The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Duru ya kwanza ya utoaji wa vitalu kwa kampuni za utafutaji wa mafuta na gesi yazinduliwa Zanzibar

Leo Machi 20, 2024, Serikali ya Zanzibar imezindua duru ya kwanza ya utoaji wa vitalu kwa kampuni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa maeneo ya baharini. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip, Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, amesema kuwa Serikali inazipa mwaliko kampuni zote za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi kushiriki katika duru hiyo ya kwanza. 

Kiongozi huyo wa Zanzibar amewakikishia wawekezaji wote wa sekta ya mafuta na gesi kuwa Serikali itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kuwa dhamira yake katika uchumi wa buluu ni kuimarisha uchumi wa nchi na kuhakikisha upatikanaji wa maendeleo endelevu ya vyanzo vya nishati ya uhakika.

Shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa upande wa Zanzibar zilianza miaka ya 1950 na kukamilika mwaka 1963. Baada ya mapinduzi ya Zanzibar, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi zilikuwa chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania.

Tangu mwaka 1964, tafiti mbalimbali zimefanyika kwa upande wa nchi kavu na baharini mwa Zanzibar na kupelekea kupatikana kwa vitalu vyenye viashiria vya kuwa na mafuta na gesi asilia.  

Vijana zaidi ya 100 wa mradi wa BBT wadaiwa kuondoka kambini

Leo Machi 20, 2024, The Chanzo tumechapisha habari kuhusu vijana zaidi ya 100 wa Programu ya Kuwezesha Ushiriki wa Vijana Katika Kilimo Biashara (BBT- YIA) waonadaiwa kuondoka katika kambi ya Chinangali, jijini Dodoma, wakidai hakuna mwelekeo kambini hapo, huku wakiishutumu Serikali kwa kushindwa kwake kutimiza ahadi ilizotangaza awali.

Kwa mujibu wa taarifa ilizozifikia The Chanzo, mpaka kufikia jioni ya Machi 19, 2024, vijana waliokuwepo kambini hapo ni kati ya 120 na 128 kutoka vijana 268. 

The Chanzo ilimuuliza Vumilia Zinkankuba, Mratibu wa Programu ya BBT, endapo kama taarifa za vijana kuondoka kambini hapo zina ukweli wowote, ambapo aliomba apewe kwanza chanzo cha taarifa hiyo ndiyo ajibu kama ni za kweli au la.

Taarifa za vijana hao kuondoka kambini Chinangali zinakuja takribani wiki moja baada ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuelezea kuwa Serikali imekuwa ikifanya mazuri mengi kwa vijana hao ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba, kuwalipa posho na kuwaandalia mashamba mazuri yenye miundombinu rafiki kwa kilimo. 

Unaweza kuitembelea The Chanzo kwa ajili ya kuisoma habari hii kwa undani zaidi.

Serikali yatetea uamuzi wake wa kuitaka DART itafute mwekezaji binafsi 

Serikali imesema kuwa uamuzi wa kumtaka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) atafute mwekezaji binafsi ili kuunusuru mradi huo utakwenda kuongeza ufanisi wa kutoa huduma, kwani mwekezaji atakayepatikana atalazimika kulipa kodi na kuwajibika endapo atashindwa kutoa huduma. 

Hayo yameelezwa leo Machi 20, 2024, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa, mara baada ya juzi Machi 18, 2024, kutoa taarifa ya kuwataka DART kuwa hadi kufikia Oktoba mwaka huu wawe wamepata mwekezaji binafsi. 

Mradi wa mwendokasi ulianza kufanya kazi mwaka 2016. Katika siku za hivi karibuni, mradi huo umekuwa ukidaiwa kushindwa kuwahudumia ipasavyo wakazi wa jiji lenye watu wengi zaidi la Dar es Salaam, hali ambayo imekuwa ikipelekea usumbufu mkubwa. 

Mpaka mwezi Oktoba mwaka jana mradi huo ulikuwa una mabasi 210, lakini kati ya hayo, mabasi 140 pekee ndiyo yanayotoa huduma.