Tukiwa bado tunaendelea na mjadala wa uwekezaji wa bandari na kampuni ya DP World, lipo fundisho kubwa ambalo kama jamii tunapaswa kujifunza, nalo linahusiana na jamii ya Kitanzania kupoteza uaminifu na imani kwa Serikali yao. Hakuna mtu anayemuamini au mwenye imani na yoyote yule!
Nilitaraji pale inapotokea mgongano wa mawazo, viongozi wakuu wanapotoa ufafanuzi, basi jambo hilo litaeleweka na litakuwa limekwisha. Kwa bahati mbaya, hivyo sivyo, hata pale viongozi wakuu na taasisi mbalimbali zilipojaribu kutoa ufafanuzi bado hazikuaminika na bado maswali mengine yamezidi kujitokeza.
Swali muhimu ambalo tunapaswa tulijadili linahusu ni mambo gani ambayo yamesababisha kuondoka kwa uaminifu na imani? Kwenye makala haya, nakusudia kujadili mambo machache ambayo nadhani yatakuwa yamechangia kutufikisha hapa tulipo.
Zilongwa mbali, zitendwa mbali
Sababu ya kwanza na kubwa kabisa inaendana na ule msemo maarufu wa Kiswahili usemao, zilongwa mbali, zitendwa mbali! Viongozi wanapokuwa matendo yao na vitendo vyao ni mbingu na ardhi, hali hiyo husababisha kuondoka kwa imani na uaminifu.
Wanasiasa wengi wamekuwa wanayohubiri si yale ambayo wanayatenda. Hali hii inaweza kabisa kupelekea wasiaminike tena. Wanasiasa wengi wakati wa uchaguzi na hata wakati mwingine, husimama katika majukwaa na kutoa ahadi nyingi na kubwa ambazo hushindwa kuzitekeleza.
Ilani za vyama vya siasa mara nyingi husheheni ahadi na maneno matamu sana kwa wapiga kura. Kwa bahati mbaya, ahadi hizo kwa miongo na miongo huwa hazitekelezwi.
Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa alipoingia madarakani, alisema kuwa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) haitekelezeki na imesheheni ahadi nyingi mno, hali iliyompelekea kuunda tume ili ifanye mapitio ya ilani hiyo!
Lakini pia mwaka 2020, ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo, ambayo ilinadiwa na Hayati John Pombe Magufuli, iliwaahidi Watanzania kuwa iwapo CCM itapewa dhamana ya kushika dola, basi wangekamilisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya, mchakato ambao ulianzishwa na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.
Baada ya kuingia madarakani, hata hivyo, katika hali iliyowasikitisha wengi, Rais Magufuli alisema kuandika Katiba Mpya haikuwa moja ya vipaumble vyake. Huu ni mfano mmoja tu wa namna viongozi wasivyotekeleza ahadi zao na kuondoa imani na uaminifu kwa wananchi.
Baadhi ya kauli mbiu ambazo zinadhihirisha pengo kubwa kati ya maneno na vitendo ni kama vile Maisha Bora Kwa Kila Mtanzania; Maji Safi na Salama kwa Wote Ifikapo 2000; Tanzania ya Viwanda; Tutajenga Uchumi wa Gesi; kutaja mifano michache.
Unafiki
Si kwa kiongozi tu, bali mtu yoyote anapokuwa si mkweli hupoteza imani na uaminifu wake. Katika moja ya mafundisho ya Mtume Muhammad S.A.W. ni umuhimu wa kuwa mkweli na kusema ukweli.
Katika mafundisho yake, Mtume aliwahi kusema kuwa alama za mnafiki ni tatu: anapozungumza husema uongo; anapoahidi hatekelezi ahadi yake; na anapoaminiwa haaminiki.
Iwapo tunataka kurudisha imani na uaminifu, basi ni vyema sote kwa ujumla, na hasa viongozi, kusema ukweli, kutekeleza ahadi na wanapopewa dhamana basi waheshimu dhamana walizopewa.
