The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Chama cha watu wenye ualbino chalaani tukio la mtoto kutekwa, chataka Rais Samia atoe tamko 

Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) kimelaani na kukemea vikali tukio la kutekwa kwa mtoto mwenye ualbino Asimwe Novath, lililotokea Mei 30, 2024, katika kijiji cha Kamachumu, wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 5, 2024, jijini Dar es Salaam, na Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Godson Mollel, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo. 

Mollel ameeleza kuwa kwa sasa chama hicho kinakusudia kuandika barua ya kuomba kukutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ili naye aweze kutoka kutoa kauli itakayowezesha kukomeshwa kwa ukatili huo, kwani ni aibu kwa nchi inayodai kuwa inathamini utu na haki za watu wake kushuhudia watu wenye ualbino wakiishi kwa mashaka. 

Juni 3, 2024, kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, Yusuph Daniel, alisema kuwa wanawashikilia watu watatu kwa ajili ya mahojiano kutokana na tukio hilo.

Matukio ya watu wenye ualbino kushambuliwa au kutekwa katika kipindi cha hivi karibuni yalipungua, na mwaka 2023 haikuripotiwa kabisa.

Licha ya hali kuonekana shwari, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia ripoti yake ya mwaka 2023 kilitoa angalizo la kuwepo kwa hofu baina ya watu wenye ualbino kwenye baadhi ya maeneo hapa nchini. 

Tanzania yasaini mkataba wa mkopo wa bilioni 422.16 kutoka Korea Kusini 

Serikali ya Tanzania imepokea mkopo kutoka Benki ya Exim ya Korea Kusini wa dola za Kimarekani milioni 163.6 ambazo ni sawa Shilingi bilioni 422.16, kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Binguni, iliyopo visiwani Zanzibar. 

Mkataba wa mkopo huo umesaimiwa jijini Soeul leo June 05, 2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Natu Mwamba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kwa upande wa benki hiyo umesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa hiyo, Hwang Kiyeon.

Uwekaji Saini wa mkataba huo umeshudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Saada Mkuya,  ambaye ameeleza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa watu wa Zanzibar.

Huu unakuwa ni mkopo wa pili wa Tanzania kuchukua kutoka Korea ndani ya kipindi hiki kifupi cha ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini humo. Juni 3, 2024, Tanzania ilisaini mkataba wa mkopo na Serikali ya Korea Kusini wa dola za Kimarekani bilioni 2.5, sawa na Shilingi trilioni 6.2 ambazo Tanzania inategemea kuzipata kwa makubaliano ambayo hayakuwekwa wazi. 

Songwe: Wananchi wafungua kesi dhidi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupinga kuhamishwa

Wakazi takribani 120 wa kijiji cha Ndolezi, mkoani Songwe wamefungua kesi katika Mahakama Kuu kanda ya Mbeya dhidi ya Serikali pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wakipinga mpango wa kuondoshwa kwenye maeneo yao ya asili ili kupisha upanuzi wa hifadhi.   

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 5, 2024, wakili wa kujitegemea, Philip Mwakilima, anayesimamia kesi hiyo kwa upande wa wananchi amesema kuwa mahakama hiyo imewapa siku saba upande wa Serikali za kuanza kuleta hoja zao kwa maandishi ambazo wataziwasilisha Juni 12, 2024. 

Na yeye kwa niaba ya wananchi hao atawasilisha majina ya watu walioweka pingamizi Juni 19, 2024, na shauri litatajwa tena tarehe Julai 10, 2024. 

Mwaka 2022 Serikali iliwataka wananchi hao wakubali kulipwa fidia ili wahamishwe kupisha uanzishwaji wa eneo la hifadhi ya kimondo chini ya NCAA. 

Hata hivyo, zoezi hilo lilidaiwa kuwa lilifanyika kwa kutumia nguvu, huku Jeshi la Polisi likidaiwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika.