The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali yakamilisha mapitio ya sera ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2007 

Serikali imekamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 2024 ambapo zipo changamoto nyingi zilizobainishwa na vijana zinazotokana na baadhi ya maeneo kukosa miongozo. 

Hivyo, kutokana na mapitio hayo imebainishwa kuwa mambo mengi yanayowahusu vijana kupitia sera hiyo mpya yatakwenda kupatiwa ufumbuzi. 

Haya yamebainishwa leo Agosti 12, 2024, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete, wakati akizindua sera hiyo iliyopitiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya vijana duniani. 

Mapitio ya sera hii imekuwa kilio kwa wadau wengi wa masuala ya vijana kwa siku nyingi. Sera hii kwa mara ya kwanza imetambua wigo mkubwa wa shughuli za vijana ikiwemo sanaa, michezo na ubunifu.

Mkutano wa vijana wa CHADEMA washindwa kufanyika. Viongozi, wanachama wakikamatwa

Mkutano wa vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo uliopangwa kufanyika leo Agosti 12, 2024, katika viwanja vya Ruanda Nzovwe huko jijini Mbeya umeshindwa kufanyika mara baada ya Jeshi la Polisi nchini kutangaza kuuzuia mkutano huo hapo jana. 

Katika hatua nyingine jeshi hilo limeendelea na kamata kamata ya viongozi wa chama hicho ambao leo hii wanadaiwa kuwakamata Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Pambalu, ambao walikamatwa mara baada ya kusasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 12, 2024, jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Benson Kigaila amesema kuwa wanachama na viongozi wa chama hicho 443 pamoja na waandishi wa habari watano wamekamatwa tangu jana na mpaka sasa hawana taarifa za ni wapi walipo viongozi wao. 

Kutokana na hali hii vyama vingine vya upinzani wakiongozwa na ACT Wazalendo pamoja na mashirika mbalimbali wameibuka na kulishinikiza Jeshi la Polisi kuwaachilia huru wanachama na viongozi wanaowashikilia pamoja na kuweka mazingira sawa na rafiki ya vyama vya siasa kutekeleza majukumu yao. 

Jeshi la Polisi lakanusha taarifa yake kuhusu kupigwa marufuku kwa mikutano ya hadhara

Jeshi la polisi nchini limesema halijapinga marufuku mikutano ya ndani na ya hadhara ya vyama vya siasa ilimradi mikutano hiyo inafuata matakwa ya sheria za nchi.

Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 12, 2024, kufuatia taarifa iliyotolewa na chama cha ACT Wazalendo ikionesha kuwa Jeshi la Polisi limezuia mkutano wa hadhara wa chama hicho uliopangwa kufanyika katika kata ya Charambe iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam. 

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Polisi wilaya ya Mbagala, Robert John, aliyeeleza kuwa mikutano ya hadhara na ya ndani imezuiliwa hadi hapo yatakapotolewa maelekezo mengine. 

Taarifa iliyokuja kutolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ikaeleza kuwa walichopiga  wamepiga marufuku mkusanyiko wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao ulipangwa kufanyika leo Agosti 12, 2024, huko jijini Mbeya. 

Mikutano wa hadhara iliwahi kuzuiliwa nchini kwa kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka 2016 hadi Januari 2023, hiyo ni baada ya kuibuliwa kwa mashinikizo kutoka kwa wadau mbalimbali hali iliyomfanya Rais Samia Suluhu Hassan kuirejesha tena.