SOMA ZAIDI: Jenerali Ulimwengu: Sakata la Bandari Limeonesha Tumepoteza Uwezo Kujadiliana kwa Hoja
Ni muhimu sana kwa kiongozi kutoa kauli thabiti na kuwa na msimamo na muendelezo kwa yale anayoamini na kuyatamka. Ugeugeu unaweza kuondoa imani na uaminifu.
Itakumbukwa, wakati wa sakata la ‘makinikia’ ambapo wananchi waliahidiwa na viongozi wa juu kabisa wa nchi – Rais wa wakati huo – kwamba watapitia mikataba na kuhakikisha neema stahiki inarejea kwa Watanzania na ikafikia hata kumithilisha na ahadi ya kila Mtanzania kupata gari aina ya Noah.
Lakini sote tunatambua hivi karibuni tuliona mwenendo wa kesi ambapo Profesa Abdulkarim Mruma, aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Madini, alivyokuwa anabanwa katika Mahakama ya ICSID,na hukumu ambayo imeigharimu nchi. Hivyo, neema ile iliyoahidiwa imegeuka gharama kubwa zaidi kwa nchi!
Hakuna kuwajibika
Wengi wetu hudhani kuwa kukubali kosa ni kuonyesha kuwa ni wadhaifu. Hivyo tunajipa sifa ya Uungu kuwa sisi hatukosei, hatuna mapungufu, hatufanyi makosa na tunakataa kuwajibika kwa makosa tuliyoyatenda.
Kwa kweli, ni ushujaa mkubwa kwa kiongozi, au yoyote yule, kukubali kosa, kukubali kukoselewa, na kuwajibika kwa makosa tunayoyafanya. Hakuna binadamu asiyefanya makosa. Ni Mungu tu ambaye siyo mkosaji.
Pale viongozi wanapokataa kuwajibika kwa makosa ya waziwazi waliyoyafanya, hupoteza imani na uaminifu kwa watu. Tabia hii pia hujenga kiburi na kuamini kuwa unajua kila kitu.
SOMA ZAIDI: Uwekezaji Bandari ya Dar es Salaam: Ubia wa Uendeshaji ni Bora Kuliko Ubinafsishaji
Ni vyema viongozi, na yoyote yule, wakati wote akakumbuka kuwa huwezi kuwa mkamilifu, na pale unapokosea basi kiri makosa na ikibidi awajibike kwa matendo yake. Hiyo itakuwa heshima, imani na uaminifu.
Ni muhimu sana kwa viongozi kukiri kuwa wanayo mengi ya kujifunza kutoka kwa wanaowaongoza. Ni muhimu wakawapa muda wa kutoa maoni yao na muhimu zaidi kuwasikiliza kwa mtazamo chanya wa kujifunza. Ni kiburi cha hali ya juu kuamini kuwa una majibu ya changamoto zote zinazowakabili wananchi. Sikiliza, na jifunze kutoka kwao.
Katika suala hili sakata la uwekezaji katika bandari na DP World, yapo mengi ambayo yamejitokeza. Lazima tukubali kuwa tumepoteza uaminifu na imani kwa taasisi, Serikali na viongozi. Hali hii ni hatari. Tunatakiwa tuiamini Serikali na viongozi wetu.
Serikali haina budi kuangalia tena mkakati wake wa mawasiliano. Ni nani mtu sahihi wa kutoa ufafanuzi? Je, anaaminika? Je, ana heshima mbele ya jamii? Na je, taarifa zitolewe wakati gani? Na maudhui yake yawe ni yapi?
Nishauri kwamba hili liwafungue macho viongozi wetu. Wanapaswa wajihoji ni namna gani waenende kurudisha imani yao kwa jamii. Viongozi wetu wajiangalie wanavyoishi, na namna kauli na matendo yao yanavyochangia kuangusha imani za wanaowaongoza.
Selemani Rehani ni mchambuzi wa masuala ya siasa na demokrasia. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia selemani.rehani.gac@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.