The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kimbunga HIDAYA kuisogelea pwani ya Tanzania  

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kimbunga Hidaya kusogea karibu kabisa na Pwani ya Tanzania kuanzia usiku wa leo, Mei 2, 2024, na kitaendelea kuwepo hadi Mei 6, 2024.  

Taarifa ya TMA iliyotolewa leo Mei 2, 2024, imeeleza kuwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba yanaweza kuathirika na hali hiyo, kwa kukubwa na vipindi vya mvua na upepo mkali.  

TMA imeshauri wananchi katika maeneo tajwa wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari kubwa ili kujiepusha na madhara yanayoweza kuletwa na kimbunga hicho.  

Mauzo ya nje ya mazao ya chakula yafikia dola bilioni 2.3

Serikali imesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 mauzo ya mazao ya chakula nje ya nchi yamefikia dola za Kimarekani bilioni 2.3, ikilinganishwa dola za Kimarekani bilioni 1.2 zilizopatikana mwaka 2019/2020.  

Hayo yamesemwa leo Mei 2, 2024, bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2024/2025.  

Bashe ameongeza kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa mwaka 2022/2023 ulifika tani milioni 20.4, ikilinganishwa na tani milioni 17.1 zilizopatikana msimu wa mwaka 2021/2022, ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 19. 

Aidha, amesema uzalishaji wa mazao ya nafaka ulikua kwa asilimia 11.6  na yasiyo ya nafaka uliongeza kwa asilimia 8.9, hali ambayo ilifanya utoshelevu chakula nchini kufikia asilimia 120 ukilinganisha na utoshelevu wa asilimia 114 uliokuwepo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.  

Sekta ya kilimo imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa uchumi kwa kuchangia kiasi kikubwa kwenye pato la taifa na kutoa ajira kwa wananchi wengi. Kwa mwaka 2023 sekta hiyo ilichangia asilimia 26.5 kwenye pato la taifa na ikatoa ajira kwa asilimia 65.6 huku ikiwa imechangia asilimia 65 ya malighafi zote za viwanda.

Sheria ya Sukari kufanyiwa marekebisho kuwawezesha NFRA kununua na kuhifadhi sukari

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema kuwa Serikali inapanga kufanya marekebisho katika Sheria ya Sukari namba sita ya mwaka 2001 kwenye sheria ya fedha ya mwaka 2024, ili kumuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua na kuhifadhi sukari kwenye hifadhi ya taifa ya chakula. 

Mpango huo umeelezwa kuwa utaenda pamoja na marekebisho ya kanuni za NFRA yatakayoiweka sukari iwe sehemu ya usalama wa chakula. 

Hayo yamesemwa leo Mei 02, 2024, bungeni jijini Dodoma, wakati Bashe alipokuwa akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka 2024/2025.  

Mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu Tanzania ilishuhudia upungufu mkubwa wa sukari, hali ambayo ilipelekea bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ya juu. 

Wananchi walilazimika kununua kilo moja ya bidhaa hiyo kwa Shilingi 4,000 hadi 5,000 kutoka Shilingi 2,800 hadi Shilingi 3,000 iliyokuwa imezoeleka. 

Ili kutatua tatizo hili, Serikali ililazimika kutoa vibali kwa wafanyabiashara ili waagize sukari tani 50,000 kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kupambana na upungufu uliokuwepo.