Bunge la Tanzania limeazimia kuwa Serikali iangalie umuhimu wa kununua ndege nyingine mpya kwa ajili ya kuwahudumia viongozi wakuu wa kitaifa.
Taarifa hiyo imetolewa Februari 13, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Joseph Mhagama, ambaye ameeleza kuwa nia ya azimio hilo inatokana na Wakala wa Ndege za Serikali kushindwa kuwahudumia kwa wakati viongozi wakuu pale zinapotokea safari kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa Mhagama kamati yake imebaini kuwa kwa sasa kuna ndege tatu zinazowahudumia viongozi wa Serikali. Ndege moja inamhudumia Rais wa Tanzania, ndege nyingine mbili zinawahudumia Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Makamu wa Kwanza na Wa Pili wa Rais wa Zanzibar na viongozi wengine wa kitaifa.
“Hali hii husababisha Wakala [wa Ndege za Serikali] kutekeleza jukumu la kuwahudumia viongozi kwa kuchelewa pindi zinapotokea safari za viongozi wote kwa wakati mmoja,” Mhagama amesema.
“Kwa hiyo basi Bunge linaazimia kwamba Serikali ione umuhimu wa kufanya ununuzi wa ndege nyingine ili kuboresha utoaji huduma za usafiri wa anga kwa viongozi wakuu wa kitaifa.”
Akifafanua suala hili wakati akihitimisha hoja ya Kamati, Mhagama alisema kununua ndege ya viongozi sio kwa ajili ya starehe bali ni kuwahakikishia usalama wao na kuwawezesha kufanya kazi zao vizuri.
“Ipo kasumba kwa baadhi ya Watanzania wenzetu kuamini kila aina ya usafiri ni starehe,” ameeleza Mhagama. “Lakini mheshimiwa Mwenyekiti unajua uwekezaji kwenye vyombo vya usafiri sio wakati wote ni starehe na vyombo vya usafiri sio wakati wote ni hasara wakati mwingine au kwa sehemu kubwa usafiri unaohusu maswala ya utawala ni mali,”
“Watu wanaamini kwamba tungeweza kutumia fedha hizi tunazopendekeza kujenga vituo vya afya na zahanati. Ili haya yote yafanyike ni lazima kuhakikisha kwanza viongozi wanakuwa salama lakini pili wanasafiri kwa haraka ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.”