The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau walaani mauji ya mtoto mwenye ualbino 

Wadau mbalimbali nchini wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, leo Juni 18 2024, wamejitokeza hadharani kulaani na kukemea vikali mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath, ambaye alitekwa na watu wasiojulikana Mei 30, 2024, wakati akiwa nyumbani kwao na mwili wake ukapatikana jana Juni 17, 2024, ukiwa hauna baadhi ya viungo.  

Akizungumza kwa uchungu bungeni kuhusu tukio hilo ambalo limetokea wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, mbunge wa viti maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi anayewakilisha watu wenye ulemavu, Khadija Shaaban maarufu kama Keisha, ameiomba Serikali itunge sheria kali zitakazokomesha mauaji hayo. 

Khadija ameongeza kuwa watu wenye ualbino hawana amani na wanaamini kuwa katika kipindi hiki cha uchaguzi kinaweka maisha yao hatarini kutokana na uwepo wa imani hasi zilizojengwa kwa watu wenye ulbino.  

Matukio ya watu wenye ualbino kushambuliwa au kutekwa katika kipindi cha hivi karibuni yalipungua, na mwaka 2023 haikuripotiwa kabisa.

Licha ya hali kuonekana shwari, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia ripoti yake ya mwaka 2023 kilitoa angalizo la kuwepo kwa hofu baina ya watu wenye ualbino kwenye baadhi ya maeneo.

Tanzania yaanza kujenga majengo ya kitega uchumi nje ya nchi 

Tanzania imeanza kutekeleza mpango wake wa kujenga majengo ya kitega uchumi kwenye mataifa mbalimbali kwa kuzindua ujenzi wa majengo pacha yenye ghorofa 22 kila moja huko Upper Hill, katikati mwa jiji la Nairobi, majengo ambayo pia yatakuwa ni makazi ya ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Akizungumza kuhusu mpango huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo itahusisha majiji ya Nairobi, Kigali, Kinshasa, London, New York na Lusaka ambapo Serikali itapata takribani Shilingi bilioni 36 kwa mwaka kutokana na uwekezaji huo.

Makamba ameongeza kuwa kwa sasa Serikali inatumia takriban Shilingi bilioni 29 kwa mwaka kwa ajili kukodisha ofisi za ubalozi na nyumba za watumishi wa ubalozi kitu ambacho mpango huo utakwenda kikutatua. 

Kwa sasa Serikali ya Tanzania inamiliki takriban majengo na viwanja 101 duniani kote ambapo vingi vipo katika maeneo ya miji mikuu. Katika jiji la Lusaka pekee Serikali inamiliki majengo na viwanja 11. 

Spika Tulia Ackson ataka Mpina ahojiwe na Kamati ya Haki na Maadili

Spika wa Bunge, Tulia Ackson, leo Juni 18, 2024, ametoa maelekezo kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imuhoji mbunge wa Kisesa kupitia Chama cha Mapinduzi,  Luhaga Mpina, kwa madai ya utovu wa nidhamu ikiwemo kudharau mamlaka ya Spika na kumkabidhi taarifa yao Juni 24, 2024.  

Kauli hii ya Spika inatokana na Mpina kumtuhumu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuwa alilidanganya Bunge kuhusu vibali vya kuagiza sukari na hivyo kutakiwa kuwasilisha ushahidi wake mbele ya Spika.

Spika amesema licha ya Mpina kuwasilisha ushahidi huo, kabla ya hatua kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na Kamati ya Bunge kuifanyia uchunguzi, Mpina aliwasilisha madai hayo kwenye vyombo vya habari, kitendo ambacho kimeelezwa kuwa ni kinyume na kanuni za Bunge.

Juni 4, 2024, wakati wa mjadala wa hoja ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka fedha 2024/2025, Bashe alisema kwamba kampuni na viwanda vya sukari vilivyopewa dhamana na Serikali ya kuhakikisha kunakuwa na sukari ya kutosha vimeshindwa kutekeleza wajibu huo kwa kushindwa kuagiza bidhaa hiyo, hali ambayo ilisababisha uhaba wa sukari nchini.