Ripoti 21 za CAG zatua bungeni leo
Ripoti 21 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinazohusu ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa Mwaka 2022/2023 zimewasilishwa bungeni leo Aprili 15, 2024, na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande.
Miongoni mwa ripoti hizo zilizowasilishwa ni ripoti ya ukaguzi wa taarifa za fedha za Serikali Kuu, taarifa za fedha za mamlaka za Serikali za mitaa na taarifa za fedha za miradi ya maendeleo.
Nyingine ni taarifa za fedha za mashirika ya umma, ufanisi na ukaguzi maalumu, mifumo ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), upatikanaji wa huduma za afya ya akili na udhibiti wa vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya vya umma.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, aliwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Machi 28, 2024, ambapo alisema katika mwaka huo ametoa jumla ya hati 1,209 za ukaguzi. Kati ya hati hizo, zinazoridhisha ni hati 1197, sawa na asilimia 99. Hati zenye shaka ni tisa, sawa na asilimia 0.7. Hati mbaya ni moja, sawa na asilimia 0.1, pamoja na hati nyingine mbili ambazo CAG alishindwa kutoa maoni.
Kichere pia aliyataja mashirika ya umma kadhaa yaliyotengeneza hasara, akitaka hatua zichukulie ili hali hiyo isijirudie. Mashirika hayo ni kama vile Shirika la Ndege (ATCL), Shirika la Mawasiliano (TTCL), Shirika la Reli (TRC), Kampuni Tanzu ya Mafuta (TanOil ) na Shirika la Posta.
Makonda kuwataja mawaziri wanaoendesha mpango wa kumtukana Rais Samia?
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, leo Aprili 15, 2024, alitarajiwa kuwataja baadhi ya mawaziri aliodai kuwa wanawalipa watu kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan, lakini mpaka dakika hii alikuwa bado hajafanya hivyo.
Makonda alisema hivyo Aprili 12, 2024, wakati wa hafla ya kumbukumbu ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, iliyofanyika Monduli Juu, mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi wakuu mbalimbali, akiwemo Rais Samia mwenyewe.
Makonda, anayejitambulisha kama mtoto wa pekee wa kiongozi huyo mkuu wa nchi, alisema kuwa anawafahamu mawaziri hao na endapo wataendelea kufanya hivyo angeyaweka majina yao hadharani leo hii.
Hii isingekuwa mara ya kwanza kwa Makonda kuwaweka hadharani watu anaodai wanafanya makosa fulani. Mwaka 2017, wakati akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, aliyaweka hadharani majina ya watu aliodai kuwa wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Hata hivyo, wakati huu imekuwa tofauti kwani tuhuma zake alizelekeza kwenye Baraza la Mawaziri ambalo kwa mujibu wa katiba ndilo ambalo linaunda Serikali.
TBS yawataka wananchi wafuate maelekezo ya matumizi ya ‘Energy Drink’
Shirika la viwango Tanzania (TBS) limewataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa kwenye vinywaji ili kuepuka madhara ya kiafya ambayo yanatokana na kutofuata maelekezo wakati wa matumizi ya vinywaji hivyo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Aprili 15, 2024, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka TBS, Lazaro Msasalaga, amesema kuwa shirika hilo limekuwa likidhibiti viwango vya viambata vinavyotakiwa kuwekwa kwenye vinywaji kama ‘Energy Drink’ na pombe kali, lakini watumiaji wake ndiyo hunywa vibaya.
Akitolea mfano kuwa, maelekezo yaliyotolewa na wazalishaji ni kuwa mtu anywe chupa moja ya ‘Energy Drink’ kwa siku, agizo ambalo anadai halifuatwi na wengine wanatumia kinywaji hicho pasipo kula, hali ambayo hupelekea athari za kiafya kama vile mgonjwa ya moyo na figo.