Habari za jioni! The Chanzo inakueletea habari kubwa zilizoripotiwa siku ya leo Ijumaa, Februari 16, 2024 hapa nchini Tanzania.
Bunge Laipa Muda Zaidi Serikali Kumaliza Mgao wa Umeme
Bunge la Tanzania limeipa muda wa miezi mitatu zaidi Serikali hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu tatizo la mgao wa umeme ambalo limekuwa likiwaathiri Watanzania wengi katika siku za hivi karibuni liwe limekwisha.
Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 16, 2024 na Spika wa Bunge Tulia Ackson mara baada ya Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga, kueleza kuwa wanatarajia kumaliza tatizo hilo mwezi Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kapinga hadi kufikia mwezi Machi Serikali itakuwa imeshawasha mitambo miwili katika bwawa la kuzalishia umeme la Mwalimu Nyerere. Mitambo hiyo inatarajiwa kuzalishia megawati 470 ambazo anadai zitakwenda kumaliza tatizo la mgao wa umeme.
Katika hotuba ya mwaka mpya 2024, Rais wa Tanzania alitangaza kuwa makali ya mgao wa umeme kupungua Februari 2024. Hii ni baada mwezi September 2023, kuwapa miezi sita TANESCO kumaliza mgao yaani ifikapo Machi, 2024.
Wizara ya Nishati ilithibitisha tena Bungeni kuwa makali ya mgao kukoma Februari 16, 2024 utakapowashwa mtambo mmoja wa uzalishaji wa umeme Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Bunge laazimia sharti la kupita JKT, JKU kupata ajira vyombo vya ulinzi na usalama liondolewe
Bunge limeazimia kuwa sharti la ili mtu aweze kupata ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama basi lazima amewahi kupata mafunzo kutoka Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Kujenga Uchumi liondolewe.
Azimio hilo limepitishwa leo Februari 16, 2024 mara baada ya mbunge wa Mbozi George Mwenisongole kupitia CCM, kuhoji juu ya sharti hilo akibainisha kuwa limepelekea baadhi ya watu wenye sifa za kujiunga na vyombo hivyo kukosa nafasi.
Sharti la kupita JKT ili kujiunga na vyombo vya ulinzi na usalama lilitokana na majukumu iliyopewa JKT tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963. Moja ya majukumu hayo yalikuwa ni pamoja na kuwalea vijana katika maadili, kuwapa mafunzo ya awali ya ulinzi na kuwajengea uzalendo.
Vijana wa Tanzania hujiunga na JKT kupitia makundi mawili yaliyowekwa kisheria. Kundi la mujibu wa Sheria, ambalo linajumuisha waliohitimu kidato cha sita na vyuo vya kati. Kundi la pili ni wale wa kujitolea ambao huandikishwa baada ya kutuma maombi na kufanyiwa usahili na Kamati za Ulinzi na Usalama.
Ripoti ya Sauti za Waandishi yabainisha kuwa hali ya sekta ya habari si yakuridhisha
Kuingiliwa kwa uhuru wa kuzalishia maudhui, hali mbaya ya kiuchumi kwa waandishi wa habari na vyombo vyao, kufanya kazi bila ya mikataba ya ajira, rushwa pamoja na maafisa wa Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuwanyanyasa waandishi ni baadhi ya mambo ambayo utafiti wa ripoti ya Sauti za Waandishi umeyabainisha.
Hayo yameelezwa leo Februari 16, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilokuwa na kiserikali la Twaweza Aidan Eyakuze wakati akizindua utafiti huo unaoelezea maoni na uzoefu wa waandishi wa habari nchini kuhusu sekta ya vyombo vya Habari kuanzia Septemba hadi Novemba 2023. Ambapo jumla ya waandishi wa habari 1,202 walishiriki kutoa maoni.
Pamoja na sekta ya habari kuelezwa kupitia katika kipindi kigumu kwa sasa Eyakuze amebainisha asilimia kubwa ya wahojiwa wameonesha kuwa na matumaini na kipindi cha miaka mitano hadi 10 ijayo wakiamini kuwa itazidi kubadilika lakini kamwe haitotoweka.