Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa hakikubaliani na kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji, ambazo zimetolewa kupitia matangazo ya Serikali namba 571, 572, 573 na 574 ya tarehe Julai 12, 2024.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 19, 2024, na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, ambapo ameeleza kuwa msimamo wao huo umetokana na kitendo cha Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupuuza mapendekezo ya CHADEMA kuhusu namna ambavyo kanuni hizo zingeweza kuboreshwa.
Mnyika ameeleza kwa kutokana na hali hiyo, kuna hatua mbili ambazo chama hicho kinahitaji kuzichukua kwa hivi sasa, moja ni kwenda mahakamani kuzipinga kanuni hizo na kuwe na utaratibu wa kisheria utakaowezesha uchaguzi wa haki kwa kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Pili, kuendelea kujiandaa na mapambano na kuwatumia ujumbe wa wazi wezi wa uchaguzi kuwa umma hatutakuwa tayari ya 2019 yajirudie, kwani wanaona kwamba Rais Samia Suluhu Hassan hana nia ya kuendesha uchaguzi ambao utakuwa huru na wa haki.
CHADEMA ilipata nafasi ya kutoa maoni yao kwa TAMISEMI kuhusu kanuni za uchaguzi huo Juni 15, 2024. Moja ya pendekezo lao ambalo halijazingatiwa ni kuhusu kuondolewa kwa mamlaka ya Waziri wa TAMISEMI kwenye uchaguzi huo.