The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Watu 15 wafariki dunia kwa kusombwa na maji ya mvua

Watu 15 wakiwemo watoto 12 pamoja na watu wazima watatu wamethibitishwa kufariki dunia baada ya kusombwa na maji ya mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali nchini. 

Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 8, 2024, na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ambapo ameeleza kuwa kuwa watu hao wamefariki katika matukio tofauti tofauti yaliyotokea kati ya Aprili 1 na Aprili 7, 2024. 

Misime ameitaja mikoa ambayo matukio hayo yametokea kuwa ni Rukwa, Lindi, Njombe, Tanga, Pwani, Manyara, Geita na Mbeya. 

Kutokana na mfululizo wa matukio hayo yaliyoelezwa kuwa yametokea katika kipindi kifupi, Jeshi la Polisi limewataka watu wote kuwalinda watoto kwa karibu sana ili kuwaepusha na madhara yanayotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mbunge ataka majibu ya Waziri Mkuu kuhusu vikwazo walivyowekewa wakazi wa Ngorongoro

Mbunge wa Ngorongoro kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Emmanuel Ole Shangay, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aeleze mpango wa Serikali dhidi ya wananchi wa Ngorongoro baada ya Serikali kutowapatia huduma za kijamii wananchi hao kwa muda wa miaka mitatu sasa. 

Kauli hiyo ameitoa leo Aprili 8, 2024, wakati alipokuwa akichangia mjadala wa Bunge la 12 linaloendelea huko jijini Dodoma.  

Kiongozi huyo amedai kuwa wakazi wa Ngorongoro wamewekewa vikwazo vinayowafanya washindwe kufanya shughuli za kimaendeleo lakini pia hawapewi huduma kama vile elimu, afya na maji. 

Mwaka 2022 Serikali ilianzisha mpango ulioelezwa kuwa ni wa hiari wa kuwahamisha wakazi wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwenda kijiji cha Msomera, wilaya ya Handeni, mkoani Tanga. Lengo likiwa ni kulinda eneo hilo linalotambuliwa kuwa ni la urithi wa dunia. 

Hata hivyo utekelezaji wa mpango huo umekuwa ukipingwa vikali na wadau mbalimbali wakiwemo watetezi wa haki za binadamu, kwa madai ya kuwa umegubikwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. 

Serikali kujenga mabwawa mawili Rufiji kuepusha mafuriko

Wizara ya Kilimo inategemea kutangaza zabuni ya kuanza ujenzi wa mabwawa mawili katika eneo la chini ya Bwawa la Uzalishaji Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ikiwa kama hatua ya kukabiliana na mafuriko kwenye wilaya za Rufiji na Kibiti, mkoani Pwani. 

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Aprili 8, 2024, na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, wakati akijibu maswali ya nyongeza ya mbunge wa viti maalumu, Subira Mgalu, aliyehoji kama Serikali haioni haja ya kujenga mradi huo ili kuendana na mradi wa Kujenga Kesho Iliyobora (BBT).

Jana Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kwenye ukurasa wake binafsi wa mtandao X alisema kuwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mabwawa hayo umekamilika. Aprili 20, 2024, miradi hiyo itatangazwa na kwamba watavuna maji na hivyo mafuriko ya Rufiji na Kibiti yatakwenda kuwa historia. 

Kwa sasa wilaya ya Rufiji imekumbwa na mafuriko yaliyopelekea nyumba 58 kuharibika. Wananchi 951 wameondolewa kwenye makazi yao huku hekta 28,374.74 za mazao ya kilimo na biashara zikiathiriwa. Mafuriko hayo yanadaiwa kutokana na maji yaliyofunguliwa kutoka Bwawa la Uzalishaji Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).