Watatu washikiliwa na polisi Kagera kwa tuhuma za wizi wa mtoto mwenye ualbino
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, Yusuph Daniel, amesema kuwa wanawashikilia watu watatu kwa ajili ya mahojiano kutokana na tukio la kuibiwa kwa mtoto wa kike mwenye ualbino, Asimwe Novath (2).
Tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Kamachumu, wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, mnamo Mei 30, 2024, ambapo siku ya tukio watu wawili walifika nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo wakiomba chumvi ili kumtibu mmoja wao aliyedaiwa kuwa ameng’atwa na nyoka.
Wakati mama wa mtoto huyo akiendelea kutoa msaada huo ndipo ambapo mmoja wa watu hao alipomnyakua mtoto huyo na kutokomea kusikojulikana hadi hivi sasa.
Kutokea kwa tukio hili kumeibua hali ya sintofahamu miongoni mwa watu wenye ualbino hapa nchini kwa sababu katika miaka ya hivi karibuni matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino yalipungua kwa kiasi kikubwa.
Ripoti ya Haki za Binadamu (2023) inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaonesha kuwa kwa mwaka 2023 hakukuwa na tukio lolote la kushambuliwa wala kuuawa kwa watu waishio na ulemavu huo wa ngozi.
Aidha, ripoti hiyo ilieleza kuwa licha ya kutokuwepo kisa cha mauaji ama kushambuliwa bado watu hao wenye ulemavu wa ngozi walikuwa wanaishi kwa hofu na mashaka.
Zuio usafirishaji wanyama hai nje ya nchi latajwa kuwaumiza wafugaji wa vipepeo, Serikali kuja na suluhu
Serikali imesema kuwa inalifanyia tathimini zuio la usafirishaji wa vipepeo nje ya nchi baada ya kubainika kuwa hatua hiyo imepelekea wafugaji wake kukosa soko la uhakika la ndani.
Hayo yamesemwa leo Mei 3, 2024, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dastan Kitandula, wakati akijibu swali la mbunge wa Donge kupitia Chama cha Mapinduzi, Mohamed Jumah Soud, aliyetaka kufahamu juu ya ruhusa ya kuuza vipepeo wafugwao nje ya nchi.
Kitandula ameongeza kuwa suala hilo liliundiwa kamati ya wataalamu iliyotarajiwa kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu mustakabali wa biashara hiyo. Hivyo, akaomba kwa sasa mbunge huyo awape fursa zaidi kwani jambo hilo linafanyiwa kazi.
Mwaka 2016 Serikali iliweka zuio la kuuza wanyama hai nje ya nchi ambapo liliathiri pia wafugaji wa vipepeo ambao soko lake lipo nje. Hadi zuio linawekwa kulikuwa na kaya zaidi 360 katika vijiji vilivyopo milima ya Amani na Usambara, na Kaskazini Unguja waliokuwa wanajishughulisha na ufugaji wa vipepeo.
Ufugaji wa vipepeo ulikuwa ukiwaingizia kipato wafugaji wastani wa shilingi 300,000 kwa mwezi. Kufuatia zuio hilo baadhi ya wafugaji hususani kutoka Zanzibar waliamua kuyageuza mashamba ya vipepeo kuwa vivutio vya utalii.
Peter Msigwa akata rufaa kupinga ushindi wa Sugu Nyasa
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, na kushindwa katika uchaguzi uliompa ushindi Joseph Mbilinyi (Sugu) ametangaza kuwa ameukatia rufaa ushindi huo akidai kwamba haukuwa halali kwani kulikuwa na mbinu chafu dhidi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 3, 2024, nyumbani kwake huko mkoani Iringa, Msigwa amedai kuwa kwenye uchaguzi huko kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi lakini pia baadhi ya wapiga kura walizuiwa kushiriki bila sababu yoyote.
CHADEMA kwa sasa ipo katika mchakato wa uchaguzi ambao ulianzia kwenye ngazi za chini na hivi sasa upo katika ngazi ya kanda. Kwenye uchaguzi huo imeshuhudiwa baadhi ya wagombea wakijitoa kwenye hatua za mwisho huku madai ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa nayo yakitamalaki.