Tanzania kupata mkopo wa Shilingi trilioni 6.5 kutoka Serikali ya Korea Kusini
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema Serikali itaingia mkataba wa msaada na mkopo nafuu wa dola za Kimarekani bilioni 2.5 sawa na takribani Shilingi trilioni 6.5 kutoka Serikali ya Korea Kusini.
Taarifa hii imetolewa leo Mei 29, 2024, wakati Makamba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, huko nchini Korea Kusini, ziara ambayo inatarajiwa kuanza kesho Mei 30, 2024 hadi Juni 6, 2024.
Aidha, ameeleza kuwa jumla ya mikataba saba itasainiwa na Rais Samia atapokuwa nchini humo ambapo ameitaja mikataba hiyo kuwa ni hati ya makubaliano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Sayansi na Miamba na Madini ya Korea, ushirikiano utakaojikita katika utafiti, uchoraji ramani, rasilimali na shughuli za maabara.
Mingine ni pamoja na mkataba wa ushirikiano katika maendeleo ya uchumi wa buluu, kutambua vyeti ya mabaharia, tamko la pamoja la uanzishwaji wa majadiliano kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi, mkataba wa makubaliano kati ya Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) na Shirika la Ukarabati wa Migodi na Rasilimali za Madini la Korea.
Shilingi bilioni 986 zinahitajika kushughulikia madhara ya mvua za El-Nino
Jumla ya Shilingi bilioni 986 zinahitajika kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu mbalimbali iliyoathiriwa na mvua za El-Nino zilizonyesha kuanzia Septemba 2023 na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na madaraja nchini.
Hayo yamesemwa leo Mei 29, 2024, bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Bashungwa ameeleza kuwa hadi Mei 2024 jumla ya Shilingi bilioni 72 zilitolewa na Hazina kwa ajili ya kazi za matengenezo ya dharura.
Akizungumzia uharibifu uliotokea katika barabara ya Mtwara, Lindi hadi Dar es Salaam, Bashungwa amesema kuwa uharibifu uliotokea ni mkubwa sana kiasi kwamba barabara yote hiyo inatakiwa kujengwa upya licha ya kuwa Serikali imechukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa mawasiliano katika barabara hiyo yanarejea.
Serikali yaiagiza TCRA kuingilia kati sakata la bei za vocha kupandishwa kiholela
Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuatilia wafanyabiashara wanaouza vocha za kukwangua kinyume na bei elekezi na kuhakikisha kuwa hawapandishi bei kiholela pasipo kufuata taratibu.
Kauli hiyo imetolewa na leo Mei 29, 2024, na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalumu kupitia CHADEMA, Tunza Malapo, aliyehoji kuhusu baadhi ya wafanyabiashara kuongeza bei za vocha za kukwangua, ambapo vocha ya Shilingi 1,000 inauzwa Shilingi 1,200 na vocha ya Shilingi 500 inauzwa Shilingi 600.
Naibu Waziri Mahundi, akaongeza kuwa taarifa hizo zimejitokeza maeneo mbalimbali nchini ikiwepo Tunduma, Mbozi na Songwe. Hivyo, TCRA imepewa maagizo kufuatilia jambo hilo na kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata utaratibu uliowekwa.
Januari 10, 2023, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) lilipiga marufuku upandaji bei ya vocha za simu kiholela baada ya kudai kuwa kitendo hicho ni batili na ni kinyume cha sheria.