The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Rais Samia Suluhu: Mfuko wa PSSSF una hali mbaya iliyosababishwa na uongozi, Serikali 

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa hali ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni mbaya na inatokana na utendaji mbovu wa viongozi wake pamoja na Serikali, kitu ambacho kimepelekea wafanyakazi kuwa na mzigo mkubwa.  

Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 11, 2024, wakati akipokea gawio na michango kutoka mashirika na taasisi za umma, hafla ambayo imefanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam. 

Kiongozi huyo mkuu wa nchi ameongeza kuwa pamoja na mfuko huo kuwa na hali mbaya bado wanafikiria kuendelea kuwekeza kwenye miradi mbalimbali licha ya kuwa tayari wanamiradi ambayo wamewekeza ikafeli baada ya kushindwa kuzalisha na mingine inazalisha kwa kiwango kidogo sana. 

Hivyo, amemtaka Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, kwenda kuyasimamia mashirika kama hayo kwa kuhakikisha yanafanya uwekezaji utakaozalisha ili wastaafu waweze kupata pesa zao kwa wakati bila kusubiri na kwa mujibu wa sheria.

Rais Samia amtengua mkuu wa mkoa Simiyu, Yahaya Nawanda 

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametengua uteuzi wa mkuu wa mkoa wa Simiyu, Yahaya Ismail Nawanda, na kutangaza kuwa nafasi hiyo itachukuliwa na Kenan Laban Kihongosi ambaye kabla ya hapo alikuwa mkuu wa wilaya ya Momba.

Taarifa za utenguzi zimetangazwa leo Juni 11, 2024, siku moja tangu zilipoanza kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikimuhusisha Nawanda na tukio la kumuingilia kinyume na maumbile binti mmoja anayedaiwa kuwa wanafunzi wa chuo. 

Taarifa hizo zilidai kuwa kiongozi huyo alitekeleza tukio hilo ndani ya gari wakati akiwa jijini Mwanza, eneo la Rock City Mall kwenye eneo la kuegesha magari la baa ya Cask. 

Siyo mara ya kwanza kwa kiongozi kutenguliwa baada ya kuibuka kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ukatili. 

Novemba 25, 2023, Rais Samia alitengua uteuzi wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul, baada ya kudaiwa kumfanyia udhalilishaji kijana mmoja mkazi wa Babati, mkoani Manyara aliyefahamika kwa jina la Hashimu Ally. 

Serikali kufanya tathmini kubaini iwapo kuna haja ya kuwa na sheria mahususi ya ukatili wa kijinsia

Wizara ya Katiba na Sheria imesema kwa kushirikiana wizara nyingine na asasi za kiraia inafanya tathmini ili kubaini iwapo ipo haja ya kuwa na sheria mahususi ya ukatili wa kijinsia au iboreshe sheria zilizopo.

Akiongea bungeni jijini Dodoma, leo Juni 11, 2024, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amesema tathmini hiyo ikikamilika itasaidia Serikali kufanya uamuzi sahihi kuhusu suala la kutunga sheria mahususi kwa makosa ya ukatili wa kijinsia au kuboresha sheria zilizopo.

Taasisi mbalimbali zinazohusika na utetezi wa haki za binadamu zimekuwa zikiitaka Serikali kuona umuhimu wa kuwa na sheria mahususi ya kuzuia ukatili wa kijinsia.

Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2023 inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imeonesha kuwa kuna umuhimu wa uwepo wa sheria hii kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kuendelea kuongezeka.

Tanzania hakuna sheria mahsusi dhidi ya ukatili wa kijinsia au ukatili wa majumbani, makosa mengi ya ukatili yapo katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu (The Penal Code Cap. 16).