The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

TRA yakusanya kodi Shilingi bilioni 12 kutoka kampuni za nje ikiwemo Google 

Kwa mara ya kwanza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hadi kufikia Machi 2024 imekusanya kodi Shilingi bilioni 12 kutoka kampuni zinazofanya kazi Tanzania lakini hazina ofisi mama nchini ikiwamo kampuni ya Marekani ya Google LLC. 

Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 29, 2024, jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Hudson Kamoga, muda mfupi baada ya kuwasilisha mada katika mkutano mkuu wa 13 wa Kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaohudhuriwa na wanachama zaidi ya 150. 

Kamoga amesema kodi hiyo imekusanywa baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 na akazitaja kampuni zingine za mtandaoni ambazo kwa mujibu wa sheria hiyo zinapaswa kulipa kodi hiyo na zimeanza kulipa kuwa ni Tiktok, Facebook na Netflix.

Serikali kuanza kulipa madeni ya vyombo vya habari ya zaidi ya bilioni 18

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema kuwa Serikali imeanza kufanya mipango ya kulipa deni la zaidi ya bilioni 18 inayodaiwa na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Nnauye ameyasema hayo leo Aprili 29, 2024, katika mkutano mkuu wa 13 wa mwaka wa kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaoendelea jijini Dodoma. 

Kiongozi huyo amesema kati ya Shilingi bilioni 18 zinazodaiwa, Shilingi bilioni tano ni deni kutoka kwenye halamashauri ambazo hazioneshi dalili za kupunguza au kulipa deni hilo na kiasi kinachobakia ni deni kutoka kwenye taasisi za Serikali. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko, ameeleza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati kulipa madeni hayo ili kuepuka kudhoofisha vyombo vya habari. Aidha, amewataka wanaodaiwa kutoa taarifa za kina kuhusu deni hilo ili hatua za kulipa ziweze kuchukuliwa haraka.  

Mbunge ataka adhabu ya kifo iondolewe kwa sababu haitekelezwi

Mbunge wa viti maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi Shally Raymond ameishauri Serikali ipeleke muswada bungeni kwa ajili ya kuiondoa adhabu ya hukumu ya kifo kwa sababu imekuwa haitekelezwi kwa muda wa takribani miaka 30 sasa. 

Shally amependekeza suala hilo leo Aprili 29, 2024, wakati akichangia hoja mara baada ya kuwasilishwa kwa hotuba ya Waziri Katiba na Sheria, Pindi Chana, kuhusu Mpango wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025.

Kwa mujibu wa Shally hukumu hiyo imekuwa ikiwaweka mahabusu watu waliohukumiwa kunyongwa kwa muda wa miaka 10 hadi 20 pasipo kutekelezwa, kitu ambacho anadai kuwa si haki. 

Ripoti ya haki za binadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2023 ilirekodi hukumu 37 za adhabu ya kifo. 

Hukumu hii imekuwa ikipigiwa kelele na wadau mbalimbali kuwa iondolewe kwa sababu mara ya mwisho kutekelezwa ilikuwa ni mwaka 1994, wakati wa utawala wa Hayati Ally Hassan Mwinyi.