Search
Close this search box.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi yazinduliwa rasmi 

Rais Samia Suluhu Hassan, leo Aprili 3, 2024, amezindua Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na mifumo ya usajili na malalamiko ya ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi, zoezi ambalo limefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Rais Samia ameiagiza tume hiyo kuhakikisha kabla ya kufika mwezi Disemba iwe imezisajili taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi ili kuhakikisha kama zinazingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni chombo kilichoundwa kutokana na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022. Sheria hii inalenga kuweka masharti kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi na kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi zinazochakatwa na vyombo vya Serikali na binafsi. 

Bima ya afya kwa wote kuanza mwezi huu 

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, amesema kuwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote itatangazwa kuanza kutumika kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Aprili kwa tarehe itakayotajwa. 

Dk Mollel amebainisha hayo leo Aprili 3, 2024, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Furaha Matondo, aliyetaka kujua ni lini bima ya afya kwa watu wote itaanza kutumika? 

Dk Mollel ameendelea kufafanua kuwa kuelekea kuanza kutekelezwa kwa mpango huo, Serikali imeshaainisha vyanzo vya mapato vitakavyohudumia watu wasio na uwezo, wakiwemo wajane na watoto wa mitaani. 

Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ulipitishwa na Bunge Novemba 1, 2023, na Rais Samia Suluhu Hassan aliidhinisha iwe sheria rasmi Disemba 5, 2023. 

Kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo huenda kukawasaidia Watanzania kuwa na uhakika wa matibabu na kuuongezea unafuu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao kwa siku za hivi karibuni ulidaiwa kuwa hatarini kufilisika.  

Serikali kufanya tathimini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya pertoli nchini 

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima ili kuondokana na utaratibu wa sasa wa kutofautiana kwa bei kulingana na mkoa.  

Hayo yamesemwa leo Jumatano Aprili 3, 2024, na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo kupitia Chama cha Mapinduzi, aliyehoji juu ya mpango wa Serikali kuweka utaratibu ili bei ya mafuta ya dizeli na petroli iwe moja nchi nzima na mchakato huo utachukua muda gani kuweza kukamilika.

Kapinga ameliambia Bunge kuwa utaratibu huo ulikuwa ukitumika zamani na baadae ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo za kisera na za kiusimamizi.

Hivyo, tathimini hiyo inayoendelea sasa itakapokamilika Serikali itaweza kujiridhisha ikiwa mpango huo utakuwa na tija na kupanga namna bora ya kuusimamia.