The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Rais Samia apokea Ripoti za CAG, TAKUKURU

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Salum Rashid Hamduni,  leo Machi 28, 2024, wamewasilisha ripoti zao za utendaji kazi kwa mwaka 2022/2023 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, zoezi ambalo limefanyika katika Ikulu ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma.

Akiwasilisha ripoti yake, Kichere amesema katika mwaka huo ametoa jumla ya hati 1,209 za ukaguzi. Kati ya hati hizo, zinazoridhisha ni hati 1197, sawa na asilimia 99. Hati zenye shaka ni tisa, sawa na asilimia 0.7. Hati mbaya ni moja, sawa na asilimia 0.1, pamoja na hati nyingine mbili ambazo CAG alishindwa kutoa maoni.

Kichere pia ameyataja mashirika ya umma kadhaa yaliyotengeza hasara, akitaka hatua zichukulie ili hali hiyo isijirudie. Mashirika hayo ni kama vile Shirika la Ndege (ATCL), Shirika la Mawasiliano (TTCL), Shirika la Reli (TRC), Kampuni Tanzu ya Mafuta (TanOil ) na Shirika la Posta.

Kwa upande wake, Hamduni ameeleza kuwa TAKUKURU katika kutekeleza jukumu la uzuiaji wa rushwa ilifanya ufatiliaji wa rasilimali za umma katika miradi ya maendeleo 1,800 yenye thamani ya Shilingi trilioni 7.7. Kati ya hiyo, miradi 171, yenye thamani ya Shilingi bilioni 143.3, ilibainika kuwa na utekelezaji hafifu na hivyo kuanzisha uchunguzi.

Akizungumza mara baada ya kupokea ripoti hizo, Rais Samia alisema kuwa ripoti hizo zinasaidia kupunguza hasara kwa kuwa mashirika na taasisi za Serikali hujifanyia tathmini na kurekebisha mapungufu mara baada ya kupewa dosari zilizobainika.

LHRC: Usalama wa wakili Joseph Oleshangay upo hatarini

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, ameuambia umma wa Watanzania na jumuiya za kimataifa kuwa usalama wa wa mfanyakazi wa LHRC na mtetezi wa haki za binadamu, Joseph Oleshangay, upo hatarini kutokana na kufuatiliwa na watu wasiofahamika.

Henga alitoa taarifa hiyo leo Machi 28, 2024, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za LHRC zilizopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Oleshangay, anayefanya kazi katika ofisi za LHRC za jijiji Arusha, amekuwa akitoa msaada wa kisheria kwa jamii yake ya Wamasai wanaopatikana ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Inadaiwa kuwa kuanzia Machi 15, 2024, hadi Machi 18, 2024, watu wanaodaiwa kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi waliweka kambi nyumbani kwa Oleshangay, wakisema wanamuhitaji mwanaharakati huyo, bila kusema kwa nini. 

Siku chache kabla ya kuanza kutafutwa ulisambazwa ujumbe kwenye mitandao ya kijamii ukiitaka Serikali imchukulie hatua Oleshangay, ukisema yeye ni mtu hatari.  

Henga alisema kuwa usalama wa Oleshangay ni kipaumbele cha juu cha LHRC, akiongeza kwamba shirika hilo linafuatilia kwa karibu taarifa hizo, na kwamba watafanya lolote linalowezekana kuhakikisha usalama wa mfanyakazi wao.

Ibada maalum kufanyika April 12, 2024, kumuombea hayati Edward Sokoine

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhudhuria ibada ya kumuombea aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine, tukio ambalo litafanyika Aprili 12, 2024, katika kijiji cha Enguik, Monduli Juu, mkoani Arusha.

Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 28, 2024, na Msemaji wa Familia ya Hayati Sokoine, Lembris Marangushi, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha kiongozi huyo.

Marangushi alimuelezea Sokoine kama kiongozi mzalendo aliyelipenda taifa la Tanzania na wananchi wake, akihakikisha rasilimali za taifa hilo zinatumika kwa manufaa ya Watanzania wote. Marangushi alisema Sokoine aliwatumikia wananchi bila kuwabagua, lakini pia alikuwa na hofu ya Mungu sana katika kufanya kazi zake.

Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania katika vipindi viwili Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984. Aliwahi pia kuwa Waziri wa Ulinzi kati ya mwaka 1972 hadi 1977 na Waziri Mdogo wa Mawasiliano, Uchukuzi na Kazi kati ya mwaka 1967 hadi 1972.