao Makuu ya Nchi

Huku makisikio yakionesha jiji la Dodoma kuwa na wakazi wapatao 1,972,968 ifikapo mwaka 2051, mamlaka jijini humo ziko mbioni kutafuta vyanzo vipya vya maji.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mamlaka jijini hapa zinaendelea kukuna vichwa kuhusu namna zinavyoweza kuwahakikishia wakazi wake huduma ya kudumu ya maji safi na salama wakati ambao idadi ya watu imeendelea kukua jijini humo tangu Serikali itangaze uamuzi wake wa kuhamia mji huu ulio katikati mwa Tanzania.

Wazo la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi ni kongwe kama ilivyo Tanzania yenyewe, likianza na Rais wa kwanza wa taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere. Hata hivyo, utekelezaji wake ulishika kasi zaidi chini ya Serikali ya Rais John Magufuli ambaye mnamo mwaka 2016 aliagiza ofisi zote za Serikali zihamishie makao yake makuu jijini humo.

Hatua hii imepelekea watu wengi kuhamia Dodoma kwa malengo ya kiutawala na kibiashara, hali iliyoiingiza jiji hilo katika changamoto nyingi ambazo hapo mwanzo hazikuwa na ukubwa kama ule wa sasa. Moja ya changamoto hizi ni huduma ya kupatikana kwa maji safi jijini humo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), mahitaji ya maji katika jiji hilo kwa sasa ni lita milioni 134 kwa siku, huku uwezo wa mamlaka ukiwa ni kuzalisha maji lita milioni 68 tu. 

Kwa mkoa ambao idadi yake ya watu imekuwa kutoka milioni 2.1 mwaka 2012 mpaka 3,086,525, bila shaka kiwango hiki cha maji kinachozalishwa ni kidogo na kinaelezea usumbufu wa kukatika katika kwa huduma hiyo, hali ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi walio wengi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Maji, chanzo pekee cha uzalishaji maji kwa matumizi ya wakazi wa mji wa Dodoma ni visima virefu vilivyochimbwa katika bonde la Makutupora. 

Bonde hilo lipo takribani kilomita 30 kutoka mjini Dodoma ambapo jumla ya visima vya uzalishaji maji 24 na visima vitano vya kuchunguza mwenendo wa maji ardhini vimechimbwa katika bonde hili ambavyo, kwa pamoja, vina uwezo wa usafirishaji maji wa mita za ujazo zipatazo 61,500m3 kwa siku.

Hali hii imeilazimisha Serikali kuja na mikakati mipya inayolenga kutatua kero ya maji jijini Dodoma, ukiwemo ule wa kutaka kuyatoa maji kutoka Bwawa la Maji la Mtera na kuyapeleka mtaani ili kuwapunguzia wananchi usumbufu unaotokana na ukosefu wa huduma hiyo muhimu.

Uvunaji maji Mtera

Mnamo Mei 6, 2023, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji, Nishati, Mazingira na Fedha ilitembelea bwawa hilo linalotumika kwenye uzalishaji wa umeme kuangalia uwezekano wa kutumia bwawa hilo kama chanzo kingine cha maji kwa wakazi wa jiji la Dodoma.

Bwawa la Mtera linakadiriwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo bilioni 3.7 linapokuwa limejaa. Maji ya bwawa hili hutumika kuzalisha umeme kwenye kituo cha Mtera, 80MW, na linatumika kama hifadhi ya maji ya akiba ya uzalishaji umeme kituo cha Kidatu, 204MW.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema Dodoma maji yapo lakini siyo toshelevu, akibainisha kwamba tayari timu ya wataalamu kutoka wizarani ipo kazini kutathmini uwezekano wa kutoka maji kutoka Bwawa la Maji la Mtera na kuyapeleka katikati ya jiji kwa shughuli za binadamu na viwanda.

SOMA ZAIDI: ‘Hayatibu Ugonjwa Wowote’: Zanzibar Yatahadharisha Unywaji wa Maji ya Chemchemi Pemba

“Tumekubaliana kwamba timu ya wataalamu imalize kazi yake na sisi [Serikali], kupitia wataalamu wetu, tutakaa na kujadiliana na kuona ni hatua gani zinazofaa kuchukuliwa kufanikisha jambo hilo,” Aweso, ambaye pia ni Mbunge wa Pangani (Chama cha Mapinduzi – CCM), aliwaambia waandishi wa habari ghafla baada ya ziara hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maji, Jackson Kiswaga, alisema hatua ya Serikali ya kutafuta vyanzo mbadala vya maji kwa ajili ya jiji la Dodoma ni ya muhimu ukizingatia ukuaji wa watu unaoendelea kutokea jijini humo tangu Serikali ihamishie Makao Makuu yake humo.

“Kama kamati tutaenda kukaa na kuchakata yale waliyotueleza wataalamu na kuona ni ushauri gani tutatoa kwa Serikali,” Kiswaga, ambaye ni Mbunge wa Magu (CCM), alisema. “Ushauri wetu utazingatia mahitaji halisi ya maji kwa watu wa Dodoma kulingana na mahitaji ya sasa.”

Hatua za ziada

Mbali na jitihada hizi, Serikali pia kwa sasa inatekeleza mradi wa upatikanaji maji ya uhakika jijini Dodoma unaotekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wa takriban Dola za Kimarekani milioni 125, ambayo ni sawa na takriban Shilingi bilioni 294 za Kitanzania.

Mradi huo ambao utekelezaji wake ulianza Mei 16, 2022, unategemewa kukamilika ifikapo Juni 10, 2027, tayari umeshuhudia awamu ya kwanza ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa hapo Juni 12, 2022, ambalo ujenzi wake umegharimu Shilingi bilioni 292, ikiwa ni sehemu ya fedha hizo za mkopo kutoka AfDB.

SOMA ZAIDI: ‘Usalama wa Maji ni Usalama wa Nchi’

Mradi huo unategemewa kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi, salama na ya kutosha katika jiji la Dodoma na miji ya Bahi, Chemba, na Chamwino. 

Mbali na ujenzi wa Bwawa la Farkwa, fedha hizo kutoka AfDB pia zinategemewa kuiwezesha Serikali kununua mtambo wa kutibu maji; usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji; usanifu wa miundombinu ya kusafirisha maji; usanifu wa miundombinu ya majitaka katika miji ya Bahi, Chemba na Chamwino; pamoja na kujenga uwezo katika usimamizi wa rasilimali za maji.

Kwa mujibu wa taarifa za Serikali, jiji la Dodoma linakadiriwa kuwa na idadi ya wakazi wapatao 500,000, idadi inayotarajiwa kuongezeka hadi kufikia 1,972,968 ifikapo mwaka 2051, hali ambayo inawafanya wataalamu wabainishe kwamba juhudu hizi za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji jijini humo kuwa za muhimu.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts