Search
Close this search box.

Waandishi wa habari wawili kutoka mkoa wa Lindi wamefariki dunia baada ya gari waliyokuwa wakisafiria  kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi kupata ajali majira ya saa 7 za usiku wa kuamkia March 26, 2024 eneo la Nyamwage mkoa wa kipolisi Rufiji, mkoani Pwani. 

Waandishi waliofariki ni Abdallah Nanda wa Channel 10 na Josephine Kibiriti wa Sahara Media Group waliokuwa wawakilishi wa vyombo hivyo vya habari mkoani Lindi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Rufiji [Pwani] Protasi Mutayoka amethibitisha kutokea kwa ajali na kusema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye baada ya ajali alikimbia kwa kuwa eneo hilo la ajali halikuwa na changamoto yoyote ya miumdombinu inayoweza kusababisha ajali. 

Aidha kwa mujibu wa taarifa ya kamanda huyo  ni kwamba katika gari walilokuwa wakisafiria waandishi wa habari hao kulikuwa na watu watatu, mwanamke mmoja na wanaume wawili.  

Baada ya ajali hiyo, mwanaume mmoja alifariki eneo la tukio na mmoja ni majeruhi amelazwa hospitali na mguu wake mmoja umevunjika wakati mwanamke alifariki wakati akipatiwa matibabu. 

Kwa  mwezi Machi 2024, hii ni ajali ya pili iliyohusisha usafiri wa gari kutokea  mkoani Pwani na kupelekea vifo vya watu.  Tarehe 10 Machi,  2024 ajali nyingine ilikoea wilayani Bagamoyo ambapo watu tisa walifariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari la abiria aina ya Toyota Cosater kutoka Dar es salaam kwenda Bagamoyo kugondana uso kwa uso na Lori katika eneo la Kiromo.