The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

LHRC yaitaka Serikali iwasilishe muswada wa mabadiliko ya katiba

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka Serikali iwasilishe bungeni muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba ili kuruhusu baadhi ya masuala yanayogusa uchaguzi kuweza kufanyiwa marekebisho. 

Kituo hicho pia kimeitaka Serikali itekeleze uamuzi wa Mahakama Kuu, katika shauri la mwanaharakati Tito Magoti, dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyowapa wafungwa haki ya kupiga kura. 

Wito huo imetolewa leo Aprili 4, 2024, na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya kituo hicho yaliyopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam. 

Henga alikuwa akichambua sheria nne za uchaguzi zilizotangazwa kuwa zimesainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 2, 2024, hivyo kuruhusu utekelezaji wake kuanza. 

Sheria hizo nne za uchaguzi zilipitishwa na Bunge licha ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wadau kwamba mapendekezo yao juu ya kuziboresha kwa kiwango kikubwa hayakuzingatiwa na mhimili huo wa utungaji sheria nchini.

Dawa za kulevya kilogramu takribani 54,506 zanaswa

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata takribani kilogramu 54,506 za dawa za kulevya za mashambani na viwandani pamoja na kuteketeza ekari 262 za mashamba ya bangi katika kipindi cha mwezi Februari na Machi 2024. 

Dawa hizo zimekatwa kufuatia operesheni iliyoendeshwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na Wakala wa Misitu (TFS), katika mikoa ya Shinyanga, Tabora, Iringa, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam. 

Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 4, 2024, na Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, wakati akiongea na waandishi wa habari,  jijini Dar es Salaam. 

Lyimo ameeleza kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kuwakamata watu 72 wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo na tayari baadhi yao wamefikishwa mahakamani. 

Tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya limekuwa likiwaathiri vijana wengi hapa nchini. Takwimu kutoka kwenye vituo vya tiba saidizi kwa waraibu wa kutumia dawa za kulevya zinaonesha jumla ya waraibu wapya 2,219 wamejiunga na tiba hiyo kwa mwaka 2023 na kufanya idadi ya waraibu wanaopata tiba ya Methadone kufikia 15,915.

Rais Samia: Jamii Namba itarahisisha utoaji huduma na ulinzi nchini

Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, ahakikishe anasimamia vyema zoezi la kuhakikisha kila Mtanzania ana namba moja ya utambulisho iliyopewa jina la Jamii Namba.  

Kauli hiyo ameitoa leo Aprili 4, 2024, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akiwaapisha viongozi mbalimbali wa Serikali aliowateua katika siku za hivi karibuni. 

Rais Samia ameeleza kwamba utaratibu huo kwa kiasi kikubwa utarahisisha zoezi la utoaji huduma na ulinzi nchini. Lakini pia, itaondoa usumbufu uliopo sasa unaowalazimisha watu kumiliki namba za utambulisho zaidi ya moja. 

Kwa mara ya kwanza Rais Samia alitoa agizo hili Agosti 10, 2023, baada ya kutoridhishwa na utitiri wa namba zinazotumika na Watanzania. 

Machi 12, 2024, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba, alisema kuwa mpango huo umeshaanza na unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2025.