Search
Close this search box.

Benki ya Dunia yazindua ripoti yake ya 20 kuhusu hali ya uchumi nchini

Leo Jumanne ya Machi 12, 2024, Benki ya Dunia imezindua rasmi ripoti yake ya 20 kuhusu hali ya uchumi nchini, uzinduzi ambao umefanyika katika hoteli ya Hyatt Regency iliyopo Posta, jijini Dar es Salaam. 

Ripoti hiyo imebeba ujumbe wa kuitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa inapambana na suala la ongezeko kubwa la idadi ya watu, huku ikihakikisha inatengeneza fursa zitakazowaondoa Watanzania kwenye dimbi la umaskini. 

Ujumbe huo umetolewa mara baada ya utafiti wa ripoti hiyo kuonesha kuwa idadi ya watu nchini itaongezeaka maradufu kila baada ya miaka 23. Hali hiyo itatokana na uwepo wa kiwango cha juu cha uzazi na kupelekea hadi kufikia mwaka 2050 Tanzania kuwa na watu milioni 140. 

Ongezeko hilo kubwa limeelezwa kuwa litapelekea uwepo uhitaji mkubwa wa huduma za kijamii na ajira. Hivyo Benki ya Dunia imependekeza kuwa Serikali ya Tanzania ione haja kuja na sera za kukabiliana na suala hilo. 

Bandari ya Mtwara yapokea mitambo mipya kuboresha utendaji kazi

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) leo Machi 12, 2024, imekabidhi mitambo inayojulikana kama ‘hubour crane’ kwenye bandari ya Mtwara kwa ajili ya kuwezesha shughuli za kupakia na kushusha shehena kwenye meli. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi mitambo hiyo Nicodemus Mushi ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, ameeleza kuwa mitambo mipya inatarajiwa  kuiwezesha bandari hiyo kufanya kazi kwa mwaka mzima na kwa ufanisi mkubwa. 

Kwa mujibu wa taarifa ya TPA kwa mwaka 2023/2024 hadi kufikia Januari mwaka huu,  bandari ya Mtwara imehudumia shehena ya tani 1,016, 296. 

Bidhaa ambazo zinahudumiwa ni pamoja na makaa ya mawe yanayochangia zaidi ya asilimia 80 ya shehena inayopita katika bandari ya Mtwara. Shehena nyiginyine ni korosho, saruji, mafuta na shehena mchanganyiko.

UNICEF kusaidia utekelezaji wa mageuzi katika sekta ya elimu Tanzania

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika utekelezaji wa mageuzi kwenye sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu bora.

Hayo yameelezwa leo Machi 12, 2024, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika wa shirika hilo Etleva Kadili, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda.

Kadili amesema kuwa wanatambua juhudi kubwa ambazo zimefanyika na hivyo ni lazima ziungwe mkono ili kufikia malengo. Hivyo UNICEF itaendelea kusaidia katika mafunzo ya walimu na kutekeleza afua zitazowezesha kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Kwa upande wake Prof Mkenda amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kufanya tafiti zitakazoangali suala la mdondoko wa wanafunzi ili kuweza kubaini sababu na kuzipatia utatuzi ili kuondoa changamoto hiyo.