The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Watanzania 17,850 wakabidhiwa nishani za miaka 60 ya muungano

Kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya muungano hapo Ijumaa ya Aprili 26, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan leo Aprili 24, 2024, amewatunuku nishani za miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Watanzania 17,850, zoezi ambalo limefanyika Ikulu, jijini Dodoma. 

Nishani alizowatunuku ni pamoja na nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nishani ya mwenge wa uhuru daraja la pili, nishani ya utumishi uliotukuka, nishani ya utumishi mrefu na tabia njema, nishani ya utumishi mrefu pamoja na nishani ya kumbukumbu ya muungano. 

Baadhi ya watu waliokabidhiwa nishani hizo ni pamoja na Hayati Rais John Pombe Magufuli, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Mkuu wa Majeshi, Jacob Mkunda pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillus Wambura. 

Sambamba na hilo, Rais Samia amezindua vitabu viwili vya muungano, kikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ofisi ambayo imekuwa ikishughulikia masuala ya muungano hapa nchini. 

Akizungumza mara baada ya kuzindua vitabu hivyo, Rais Samia amewataka Watanzania kudumisha amani na mshikamano wa taifa la Tanzania, kufanya kazi kwa bidii na kudumisha uzalendo kama sehemu ya kuwaenzi waasisi wa muungano huu. 

LHRC: Hali ya haki za binadamu mwaka 2023 ilidorora ikilinganishwa na mwaka 2022

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimebainisha kuwa hali ya haki za binadamu kwa mwaka 2023 ilidorora ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2022 kwa sababu kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za kiraia na kisiasa.  

Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 24, 2024, wakati kituo hicho kilipokuwa kinazindua ripoti yake ya 22 ya haki za binadamu kwa mwaka 2023, zoezi ambalo limefanyika kwenye makao yake makuu yaliyopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam. 

Akizitaja haki kuu ambazo zilikiukwa sana kwa mwaka 2023, afisa utafiti kutoka LHRC, Fundikila Wazambi, amezitaja kuwa ni haki ya kuishi, uhuru dhidi ya ukatili, haki ya usawa mbele ya sheria, haki ya kuwa huru na salama pamoja na uhuru dhidi ya utesaji. 

Wazambi ameendelea kubainisha kuwa, kundi la watoto ndiyo limeonekana kuwa waathirika wakubwa wa ukiukwaji wa haki zao kwa asilimia 45 wakifuatiwa na wanawake ambao ni waathirika kwa asilimia 30, viwango ambavyo vimepungua ukilinganisha na mwaka jana. 

Kwa upande wa makundi ya wazee na wanaume, kiwango cha ukatili kimeonekana kuongezeka, ambapo wazee ni asilimia 12 kutoka asilimia 10 ya mwaka 2022 na wanaume pia ni asilimia 10 kutoka asilimia sita ya mwaka 2022. 

Ripoti hiyo kwa sasa inapatikana bure kupitia tovuti ya LHRC.  

Maombi ya leseni za madini 227 yafutwa 

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amebainisha kwamba Serikali, kupitia Tume ya Madini, imefuta jumla ya maombi ya leseni 227 ambayo yamekosa vigezo vya kuendelea kufanyiwa kazi.

Hayo ameyasema leo Aprili 24, 2024, jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari. 

Mavunde amesema kuwa maombi hayo yamefutwa kutokana na sababu ya kutolipiwa ada stahiki za maombi kwa mujibu wa sheria pamoja na kukosa nyaraka zinazotakiwa kuambatanishwa na maombi hayo. 

Ndani ya miezi miwili hii, Serikali itakuwa imefuta jumla ya maombi 2,875 kwa sababu Machi 22, 2024, Serikali ilitangaza kufuta maombi na leseni za utafiti 2,648 ambayo yalibainika kuwa na makosa mbalimbali. 

Nchini Tanzania, sekta ya madini ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wananchi. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2022/2023, migodi ilifanya manunuzi ya dola za Kimarekani bilioni 1.6, ambapo dola bilioni 1.4 zilihusisha kampuni za Kitanzania na hivyo kufanya zaidi ya asilimia 86 ya manunuzi yote ya migodi katika mwaka huo yawe yamefanywa na Watanzania.