The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Makonda ajibu mapigo sakata la udhalilishaji wa mtumishi wa kike

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema kuwa ataendelea ‘kuwapiga spana’ watumishi wa Serikali anaowaona kuwa wanakwamisha miradi ya maendeleo huku akiwaonya wale wanaowatetea kwa kile alichodai kuwa nao ni sehemu ya kundi hilo.

Makonda ametoa kauli hii leo Mei 27, 2024,  wilayani Monduli, wakati alipokuwa kwenye muendelezo wa ziara yake ya siku sita katika halmashauri za mkoa huo. 

Utetezi huu wa Makonda unakuja siku chache tangu Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jumuiya ya Wanawake CCM, pamoja na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), walipotoa matamko yao ya kumkemea kiongozi huyo.

Wadau hawa kwa pamoja walikuwa wanalaani kitendo chake kilichoelezwa kuwa ni cha kumdhalilisha mtendaji wa kike wa Serikali toka halmashauri ya Longido na walimtaka   kuomba radhi kwa kutweza utu wa mwanamke.

Wakurugenzi watakiwa kuwasilisha Serikalini madeni ya watumishi kwa ajili ya malipo

Serikali imewataka waajiri wote nchini hasa wakurugenzi wa halmashauri kuhakiki na kuwasilisha madeni ya watumishi wao kwa ajili ya taratibu za uhakiki na kuendeleza mchakato wa malipo wa madeni hayo. 

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Mei 27, 2024, na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi, Neema William Mgaya, aliyehoji ni lini Serikali itamaliza kulipa madeni ya muda mrefu ya watumishi.

Kikwete ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti uzalishaji wa madeni ya watumishi ikiwemo malimbikizo ya mishahara kwa kujenga Mfumo Mpya wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ambao umeweza kudhibiti uzalishaji wa malimbikizo mapya ya mishahara.

Aidha, ameongeza kuwa  pamoja na hatua hiyo, kuanzia mwezi Mei 2021 hadi sasa Serikali imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 132,611 yenye thamani ya Shilingi 219,732,820,025.74.

Serikali yasema watoto watatibiwa bila vikwazo baada ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote kuanza

Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel, amesema kuwa kuanza kwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kutawezesha watoto kupata huduma za afya kwa urahisi pasipo kuwa na vikwazo. 

Kauli hiyo ameitoa leo Mei 27, 2024, bungeni, jijini Dodoma, wakati alipokuwa akijibu swali la mbunge viti maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi, Rehema Migilla, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwasaidia watoto kupata matibabu baada ya kufutwa kwa bima ya toto afya kadi. 

Mollel ameongeza kuwa kwa sasa watoto wanajiunga na bima ya afya kupitia utaratibu wa shule na vifurushi vya bima ya afya vya najali, wekeza na timiza ambapo wanajiunga kupitia wazao wao. 

Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ulipitishwa na Bunge Novemba 1, 2023, na Rais Samia Suluhu Hassan aliidhinisha iwe sheria rasmi Disemba 5, 2023. 

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alieleza kuwa kwa mwaka huu Serikali itatenga Shilingi bilioni sita kwa ajili ya kutekeleza afua sita ikiwemo ya bima ya afya kwa wote kwa kuanzisha mchakato wa mfumo wa utambuzi na elimu.