The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hoja nne zabaki kuwa kero kwenye muungano 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jafo, amesema kuwa kero nne ambazo zimebaki kwenye muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar unaofikisha miaka 60 mwaka huu zinaendelea kupatiwa ufumbuzi. 

Hayo yameelezwa leo Machi 26, 2024, jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kueleza mafanikio ya wizara yake, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya muungano.

Jafo ametaja kero zilizobaki kuwa ni suala la mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, mgawanyo wa faida kutoka Benki Kuu, suala zima la uingizwaji wa sukari inayozalishwa katika kiwanda cha Mahonda, Zanzibar katika soko la Tanzania Bara pamoja na usajili wa vyombo vya moto.  

Aidha, amefafanua kuwa kero zote hizo kwa sasa zinatafutiwa ufumbuzi na kwamba katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ufanisi umekuwa mkubwa kwa sababu zaidi ya nusu ya kero za muungano zimetatuliwa katika kipindi hiki.

Ndege mpya aina Boeing B 737-9 Max yawasili nchini  

Ndege mpya aina ya Boeing B 737-9 Max ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) yenye uwezo wa kubeba abiria 181 imewasili nchini leo Machi 26, 2024, ikitokea nchini Marekani ilikotengenezwa. 

Kuongezeka kwa ndege hiyo kunalifanya shirika hilo liwe na jumla ya ndege 14 ambapo, kati ya ndege hizo moja ni ya mizigo na zinazobakia ni za abiria.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kuwa uwepo wa huduma za uhakika za usafiri na usafirishaji ni msingi katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.

Hivyo, Serikali ya awamu ya sita kwa kutambua umuhimu wa sekta ya uchukuzi kwenye ukuaji wa uchumi, imeendeleza yale yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano kwa kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha sekta hiyo, ili iendelee kuwa injini ya uchumi wa taifa.

Waandishi wa habari wawili wafariki kwa ajali ya gari 

Waandishi wa habari wawili wa mkoa wa Lindi wamefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea leo Machi 26, 2024, saa saba usiku katika eneo la Nyamwage mkoani Pwani. 

Waandishi hao ni Josephine Kibiriti wa kampuni ya Sahara Media Group na Abdalah Nanda wa Channel Ten. Ambapo, walikuwa wakitokea Dar es Salaam kwenye semina iliyoandaaliwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP).

Kamanda wa polisi wa mkoa wa kipolisi Rufiji, Protas Mutayoba, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni gari walilokuwa wakisafiria kugongana na lori.